Waganga Wa Tiba Asili Waigomea Serikali Kuzuia Kujitangaza........Wasema Dr. Kingwangalla Anatafuta Sifa, Waonya Matumizi Mabaya Ya 'Hapa Kazi Tu' - LEKULE

Breaking

28 Dec 2015

Waganga Wa Tiba Asili Waigomea Serikali Kuzuia Kujitangaza........Wasema Dr. Kingwangalla Anatafuta Sifa, Waonya Matumizi Mabaya Ya 'Hapa Kazi Tu'


Waganga wa Tiba Asili Nchini wamepinga tamko la Serikali lenye maagizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku waganga hao kujitangaza katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
 
Waganga hao wamefikia uamuzi wa kupinga agizo hilo la serikali kwa madai kwamba agizo hilo halikushirikisha wadau wote na halikuzingatia sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala

Wakizungumza kwenye mkutano ulifanyika jana kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam waganga hao kwa pamoja walisema agizo la serikali linaonesha ni kiasi gani wanadharaulika na serikali haijali mchango wao katika jamii na taifa.

Aidha, waganga hao walisema kwamba uwepo wao hapa nchini unalindwa na sheria zilizopo hivyo uamuzi wowote dhidi yao ulipaswa kutangazwa tofauti na ilivyofanya serikali kwa kuwaagiza kupitia vyombo vya habari.

Miongoni mwa wajumbe wa mkutano huo na mdau wa tiba asili Boniventure Mwalongo alisema wao kama waganga wa tiba asili na tiba mbadala hawakubaliani na agizo hilo la serikali kwa kuwa hawakushirikishwa

Naye Mkurugenzi wa Ulcers Clinic Tabibu Rahabu Rubago alieleza jinsi alivyosikitishwa na taarifa za agizo la serikali linalowapiga marufuku kujitangaza hali iliyomsababishia kulazwa hospitalini akidai kwamba wakati anasikia taarifa hiyo alikuwa tayari ametoka kulipia matangazo yake ya mwaka mzima katika kituo cha Star Tv.

Mkurugenzi wa Ulcers Clinic Tabibu Rahabu Rubago akizungumza kwenye mkutano huo alipopata nafasi kuchangia
Tabibu Rahabu Rubago aliendelea kusema kwamba “ Huku ni kurudishana nyuma kimaendeleo ..sielewi ni kwanini serikali inatupiga marufuku. Agizo hili halituumizi sisi watoa huduma pekee bali hata wananchi wake kwa ujumla”

Mbali na hayo, Tabibu Rahabu Rubago alisema kwamba “ mimi nadhani kama kuna eneo tunakwenda kinyume ni vyema serikali ingetuita na kutuambia kupitia mabaraza yetu ili turekebishe eneo hilo lakini hii ya kupiga marufuku tu kijumlajumla kwa kweli haiko sawa”


Pamoja na hayo katika kikao hicho wadau hao wa tiba asili kwa nyakati tofauti walionekana kutupa lawama zao kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jami, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Khamis Kigwangalla huku wakisema kuwa amedandia suala hilo kwa ajili ya kujitafutia umaarufu kisiasa na kuitumia vibaya kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano ya ‘Hapa Kazi Tu’

Haya yote yanafuatiwa na taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na Wizara ya Afya yenye agizo linalowataka waganga wote wa tiba asili wenye vibali vya kutoa huduma hiyo kuwasilisha vibali hivyo katika Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kwa ajili ya kuvipitia upya vibali hivyo.

Katika agizo hilo  serikali imetoa siku 14 kwa watoa huduma wa Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini kuwa wamewasilisha nyaraka zao zote zinazowaruhusu kutoa huduma hiyo na ziwasilishwe kwenye baraza hilo.

Agizo hili lilikuja siku chache baada ya  Naibu Waziri wa Afya Dk Kigwangalla, Desemba 14, mwaka huu kufanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha Tabibu Juma Mwaka jijini Dar es Salaam 

No comments: