Leticia Nyerere Mahututi Marekani......Apumulia Mashine, Familia Yaanza Kujipanga - LEKULE

Breaking

28 Dec 2015

Leticia Nyerere Mahututi Marekani......Apumulia Mashine, Familia Yaanza Kujipanga



HALI ya afya ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Leticia Nyerere si nzuri.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, Leticia amelazwa katika Hospitali ya Doctors Community iliyopo Maryland nchini Marekani.

Chanzo hicho kimeeleza kuwa mwanasiasa huyo amelazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU), ingawa haijafahamika anasumbuliwa na tatizo gani.

Tangu juzi usiku, kumekuwapo na taarifa nyingi kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii zinazodai kuwa Leticia amefariki dunia, jambo ambalo si kweli.

Habari za uhakika ambazo zimepatikana kutoka kwa mmoja wa wanafamilia ya Nyerere  ni kwamba Leticia yupo hai ingawa anaumwa.

“Hali ya Leticia si nzuri yuko ICU nchini Marekani, kwa muda mrefu sasa amekuwa akiumwa. Tumejaribu kuwasiliana na mmoja wa watoto wake kule Marekani, ametwambia hali si ya kuridhisha kabisa.

“…tunamwombea Mungu ampe  nguvu ili arudi katika hali ya kawaida. Tumeshangazwa na uvumi wa taarifa hizi kwenye mitandao ya kijamii kuwa amefariki dunia, jamani hebu tuwe na subiri ya kuwaombea  wenzetu wanapokuwa kwenye matatizo na si kukimbilia kusema fulani kafa,” alisema mwanafamilia huyo.

Leticia aliolewa kisha kutengana na mtoto wa Hayati Baba wa Taifa, Madaraka Nyerere mwaka 1996, ambapo walifanikiwa kupata watoto watatu.

Jana Msemaji wa Familia ya Mageni Msobi, John Shibuda, alikiri kuugua kwa mbunge huyo wa zamani, huku akisita kueleza ugonjwa unaomsumbua.

“Ni kweli Leticia anaumwa na amelazwa Marekani na hali yake si nzuri, kwa sasa tunawasiliana na madaktari pamoja na wanafamilia walioko huko kwa ukaribu zaidi.

“Siwezi kusema ugonjwa kwa sasa kwani suala hilo ni siri kati ya mgonjwa na daktari wake ila sisi kama familia tutaeleza kwa kina wakati utakapofika,” alisema Shibuda.

Julai 27 mwaka huu, Leticia  alitangaza kuihama Chadema  na kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akitangaza uamuzi wake, Leticia alisema aliamua kuihama CCM baada ya kutoridhishwa na baadhi ya mambo wakati huo. Hata hivyo alikiri kuwa alikurupuka katika kufikia uamuzi huo.


“Moyo wangu umekuwa ukisononeka kutokana na kukaa Chadema na kuacha kukaa katika chama kilichonilea na kunisomesha nje ya nchi, sasa nasema narudi nyumbani kukitumikia chama changu,” alisema.

No comments: