Wafanyakazi
wawili wa Tanesco na raia wawili wa China wamefikishwa katika mahakama
ya hakimu mkazi mkoa wa Kagera kwa tuhuma za kutenda makosa kumi na
sita na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi bilioni moja.
Watuhumiwa
kutoka Tanesco Isaack Tibita na Olver Mushumbusi kwa nyakati tofauti
walikuwa mameneja Wilayani Karagwe wanadaiwa kushirikiana na wafanyakazi
wa kampuni ya ujenzi wa barabara ya Chico kufanya udanganyifu na
kujipatia fedha hizo.
Raia
wa China katika kesi hiyo ni Wang Lei na Zhang Shuaitong ambao kwa
pamoja wanadaiwa kutenda makosa 16 wakati wa kuhamisha miundombinu ya
umeme zikiwemo nguzo ili kupisha ujenzi wa barabara ya lami ya
Kyaka,Bugene.
Katika
kesi hiyo namba 65 ya mwaka 2015 Wakili Mfawidhi kutoka ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hashimu Ngole alisema watuhumiwa kati ya
mwaka 2011 na 2014 kwa nyakati tofauti walitenda makosa hayo na
kusababisha hasara ya kiasi hicho cha fedha.
Miongoni
mwa makosa waliyosomewa washitakiwa ni kughushi nyaraka zikiwemo hundi
za malipo zinazonyesha kuwa kampuni ya Chico imelipwa fedha kupitia
mradi wa ujenzi wa barabara ya lami ya Kyaka Bugene.
Mtuhumiwa
wa tatu ambaye ni raia wa China Wang Lei alikuwa meneja wa mradi huo
na alisomewa mashitaka mawili peke yake huku mtuhumiwa wa nne Zhang
Shuaitong akifanya tafsili kutokana na raia mwenzake kufahamu lugha ya
Kichina pekee.
Pia
wafanyakazi hao wa Tanesco miongoni mwa mashitaka mengine
yanayowakabili ni kughushi nyaraka zilizoonyesha kuwa shirika hilo
lilikuwa linadai kulipwa na kampuni ya Chico na kuwa kwa nyakati tofauti
walipokea fedha kutokana na nyadhifa zao.
Watuhumiwa
wote walikosa dhamana baada ya hakimu Charles Uiso kusema kuwa hakimu
anayehusika na kesi hiyo alikuwa na majukumu mengine na itatajwa tena
Desemba 7,na kupewa masharti ya dhamana.
No comments:
Post a Comment