TAASISI isiyo ya kiserikali ya HakiElimu leo imezindua ripoti iliyobainisha madudu yaliyofanywa katika utawala wa Awamu ya Nne chini ya Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.
Ndani
ya ripoti hiyo iliyobeba miaka 10 ya utawala wa Rais Kikwete sekta ya
elimu, imeeleza kuwa katika uongozi wake, ubora wa kiwango cha elimu
uliporomoka kuliko wakati mwingine wowote katika histolia ya Tanzania.
Katika
ripoti hiyo ambayo iliandaliwa na jopo la wataalamu na wadau wa elimu
mbalimbali ambao walifanya katika mwezi Julai na Agosti mwaka huu, pia
imebaini utekelezaji hafifu wa ahadi zake alizokuwa akizitoa kwenye sera
zake kuhusu uboreshaji wa sekta ya elimu.
Akichambua
ripoti hiyo baada ya kuzinduliwa na Mwenyekiti wa Bodi HakiElimu,
Martha Qorro, Mhadhili wa Chuo Kikuu Dar es Salaam Prof. Kitila Mkumbo
amesema, katika utafiti huo pia walibaini kuwa, Rais Kikwete hakuongeza
vitu vipya katika uongozi wake kuhusu sekta ya elimu bali aliendeleza
yale aliyoachwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
“Hakuwa
na falsafa mpya katika sekta ya elimu bali alichokuwa anafanya ni
kuyabeba kila anayoyapata kama yalivyo na kuanza kufanyia kazi.
“Mfano;
alisema ataanzisha shule za kimataifa nchini lakini hizo hizo
alizoziongeza ndio zipo hoi, hadi sasa shule zenye viwango
vinavyokubalika nchini ni asilimia nne tu,” amesema Mkumbo.
Mkumbo
amesema, alichofanikiwa Rais Kikwete katika uongozi wake ni kupanua
fursa za elimu ambapo aliweza kuongeza miundombinu kwa kuongeza
madarasa, matundu ya vyoo, kuongeza idadi ya walimu, vitabu, udahili,
uwiano kati ya wasichana na wavulana wanaojiunga na shule ya msingi na
sekondari lakini sio katika suala la ubora wa elimu.
“Mathalani,
shule za msingi zimeongezeka kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi 16,538 mwaka
2015 huku wanafunzi wa shule za msingi wakiongezeka kutoka 7,541,208
hadi 8,202,892, shule za sekondari zimeongezeka kutoka 1,745 mwaka 2005
hadi 4,753 mwaka 2015 huku idadi ya wanafunzi shule za sekondari
zikiongezeka 524,325 mwaka 2001 hadi 1,804,056 mwaka 2015.
“Vyuo
vya ufundi pia vimeongezeka kutoka 184 mwaka 2005 hadi 744 mwaka 2015
huku idadi ya wanafunzi katika vyuo ikiongezeka kutoka 40,059 hadi
145,511 mwaka 2015. Licha ya wanafunzi kuonekana kuwa wengi shuleni na
vyuoni, tafiti mbalimbali zilizofanyika zinaonesha wanafunzi wengi
hawajui kusoma wala kuandika,” amesema Mkumbo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa HakiElimu, John Kalage akisoma mapendekezo yaliyopo kwenye
ripoti hiyo amesema kuwa, serikali iliyopo madarakani hivi sasa
inatakiwa kuchukua maoni yaliyopendekezwa kwenye ripoti hiyo na
kuyafanyia kazi ili kuboresha sekta ya elimu nchini.
Akitaja
baadhi ya mapendekezo yaliyomo katika ripoti hiyo Kalage amesema,
serikali ya Awamu ya Tano inatakiwa iwatazeme walimu kwa jicho lingine.
Ili
elimu iwe bora lazima walimu pia wawe bora na sio bora walimu hivyo
iunde bodi ya kuwachunguza walimu labla ya kuanza kazi kama ilivyo kwa
madaktari baada ya kumaliza masomo.
Amesema
mapendekezo mengine ni kuwajali walimu ili wapate moyo wa kufanya kazi
hiyo kwa kuwajengea nyumba kwani ni asilimia 22 tu ya walimu ndio
wamepewa nyumba na kuboresha mioundombinu katika mazingira wanayoishi.
Kuboresha madarasa, vifaa vya kufundishia, ukaguzi kwa walimu na
mazingira ya shule yaimarishwe.
“Ni
kazi ya Rais John Magufuli sasa kuiboresha sekta ya elimu kwani hiyo
ndio sekta muhimu na kubwa kuliko zote na ndiyo yenye bajeti kubwa
kuliko zote lakini utendaji wake ni ziro sasa hiyo bajeti inaendaga
wapi?
“Walimu mishahara haiboreshwi, wanafunzi wengi hawajui kusoma wanamaliza shule kichwani hakuna kitu,” amesema Kalage.
No comments:
Post a Comment