Baadhi
ya wenyeviti toka Halmashauri ya wilaya ya Kishapu wakimsikiliza
mkufunzi (hayupo pichani) wakati wa mafunzo yao yaliyofanyika wilayani
hapo.
“Unakuja
kwenye ofisi yangu na kutoa taarifa za ubadhirifu wa mtendaji wa
kijiji. Nakuuliza, je umechukua hatua zipi kama kiongozi wa kijiji kabla
kuja kwenye ofisi yangu? Unanijibu hapana, hii si sahihi,” Hayo ni
maneno ya mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Hashim Mgandilwa, aliyoyatoa
wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wenyeviti wa vijiji, watendaji wa kata
na vijiji kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Loliondo.
Alisema
hayo kwa lengo la kufafanua dhana ya uwajibikaji kwa viongozi kama njia
muhimu ya kutatua kero zinazowakabili wananchi wa maeneo ya vijijini
katika wilaya yake. Ni dhahiri kwamba viongozi wa ngazi za vijiji na
kata wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiutendaji katika maeneo
husika. Kuna nafuu kwa watendaji wa kata na vijiji, ambao ni waajiriwa
wa serikali na hupewa kazi kutokana na miongozo, lakini siyo kwa
wenyeviti wa vijiji na madiwani, wakati mwingine hata wabunge.
Akielezea
changamoto hiyo wakati wa mafunzo ya wenyeviti wa vijiji kupitia mradi
wa Chukua Hatua yaliyofanyika Septemba mwaka huu na shirika mdau la
CABUIPA, mwenyekiti wa kijiji cha Nyakafulu kilichopo wilaya ya Mbogwe,
mkoani Geita, Salum Said amesema: “Baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti
wa kijiji hiki, hakika sikufahamu vya kutosha kuhusu majukumu yangu
mapya kama kiongozi. Na hii ni changamoto kubwa kwa wenyeviti wa vijiji
karibu vyote vya wilaya yetu.”
Yeye
ni mmoja kati ya wenyeviti 200 wanaopatiwa mafunzo katika mikoa ya
Shinyanga, Geita na Simiyu. Wakati wananchi wakiwezeshwa kuwasimamia
viongozi wao, viongozi hawakuwa wakiwezeshwa kutimiza majukumu yao
kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi wao. Hivyo kuna haja ya kutoa
mafunzo kwa viongozi hao ili waweze kutimiza majukumu yao kwa wananchi
waliowachagua, ilikuwa lazima.
Wanakijiji wa Kijiji cha Uchunga wilayani Kishapu wakiendelea na mkutano pamoja na viongozi wa kijiji na wazee Maarufu.
Akielezea
umuhimu wa kuwawezesha wenyeviti wa vijiji wakati wa uzinduzi wa
mafunzo ya wenyeviti na watendaji wa kata Julai 2015, mkurugenzi
mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, Jane
Mutagurwa alisema “Kwa muda mrefu wenyeviti mmekuwa mkilalamika
kusahaulika kwenye programu zetu za mafunzo, fursa ndio hii imekuja.
Tunafahamu
kwamba wenyeviti wetu mnakutana na changamoto nyingi za kiutendaji
zinazotokana na uwelewa mdogo katika majukumu yenu, hasa kwa wale
wanaoingia madarakani kwa mara ya kwanza. Hivyo mtumie mafunzo haya
vizuri.”
Pamoja
na umuhimu wa mafunzo hayo kwa viongozi wa ngazi ya kijiji na kata,
bado imekuwa ni changamoto kubwa kwa serikali kuwawezesha wenyeviti
kujua majukumu yao. Na hii inatokana bajeti kuwa na vipaumbele vingine
ambavyo halmashauri huwa wamejiwekea katika kutimiza majukumu yao."
Kwa
upande wa Ngorongoro, mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya hiyo mkoani
Arusha anaeleza:“Tangu tulipofanya uchaguzi mwaka jana hatujawahi kutoa
mafunzo kwa wenyeviti. Kwa hiyo tunaunga mkono mafunzo haya yanayotolewa
na PALISEP yatasaidia sana kwenye kuwawezesha viongozi hawa na
watendaji wetu,” Kutokana na hali hii, wenyeviti wamekuwa na changamoto
za kuelewa mipaka ya majukumu yao, hivyo muda mwingine hujikuta kwenye
mzozo na watendaji wa vijiji vyao.
Mwenyekiti
anawajibika kwa mwananchi aliyemchagua, wakati mtendaji anawajibika kwa
mkurugenzi aliyemwajiri. Kutokana na tofauti hizo, mafunzo ya sasa ya
wenyeviti na watendaji yanaendeshwa kwa pamoja kuwafanya waelewe mipaka
yao ya kiutendaji, hivyo kuboresha utendaji wao.
Afisa
Programu wa CABUIPA, Michael Ikila anafafanua: “Tunawafundisha vitu sita
muhimu; taratibu za uendeshaji serikali za mitaa, majukumu na haki za
wenyeviti wa vijiji, uwajibikaji na utawala bora, mamlaka za vijiji,
masuala ya fedha, ikiwamo uandaaji wa bajeti na mawasiliano mazuri
baina ya viongozi wa vijiji.”
Mada
hizi ni kwa mujibu wa mwongozo wa wizara ya Tawala za Mikoa and Serikali
za Mitaa (TAMISEMI). Majukumu mengine ya wenyeviti hawa ni pamoja na
kuhamasisha shughuli za maendeleo, utawala na kuhakikisha usalama wa
watu katika maeneo yao kwa kushirikiana na watendaji wa kata na vijiji.
Viongozi wa Kijiji cha Negezi wakiwa pamoja na wanakijiji kujadili mambo mbalimbali ya eneo lao.
Kwa
upande wa Wilaya ya Ngorongoro, hii ni mara ya kwanza kwa wenyeviti
kufundishwa majukumu yao. Mwanzoni mafunzo haya yaliwalenga madiwani
ambao kimsingi hawakuyapenda kwa sababu ya kutokuwapo kwa posho. Hivyo
mafunzo yao yakaamishiwa kwa wenyeviti wa vijiji ambao walipokea mwaliko
kwa furaha pasipo kudai posho. “Mafunzo haya yatatusaidia kuboresha
mahusiano na utendaji wetu.
Mara
kadhaa unakuta wenyeviti wanaingilia mipaka yetu ya kazi, hivyo kuathiri
uhamasishaji wa shughuli za maendeleo. Na hii hutokea pale mwenyekiti
mpya anapotaka kuwaonyesha wapigakura wake kwamba mwenzake aliyepita
hakufanya kazi,” anaelezea mmoja wa watendaji wa kijiji aliyehudhuria
mafunzo hayo.
Pamoja
na changamoto hizo, bado washiriki ambao ni wenyeviti, watendaji wa
kata na vijiji wamekiri kwamba mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kumaliza
tofauti zinazojitokeza baina yao. Lakini si hivyo tu, viongozi wa wilaya
wameonyesha kuunga mkono mafunzo hayo kwa kuwa yanasaidia kuhamasisha
wananchi kutimiza majukumu yao.
Lakini
pia viongozi hao walionyesha umuhimu wa kufikia wajumbe wengi zaidi ya
halmashauri za serikali ya kijiji. Kwa mfano, wakati akizungumza na
wakufunzi kwenye ofisi yake, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya
Kishapu, alisema: Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ina jumla ya vijiji
117 vyenye wajumbe 2,925.
Katika
mazingira hayo, mkurugenzi alitoa ombi maalumu la kusaidiwa kuwawezesha
wakufunzi 25 wa wilaya watakaotoa mafunzo kwa wajumbe wa halmashauri za
vijiji hivyo. Gharama za wakufunzi hawa kuwafikia wajumbe wengine
zitakuwa ni za serikali. Na huu ni ushirikiano unaotakiwa baina ya
sekta ya umma na binafsi kwa kuwa ni jukumu letu sote kwa mustakabali wa
maendeleo yetu.
No comments:
Post a Comment