Na Raymond Mushumbusi- MAELEZO
Kipindupindu
ni ugonjwa wa kuharisha na kutapika unaosababishwa na vimelea vya
bacteria vinavyoitwa kwa lugha ya kitaalam “vibro cholera”. Chanzo cha
kikubwa cha ugonjwa huu huletwa na vimelea vilivyomo kwenye kinyesi na
matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu.
Kwa
miaka mingi sasa wananchi wa Tanzania tumekumbwa na magonjwa ya aina
mbalimbali ya mlipuko ukiwemo ugonjwa wa kipindupindu ambao umeenea kwa
kasi kubwa sana kutokana na kuwepo kwa mazingira hatarishi yanayochochea
mlipuko wa ugonjwa huo.
Kwa
mwaka 2015 ugonjwa wa kipindupindu umetikisa nchi yetu kwa kiasi kikubwa
na kusababisha watu kupoteza uhai na kupunguza nguvu kazi, watoto kuwa
yatima wake kwa waumwe kuwa wajane na wengine kuwapoteza ndugu jamaa na
marafiki zao.
Siyo
mara ya kwanza kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini ila
imekuwa ni tabia ya watanzania kuchukulia mazoea na kuuona ugonjwa huu
kama michezo ya watoto kwenye televisheni ( TV Game) na huku miaka
nenda rudi unazidi kuteketeza watanzania. kwanini watanzania hatulioni
hili kuwa ni janga la kitaifa?
Ugonjwa
wa kipindupindu ulioanza Agosti 15 2015 katika mkoa wa Dar es salaa na
kuenea kwa kasi katika mikoa mingine 20 nchini, kwa mujibu wa taarifa ya
tarehe 15 Desemba 2015 kumekuwa na wagonjwa wapya 141 na kufanya jumla
ya wagonjwa waliokwa wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye vituo vya
kutolea huduma katika mikoa yote iliyoathirika kuwa 184 na vifo vipya
viwili.
Tangu
ugonjwa huu uanze jumla ya watu 11,257 walipata ugonjwa huu na kati yao
177 wamefariki kwa ugonjwa huu ambayo ni sawa na asilimia 1.5 ya
waliougua, mpaka sasa kwa wastani ugonjwa huu umepungua katika mikoa ya
Dar es salaamna kwa mkoa wa Iringa na mji wa Moshi kwa kiasi kikubwa
wamefanikiwa kudhibiti ugonjwa huu.
Katika
tamko la Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto Mhe
Ummy Mwalimua alilolitoa tarehe 16 Desemba 2015 kuhusu mapambano ya
ugonjwa wa kipindupindu, Waziri huyo alipiga marufuku uuzaji wa matunda
yaliyokatwa na vyakula sehemu za wazi(barabarani) na kutoa amri
watakaokiuka wachukuliwe hatua mara moja.
“
Nahitaji nipatate taarifa ya utekelezaji kila siku kutoka kwa Waganga wa
Mikoa na Wilaya na Serikali haitasita kuchukua hatua kwa viongozi ambao
watashindwa kudhibiti ugonjwa huu katika maeneo yao” alisema Waziri
Ummy katika tamko lake kupitia Vyombo vya Habari.
Mara
baada ya kutolewa kwa tamko hilo siku tatu baadae mwandishi wa makala
hii nilifanya ziara ndogo kuzunguka baadhi ya maeneo ya Jiji la Dares
salaam hasa katikati ya Jiji na kugundua kuwa bado kuna uuzaji wa
matunda yaliyokatwa na vyakula sehemu za wazi(barabarani) unaendelea.
Katika kufatilia hilo kujua nini Jijini limefanya hasa Manispaa ya Ilala
ambayo ndo muhusika wa maeneo ya katikati ya Jiji niliwasiliana na
msemaji wa Manispaa ya Ilala Bw. Daud Langa na kutoa ufafanuzi wa suala
hilo.
Msemaji
wa Manispaaa ya Ilala alisema katika suala hili watendaji wa kata na
mitaa wanahusika moja kwa moja kusimamia na kufatilia kwa karibu
operesheni hii na kusisitiza sheria za afya kuzingatiwa na hakutokuwa na
huruma kwa yoyote atakayevunja sheria.
“ Kwa
mfanyabiashara yoyote tutakayemkamata anauza matunda yaliyokatwa na
vyakula maeneo ya wazi tutamkamata na kumfungulia mashtaka ya kuvunja
sheria za Afya na adhabu yake ni faini ya Sh 30,000 au kwenda jela miezi
mitatu au vyote kwa pamoja” alisema Langa alipokuwa akitoa maelezo
hayo.
Nakumbuka
Desemba 9 mwaka huu ilitangazwa kuwa ni siku ya Uhuru na Kazi na Mhe
Rais Dkt Jhn Pombe Joseph Magufuli na kuamuriwa iwe siku ya kufanya
usafi katika maeneo yetu ikiwa ni mapambano dhidi ya ugonjwa wa
kipindupindu ulioenea kwa kasi . katika ziara yangu nilipita maeneo ya
kawe sokoni na mto Mbezi ambapo wananchi kushirikiana na watumishi wa
taasisi za umma na binafsi walijitokeza kufanya usafi katika maeneo
hayo.
Katika
maeneo ya Kata ya kawe eneo la mto Mbezi watumishi wa iliyokuwa Wizara
ya kazi na Ajira ambayo imehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na kuwa Sera,
Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu walijitokeza kufanya usafi
wakishirikiana na wanachi wa maeneo hayo. Cha kushangaza ni pale
watumishi hao walipofika na kuanza kufanya usafi na huku wananchi wa
pale wakiwaangalia kama wafanya maonesho ya sanaa za maigizo.
Hivi
tunasubiri waje watu toka nje ya Tanzania watusafishie maeneo yetu
sisemi watanzania wote ni wavivu hapana ndio wapo wachache waliobarikiwa
kwa kuelewa nini wajibu wao katika jamii inayowazunguka lakini wachache
pia wanaharibu sifa ya watanzania na kufanya watanzania tuonekane
wavivu kazi kutoa lawama hata kwa yale tutanayoweza kuyafanya yaliyo
ndani ya uwezo wetu.
Tabia
yetu watanzania tulio wengi ni kutupia lawama na malalamiko kwa Serikali
hivi kwani Serikali ni nani? Serikali ni mimi na wewe na yule swala sio
Serikali imekufanyia nini ila wewe umeifanyia nini nchi yako? Suala la
usafi liko chini ya uwezo wetu tulifanye basi kwa bidii na hatuifanyii
serikali bali tunaifanyia nchi yetu na vizazi vyetu tukiwa na tabia ya
usafi toka tunakoishi mitaani basi itakuwa tabia ya taifa zima kwa
ujumla.
Watanzania
tujilaumu wenyewe kuugua kipindupindu kwasababu tunaweza kukizuia kwa
kuzingatia usafi wa mazingira na usafi wa mipango miji pia kutojenga
kwenye mikindo ya maji mito na maziwa na vyanzo vya maji kwani maji ndo
chanzo kikubwa cha kipindupindu kwani maji yanatumika kwa asilimia kubwa
katika matumizi ya binadamu ya kila siku.
Serikali
kwa upande wake inapambana sana na suala hili la kipindupindu kwa kasi
kubwa kupitia wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto
ikishirikiana na Halmasahuri za Wilaya, Ofisi za Afya za Mikoa na
Wilaya na katika kukabilana na ugonjwa huu sekta zote husika zikiwemo
Maji, Elimu, Mawasilano, Uchukuzi na Ujenzi hazina budi kushirikiana kwa
pamoja ili kutokomeza ugonjwa huu.
Aidha
wadau wa maendeleo ya jamii hawakuwa nyuma kusaidia kampeni hii ya
kutokomeza kipindupindu nchini, mashirika kama vile shirika la Afya
Duniani (WHO), CDC, USAID, MSF, Red Cross na UNICEF kwa kushiriki katika
kukabiliana na mlipuko huu. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee wadau hawa wamechangia msaada wa fedha na vifaa
vyenye thamani ya Tsh 1,884,000,000 na serikali ikatoa Tsh 900,000,000
katika kupambana na ugonjwa huu.
Watanzania
tunahamasishwa kupambana na ugonjwa huu kwa kuona kuwa kipindupindu ni
aibu kwetu mtu kuugua ugonjwa huu wakati unazuilika kwa kuzingatia usafi
tu. Wote kwa pamoja kupitia magazeti Radio, Televisheni mitandao ya
Jamii kama Whatsaap, Twitter na Instagram tuelimishane kuhusu usafi wa
mazingira ili kutokomeza kpindupindu na kikwa historia nchini.
Kwa
taarifa kuhusu ugonjwa wa kindupindu unaweza kuzipata kupitia ujumbe
mfupi kwenye simu yako kuandika neon kipindupindu kwenda 15774 na
utapata taarifa sahihi juu ya ugonjwa wa kipindupindu na ujembe huu
unapatikana bila malipo. Tukumbuke kuwa kinga ni bora kuliko tiba,
kuugua Kipindupindu ni aibu.
No comments:
Post a Comment