Sehemu
inayoendelea kufukiwa hapo Mtoni Marine ambayo itatumika hapo baadae
kwa ajili ya eneo maalum litakalotoa fursa kwa Wananchi kupata
mapumziko.{ Public Beach }.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } Nd.
Salum Khamis Nassor akimueleza Balozi Seif hatua zinazochukuliwa na
Taasisi yake katika kuona taratibu za uwekezaji zinachukuliwa kwa
wanaowekeza vitege uchumi vyao Nchini.
Balozi
Seif akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baghresa
Group Bwana Said Salim wakitembelea kuona mradi wa Ujenzi wa Majengo
Mapya ya Hoteli ya Mtoni Marine ambayo iko chini ya Kampuni hiyo kwa
hivi sasa.
MRADI
mkubwa wa Kimataifa wa ujenzi wa kisiwa cha Kitalii ambacho
kitatengenezwa kwa mfumo wa ufukiaji Bahari umeanza rasmi katika eneo la
Hoteli ya Utalii iliyopo Mtoni Marine kaskazini Magharibi ya Mji wa
Zanzibar.
Hata hivyo gharama kamili za Mradi huo bado hazijafahamika wakati utakapokamilika rasmi ujenzi wake hapo baadaye.
Mradi
huo unaoendeshwa na Kampuni ya Kizalendo ya Baghresa Group utahusisha
ujenzi wa Hoteli ya Kimataifa ya Ghorofa Tano ya Daraja la Tano { Five
Star + }, utengenezaji wa eneo la wazi la mapumziko { Public Beach }
pamoja na kutengeneza Kisiwa cha Mji mpya.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alishuhudia harakati
za ujazaji wa mchanga katika eneo linalofukiwa ambazo hufanywa kwa
utaalamu wa hali ya juu.
Mhandisi
wa Mradi huo Bwana Ahmed Shamsi alimueleza Balozi Seif kwamba chombo
maalum kinachotumika kwa kazi ya uchimbaji wa mchanga Baharini kina
uwezo wa kunyonya na kusafirisha mchanga kutoka ndani ya Bahari
sambamba na kukata Majabali.
Mhandisi
Shamsi alisema kazi hiyo inafanyika kwa saa 12 kila siku ambapo takwimu
zinaonyesha wazi kwamba uchimbaji huo wa mchanga unaokwenda zaidi ya
mita 15 chini ya Bahari unafikia Tani 600 za mchanga kwa saa Moja.
Alifahamisha
kwamba harakati za uchimbaji na kufukia mchanga katika eneo hilo
zilizoanza Mwezi uliopita wa Novemba zinatarajiwa kukamilika mwezi
Januari mwaka ujao.
Naye
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baghresa Group Bwana Said Salim
Baghresa alisema kwamba ujenzi wa mradi huo muhimu kwa uchumi wa Nchi
utasaidia mapato ya Taifa pamoja na kutoa ajira kubwa kwa vijana
Wazalendo hapa Nchini.
Bwana
Baghresa alisema mfumo wa ufukiaji Bahari kwa ajili ya kuanzisha miradi
ya Kiuchumi ni mfumo unaotumiwa na Mataifa mbali mbali Duniani ambapo
kwa Afrika mradi kama tayari umeanza kutumiwa katika Kisiwa cha
Seycheles.
Akitoa
nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
ameupongeza Uongozi wa Baghresa Group kwa uamuzi uliochukuwa wa
kuanzisha mradi huo mkubwa wa Kimataifa.
Balozi
Seif alieleza kwamba kukamilika kwa mradi huo mkubwa ambao
umeshazoeleka katika Mataifa yaliyoendelea utasaidia kuitangaza Zanzibar
na Tanzania kwa ujumla Kiutalii Kimataifa.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi huo wa Baghresa
Group kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila msaada
unaohitajika katika kuona mradi huo unafikia malengo uliojipangia.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamui wa Pili wa Rais wa Zanzibar
1/12/2015.
No comments:
Post a Comment