Trump akemewa kwa matamshi kuhusu Waislamu - LEKULE

Breaking

9 Dec 2015

Trump akemewa kwa matamshi kuhusu Waislamu


Trump
Trump anaongoza kwenye kura za maoni miongoni mwa wagombea wa Republican
Vigogo wa chama cha Republican nchini Marekani wamemkemea mwenzao Donald Trump, anayetaka kuwania urais kupitia chama hicho, kwa kupendekeza Waislamu wazuiwe kuingia Marekani.
Mmoja wa wanaoshindani tiketi ya kuwania urais Jeb Bush amesema Bw Trump "mwenye kasoro akilini”. Makamu wa rais wa zamani Dick Cheney naye alisema pendekezo hilo "linaenda kinyume na yote ambayo huwa tunatetea”.
Ikulu ya White House, Umoja wa Mataifa na viongozi wa Kiislamu pia wamekosoa matamshi hayo ya Trump.
Bw Trump alikuwa amesema Waislamu wengi wana "chuki” dhidi ya Marekani.
Kwenye hotuba wakati wa kampeni, aliomba "Waislamu wote wazuiwe kuingia Marekani hadi wawakilishi wa nchi wajue ni nini kinachoendelea”
Meneja wake wa kampeni alisema marfuku hiyo ingeathiri "kila mmoja” bila kubagua kama ni mhamiaji au mtalii.
Trump
Trump amekuwa akitoa matamshi yanayozua utata
Lakini Bw Trump aliambia Fox News kwamba haingeathiri “watu wanaoishi humu nchini (Marekani), akiongeza kuwa Waislamu wanaohudumu katika jeshi la Marekani wangekaribishwa "nyumbani”.
  • Mambo 20 makuu anayoamini Donald Trump
  • Trump ashutumiwa kwa kupanga kufurusha wahamiaji
  • Trump: Dunia ingekuwa bora na Gaddafi na Saddam
Matamshi hayo ya Bw Trump yalitolewa Marekani ikiendelea kuomboleza kufuatia shambulio mbaya zaidi la kigaidi kutekelezwa tangu shambulio la Septemba 11, 2001.
Wiki iliyopita, wanandoa wawili Waislamu, ambao wanaaminika kukumbatia itikadi kali, walifyatua risasi na kuwaua watu 14 na kuwajeruhi wengine 21 katika kituo cha afya San Bernardino, jimbo la California.
Bw Trump alishangiliwa sana aliporudia ahadi yake katika mkutano wa kampeni jimbo la South Carolina saa chache baada ya kutoa matamshi hayo mara ya kwanza.

No comments: