Meneja
Mkuu Shirika la Uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC),
Mhandisi Boniface Njombe (kushoto) pamoja na Mtaalamu Mkuu toka Kampuni
ya TOSHIBA Bwana Kentaro Kurahara wakiweka saini Mkataba wa wa Maelewano
(MOU) wa kufanya tafiti kwa pamoja zinahusu maeneo yenye viashiria ya
upatikanaji wa nishati ya jotoardhi katika Ofisi za TGDC zilizopo Jijini
Dar es Salaam.
Meneja
Mkuu Shirika la Uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC),
Mhandisi Boniface Njombe (kushoto) pamoja na Mtaalamu Mkuu toka Kampuni
ya TOSHIBA Bwana Kentaro Kurahara wakikabidhiana Mkataba wa Maelewano
(MOU) wa kufanya tafiti kwa pamoja zinahusu maeneo yenye viashiria ya
upatikanaji wa nishati ya jotoardhi katika Ofisi za TGDC zilizopo Jijini
Dar es Salaam.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja
(kulia) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa ICEIDA, Bwana Engilbert
Gudmundsson, wakiweka saini Mkataba wa Makubaliano ya Ushirkiano wa
kufanya tafiti kwa pamoja zinahusu maeneo yenye viashiria ya upatikanaji
wa nishati ya jotoardhi katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini
zilizopo Jijini Dar es Salaam.
Na Benedict Liwenga-MAELEZO.
KUTOKANA na ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme nchini,
nishati itokanayo na jotoardhi (Geothermal Energy) imetajwa kuwa ni
muhimu katika kuepukana na hasara kubwa na isiyo ya lazima inayotokana
na matumizi ya mitambo ya mafuta katika kuzalisha umeme na kuifanya
Tanzania kuondokana na tatizo la umeme usiokuwa na uhakika pamoja na
kuleta maendeleo nchini.
Ili kuleta Maendeleo haya katika sekta ya nishati, Tanzania
hainabudi kugeukia katika vyanzo vingine vya uzalishaji umeme ikiwemo
nishati hiyo ambayo kwa kutumia mvuke wa maji yaliyochemshwa na joto la
asili lililopo chini ya ardhi, nishati ya umeme inaweza kuzalishwa na
kukidhi mahitaji ya nishati ambayo yatasaidia kuwa kiunganishi cha
ukuaji wa uchumi nchini.
Tanzania iko katika ukanda wa Bonde la Ufa (Rift Valley), hivyo
kuna uwezekano mkubwa wa uwepo wa hifadhi kubwa ya nishati itokanayo na
jotoardhi ambayo inaweza kutumika katika uzalishaji wa umeme na kuinua
uchumi wan chi yetu.
Nishati hii itakuwa mkombozi kwa taifa letu hususani kwa mwananchi
wa kipato cha chini kwani tunaamini kuwa matumizi ya nishati hiyo
yatapelekea kupungua kwa gharama za manunuzi ya umeme na kutokana na
ukweli kwamba nishati hiyo pindi ipatakinapo haitarajiwi kuisha.
Unafuu wa umeme utakaozalishwa na jotoardhi unatokana na ukweli
kwamba mitambo inayotumika kuzalisha umeme huo kuendeshwa kwa mvuke
ambao unatokana na majimoto toka ardhini tofauti na uzalishaji wa umeme
uliokuwa unatumika kwa kutumia mitambo yenye kutumia mafuta ambayo
gharama yake ilikuwa juu kwa Serikali.
Hapa nchini, kuna viashiria vingi vinaonyesha uwepo wa jotoardhi
hasa kwa maeneo ya vijijini ambako umeme sehemu nyingi haujafika,
kutokana na hilo sasa Serikali yetu hainabudi kutupia macho katika
nishati hii kwa kuhakikisha kwamba wananchi ambao wnaaishi maeneo ambayo
nishati hiyo inapatikana wananufaika na umeme huo.
Jotoardhi ina matumizi mengi kwa jamii yetu, mfano majimoto
yatokayo ardhini yanaweza kutumika katika kukaushia mazao mfano matumizi
ya Vitalu shamba(Green Houses) badala ya kutegemea jua. Mwananchi wa
kipato wa chini anaweza kutumia majimoto kukausha mazao yake kwa mfano
mpunga, maharage, mahindi, karanga katika ubora ule ule kama wa jua.
Matumizi mengine ya majimoto ni katika kupasha nyumba joto hasa
katika wananchi wale waishio mikoa yenye baridi kali kwa kujenga mabomba
ya kupitisha maji ya moto ndani ya nyumba zao.
Shirika la Uendelezaji Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC)
imepewa lengo na Serikali la kuhakikisha kuwa inazalisha umeme wa
Megawati 200 na kuuingiza katika gridi ya Taifa kufikia mwaka 2020.
Hivi karibuni, TGDC kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (ESMAP)
zilifanya warsha ya siku mbili iliyofanyika Jijini Dar es Salaam ambayo
iliwakutanisha wadau kutoka Mashirika mbalimbali yanayoshughulikia
masuala ya jotoardhi yakiwemo GDC la Kenya, Shirika la Maendeleo la
Japan (JICA), BGR la Ujerumani, ICEIDA la Iceland, Chuo cha Umoja wa
Mataifa kinachofundisha nishati ya Jotoardhi (UNU), TNO la Uholanzi
pamoja na Shirika la Star Energy la nchini Indonesia ambapo wadau hawa
wote wameweza kufanikiwa kuipata nishati hiyo, hivyo watatoa mchango
mkubwa kuliwezesha shirika la TGDC kupata mafanikio na hatimaye nishati
hiyo kuweza kupatikana.
Katika warsha hiyo, Meneja Mkuu wa Shirika la Uendelezaji nishati
ya Jotoardhi (TGDC), Mhandisi Boniface Njombe alisema kuwa warsha hiyo
inalenga kujadili kwa kina njia mbalimbali zilizotumiwa na baadhi ya
mashirika hayo hadi kufanikiwa kupata nishati hiyo ikiwemo uanishaji wa
huduma tofauti zifanywazo na mashirika hayo katika kulisaidia shirika la
TGDC.
“Matokeo ya warsha hii tuliyoifanya tumeweza kuwasiliana na
wenzetu wa Benki ya Dunia (ESMAP) kwa kukusanya wataalam toka taasisi
mbalimbali pamoja na Mashirika mbalimbali ambayo yamewahi kufanya kazi
hii ya utafutaji wa nishati ya jotoardhi na lengo letu ni kutaka
kufahamu njia ambazo wenzetu walizitumia mpaka kufanikiwa ili na sisi
tupate kujifunza”, alisema Njombe.
Mhandisi Njombe aliongeza kuwa warsha hiyo itawezesha rasilimali
chache zilizopo ziweze kutumika ipasavyo katika kuleta matokeo ambayo
TGDC inatarajia kuyapata ili kuhakikisha kuwa lengo la upatikanaji wa
nishati hiyo linafikiwa.
Sambamba na warsha hiyo, Serikali kupitia TGDC na Shirika la
Kimataifa la Maendeleo la nchini Iceland (ICEIDA), wamesaini Mkataba wa
Makubaliano utakaowezesha Tanzania kunufaika na msaada wa kiasi cha Dola
za Marekani 1,565,000 kwa ajili ya kupata Mtaalam mwelekezi kufanya
tafiti katika maeneo yenye viashiria vya Jotoardhi ikiwemo kuwajengea
uwezo Wataalam wetu wa hapa nchini pamoja na kuwezesha upatikanaji wa
vifaa vya utafiti wa nishati hiyo.
Makubaliano hayo yalifikiwa Jijini Dar es Salaam katika Makao
Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini, kati ya Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja na Mkurugenzi Mkuu wa
ICEIDA, Bwana Engilbert Gudmundsson, huku likishuhudiwa na Meneja Mkuu
wa TGDC, Mhandisi Boniface Njombe, Kamishna Msaidizi wa Nishati
anayeshughulikia Uendelezaji wa Nishati Jadidifu, Bwana Edward Ishengoma
pamoja na baadhi ya Maafisa kutoka TGDC na Wizara ya Nishati na Madini.
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa Mkataba huo, Mhandisi Paul
Masanja alisema kuwa, matarajio ya Tanzania ni kuzalisha kiasi cha
megawati 200 za umeme unaotokana na nishati ya jotoardhi ifikapo mwaka
2020, ambapo taarifa za awali zinaeleza kuwa, hazina iliyopo kupitia
nishati hiyo ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya umeme wa megawati 5,000,
kutokana na nishati ya jotoardhi toka ardhini.
Mhandisi Masanja aliongeza kuwa, utayari na ushirikiano
unaoonyeshwa na nchi ya Iceland kupitia Shirika la ICEIDA itakuwa
kichocheo kikubwa kufikia malengo ya Serikali ya kuwa na nishati ya
kutosha ya umeme na kuchochea maendeleo nchini.
“Tuna malengo mengi kupitia nishati hii ya jotoardhi, utafiti ndio
njia itakayotufanya kufikia malengo haya, ushirikiano huu ni mwanzo
mzuri kwa upande wetu sisi Tanzania, na nafahamu kuwa Iceland mlianzia
katika hatua za chini kabisa lakini sasa mko mbali, zoefu wenu katika
masuala haya ya nishati hii utatuwezesha kuweza kufika mahali
tunapotarajia,” alisema Mhandisi Masanja.
Naye, Mkurugenzi wa ICEIDA, Bwana Engilbert Gudmundsson alieleza
juu ya umuhimu wa nishati hiyo na unafuu wake wa gharama ikilinganishwa
na nishati nyingine na kueleza kuwa, zaidi ya asilimia 25 ya umeme
unaozalishwa nchini Iceland unatokana na nishati ya jotoardhi, hivyo
Tanzania inaweza kufikia malengo yake ya kupata nishati hiyo kwa
kuonyesha juhudi zake ikiwemo kushirikiana na ICEIDA.
“Sisi Ilituchukua kipindi cha miaka 25 kufikia mafanikio
tuliyonayo katika nishati ya jotoardhi, hivyo kutokana na uzoefu wetu
huu hatunabudi kutoa uzoefu wetu kwa TGDC ili kuhakikisha inafakia
malengo,” alisema Gudmundsson.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TGDC, Mhandisi Boniface Njombe
alishukuru na kuonyesha hali ya utayari wa ICEIDA katika kuhakikisha
kwamba Tanzania inafikia malengo yake ya kuendeleza nishati hiyo,
utakaosadia kufanyika kwa tafiti katika maeneo mbalimbali yenye
viashiria vya nishati hiyo kama vile maeneo ya Luhoi pamoja na Kibiti
Mkoa wa Pwani.
Mhandisi Njombe anabainisha kuwa, kutokana na utafiti utakaofanywa
kwa ushirikiano kati ya TGDC na ICEIDA, utawezesha upatikanaji wa
takwimu sahihi na halisi ambazo zitafungua njia ya kupata misaada zaidi
kutoka katika taasisi na wahisani mbalimbali ambao wamejikita katika
masuala nishati hiyo.
Moja ya hatua mbalimbali ambazo zilizofanywa na TGDC mpaka hivi
sasa ni kwamba jotoardhi inakuwa chanzo kingine cha uzalishaji umeme
nchini na kupitia makubaliano hayo, ICEIDA itawezesha Wataalam wa ndani
kutoka TGDC kupata ujuzi na uzoefu utakaowezesha kufanyika kwa tafiti
nyingine katika maeneo mengine huko mkoani Mbeya.
Katika hatua nyingine TGDC pamoja na Kampuni ya TOSHIBA ya nchini
Japan zimetiliana saini Mkataba wa Maelewano wa kufanya tafiti kwa
pamoja zinahusu maeneo yenye viashiria ya upatikanaji wa nishati ya
jotoardhi.
Utiaji saini wa mkataba ni hatua nzuri ambayo sasa inaliwezesha
Shirika la TGDC kuweza kupata msaada wa kitaalam ambao utaliwezesha
shirika hilo kuweza kuchimba ardhini kwa lengo la kupata mvuke
utakaoweza kuzalisha umeme.
Akiongea wakati wa tukio la utiaji saini wa Mkataba huo, Meneja
Mkuu wa TGDC, Mhandisi Boniface Njombe alisema kuwa kupitia Serikali ya
Japan hususani Shirika la Maendeleo Japan (JICA), Kampuni ya TOSHIBA
watasaidia kuomba ufadhili wa Serikali yao ili kuweza kuendeleza ujenzi
wa kituo cha kuzalisha umeme pamoja na matumizi mengine yanayoendana na
nishati hiyo.
“Katika utafiti wa nishati ya jotoardhi tunahitaji watu wenye
elimu na uzoefu na ujuzi wa kutosha, miongoni mwa makubaliano ndani ya
mkataba huu tuliosaini leo ni wafanyakazi wetu kadhaa kuwapeleka nchini
Japan kwenye vyuo vyao ili kuweza kupata mafunzo ya darasani na
kutembelea maeneo ambayo Japan wana vituo vya jotoardhi ili wapate ujuzi
wa kufanya kazi na Wajapan na kutuletea ujuzi huo hapa nchini”, alisema
Njombe.
Kupitia ushirikiano huu unaoonyeshwa na Serikali ya Awamu ya Tano
ya Tanzania, tuna imani kuwa nchi ya Japan itaendelea kuisadia Tanzania
katika kuendeleza nishati ya jotoardhi kwakuwa ni nishati yenye tija
katika kutimiza ndoto za Tanzania kwa kuifanya kuwa nchi yenye kipato
cha kati kufikia mwaka 2020.
TGDC inatarajia kuanza kuainisha maeneo ya ushirikiano wa pande
hizi mbili (TGDC na TOSHIBA) ikiwemo kuyawekea muda wa utekelezaji
ambapo mwezi Machi mwakani, Wataalam toka TGDC wataweza kwenda nchini
Japan kwa ajili ya kwenda kupata elimu zaidi kuhusu nishati hiyo.
Mtaalamu Mkuu toka Kampuni ya TOSHIBA Bwana Kentaro Kurahara
anaeleza kuwa kampuni yao iko tayari kuisaidia Tanzania katika masuala
yanayohusu jotoardhi na iko tayari kuomba ufadhili kupitia Serikali ya
Japan ikiwemo kuwapa Wataalam wa TGDC elimu ya kutosha inayohusu nishati
hiyo ili waweze kuhakikisha kuwa nishati hiyo inapatikana na kuleta
maendeleo kwa Tanzania.
“Tunafuraha ya kushirikiana na TGDC katika kufanya tafiti
zinazohusu jotoardhi kama mkataba wetu tuliousaini unavyosema, kupitia
Serikali ya Japan na Shirika la JICA tutaomba ufadhili kwa ajili ya TGDC
ili muweze kuleta wataalam wenu kuja kujifunza Japan pamoja kuwasaidia
katika masuala mengine yanayohusu shughuli ya utafutaji wa nishati hii”,
alisema Kurahara.
TGDC ikiwa kama Shirika Tanzu lililopo chini ya Kampuni ya Ugavi
wa Umeme Tanzania (TANESCO) limepewa lengo na Serikali la kuharakisha
upatikanaji wa nishati ya jotoardhi kufikia Megawati 200 mwaka 2020.
Kampuni hiyo imesajiliwa Disemba 19, 2013 na kuanza kufanya kazi Julai
2014 huku ikipewa jukumu la kuharakisha uendelezaji wa nishati ya
Jotoardhi nchini ambapo mpaka hivi sasa TGDC imegundua Zaidi ya maeneo
yenye viashiria vya jotoardhi ambayo yamegawanyika katika Kanda Nne
ambazo ni Kanda kaskazini–Ziwa Manyara, Kreta ya Ngorongoro, Natron na
Majimoto Mara, Kanda ya Mashariki–Utete (Pwani), Kisaki (Morogoro),
Luhoi (Pwani), Kanda ya Magharibi–Ibadakuli (Shinyanga),
Mtagata(Kagera), maeneo mengine ni Dodoma, Singida pamoja na Tanga.
No comments:
Post a Comment