MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
ISO 9001:2008 CERTIFIED
TAARIFA KWA UMMA
TAHADHARI KUHUSU KUINGILIA AU KUFUATILIA MAWASILIANO YA WATU
***
Katika
siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa za kuwepo kwa Programu
(Application) ya simu ikijulikana kama SOFTBOX TANZANIA iliyosemekana
iko kwenye Google PLAYSTORE.
Ilidaiwa
kuwa program (Application) hiyo ya SOFTBOX TANZANIA ilikuwa na uwezo wa
kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na
mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu ya mtu binafsi.
Kwa
yeyote aliyekuwa na nia hiyo ya kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu,
ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu ya
mtu mwingine alihitajika kulipia fedha kiasi cha Tshs 35,000/= kupitia
mitandao ya simu ili kupata namba ya siri kwa ajili ya kuwezesha nia
hiyo.
Mamlaka
ya Mawasiliano imefanya uchunguzi kubaini kuwepo kwa programu hiyo na
ukweli kuhusu uwezo wake wa kufanya kilichodaiwa, ikiwa ni pamoja na
kuangalia madhara ya program hiyo na sheria inasema nini kuhusu suala
hili.
Baada
ya kufanya uchunguzi wa kina, Mamlaka ya Mawasiliano ilibaini na
imejiridhisha kuwa program (Application) hiyo haina uwezo huo wa kunasa
au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya
WhatsApp kutoka kwenye simu ya mtu binafsi kama ilivyodaiwa.
Aidha
Mamlaka imebaini kuwa watengenezaji (Developers) wa programu hiyo
walikuwa na nia ya kutapeli na kujipatia fedha hiyo kiasi cha Tshs
35,000/= kwa njia ya udanganyifu wakitumia kivutio cha kunasa au
kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya
WhatsApp kutoka kwenye simu za watu binafsi.
Programu (Application) nyingine ya aina hiyo iliibuka tena ikiitwa SIMNET Tanzania ikiwa na maelezo kama ya awali.
Wakati
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania pamoja na Jeshi la Polisi wakiendelea
na uchunguzi zaidi, tunapenda kuuarifu umma wa Watanzania kuepuka
kufanya mambo yafuatayo:
1.
Kuvutiwa na matendo yaliyo kinyume na sheria na maadili ya matumizi
mazuri ya mawasiliano kama hili la kunasa au kuingilia mazungumzo ya
simu, ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu
ya mtu binafsi.
Kitendo
hiki ni kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu cha 6 na 10 cha Sheria ya
Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 na kifungu cha 123 cha Sheria ya
Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya Mwaka 2010.
Sheria
katika vifungu hivyo inakataza mtu yeyote kuingilia mawasiliano ya mtu
mwingine. Adhabu kali ya makosa haya ni faini isiyopungua shilingi
milioni tano au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja
au vyote kwa pamoja.
2.
Mamlaka inawatahadharisha watumiaji wa huduma za mawasiliano kutokuwa
wepesi na kudanganyika kufanya malipo yoyote kwa njia ya mitandao kwa
huduma wasiyokuwa na uhakika nayo au bila kujiridhisha na uwepo wa
huduma hiyo.
Ni
vizuri kutoa taarifa kwa mtoa huduma wako au kuwasiliana na Mamlaka ya
Mawasiliano kupitia barua pepe malalamiko@tcra.go.tz au kupiga simu
namba 0784558270/1.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
04/12/2015.
No comments:
Post a Comment