Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, ameishangaa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kutogawa bure Mashine za EFDs, na wao kubaki na kazi ya kukusanya mapato.
Akizungumza
katika mkutano wa wafanyabiashara na wawekezaji jana jijini Dar es
Salaam, ulioandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na Baraza la
Biashara la Taifa (TNBC), alisema muda uliopotea na kodi ambayo
haikukusanywa wakati wa mvutano na wafanyabiashara ungetosha kununua
mashine mpya na kuwagawia.
“Kama
mnajua mashine hizi ni halali na ni zenu, wapeni bure kazi yenu iwe ni
kukusanya kodi, ni hesabu rahisi sana isiyohitaji kwenda chuo kikuu kuwa
muda uliopotea na fedha hazifiki bilioni 12 zingetosha kununua na iwe
kazi ni kukusanya kodi,” alisema.
Awali
katika salamu zake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Jonson
Minja, alimpongeza rais kwa kazi kubwa aliyofanya Bandarini na TRA kwa
kuwa imewezesha kodi kukusanywa kwa usahihi na kwamba kipindi cha nyuma
fedha nyingi zilipotea, kutokana na mfumo wa ukusanyaji kodi kutowekwa
wazi.
Aidha,
alisema mashine za EFDs zitatumika kwa wafanyabiashara wote mwakani,
kwa kuwa changamoto zilizosababisha mvutano baina yao na serikali
zimemalizika.
Aidha,
alimtaka rais kufuatilia kwa karibu ukwepaji kodi katika sekta isiyo
rasmi na kwamba kukiwa na mipango madhubuti serikali itaweza kupata kodi
kwa wananchi wote.
“Kasi
ya rais inatupa matumaini makubwa sana, tunachoweza kusema, Mungu
akubariki akupe hekima na nguvu...tunaomba uimarishe viwanda vya kati na
vidogo ili malighafi zisisafirishwe kwenda nje, bidhaa ambazo
zitasaidia kukuza uchumi na kuimarisha shilingi dhidi ya Dola ya
Marekani,” alisema.
Tangu
mwaka juzi kulikuwa na mvutano mkali baina ya wafanyabiashara na TRA,
ambao waligoma kutumia mashine hizo hadi serikali itakaposhughulikia
kero zao ikiwamo bei ya mashine, utitiri wa kodi, ukwepaji kodi na
urasimu uliopo.
Wafanyabiashara
kwa umoja wao waliitisha mgomo nchi nzima na kumekuwa na mazungumzo ya
mara kwa mara na serikali, ambayo wakati mwingine hayakufikia ukingoni,
hatua iliyofanya baadhi ya viongozi wa wafanyabiashra kukamatwa.
Minja
alikamatwa na Polisi mkoani Dodoma mwaka jana, na kuswekwa ndani, jambo
lililofanya wafanyabiashara kuitisha mgomo wa siku tatu hadi serikali
itakapoeleza alipo kiongozi wao.
Baadaye
ilibainika anashikiliwa na Polisi mkoani humo, na alipandishwa mahakama
ya mkoa na kusomewa mashtaka ya kuchochea mgomo wa wafanyabiashara
nchini.
Baadaye mahakama ya mkoa ilimuachia huru kiongozi huyo.
No comments:
Post a Comment