Serikali Yasema Tamko Lake La Tiba Mbadala na Asilia Liko Palepale - LEKULE

Breaking

29 Dec 2015

Serikali Yasema Tamko Lake La Tiba Mbadala na Asilia Liko Palepale



Serikali imesema kwamba tamko lake lilitolewa hivi karibuni kuhusu matangazo ya Tiba Asili na Tiba Mbadala liko palepale kwa kuwa lengo lake ni kuboresha huduma hiyo. Hivyo kama  kuna mtoa huduma ambaye amekwazika na tangazo hilo Wizara ipo tayari kuzungumza naye.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tamko hilo kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo jijini Dar es Salaam.

Tamko hilo lilitolewa Desemba 24, mwaka huu,ambapo limepiga marufuku  matangazo yote yanayohusu tiba asili na tiba mbadala kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Kwa wale wenye vibali wanatakiwa kuviwasilisha vibali na matangazo yao kwenye Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala ili vifanyiwe mapitio.

Tamko hilo  liliendelea  kufafanua kwamba  utoaji wa elimu ya afya kwa umma unaofanywa na watoa huduma za tiba asili na tiba mbadala kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii umepigwa marufuku hadi hapo utaratibu mwingine utakapotangazwa.

‘Watoa huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini kote wanaagizwa wawasilishe kwenye Baraza nyaraka zote muhimu ndani ya wiki mbili kuanzia leo Desemba 2015. Baadhi ya nyaraka hizo ni zile zinazohusu kuuza dawa za asili na tiba mbadala, nyaraka za kumiliki mashine zinazotumika katika kufanya uchunguzi katika tiba asili na tiba mbadala,’ lilieleza tamko hilo.

Tamko hilo lilifafanua kwamba  Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala linaagizwa katika kipindi cha siku 14 kuanzia  24 Desemba 2015, lipitie nyaraka zote zikapowasilishwa zinazohusu usajili wa watoa huduma, usajili wa vituo vyao, ikiwa ni pamoja na maduka ya dawa za asili na dawa za tiba mbadala, usajili wa dawa zote zinazotumika katika huduma hizo na usajili wa mashine zote zinazotumika katika huduma za tiba asili na tiba mbadala.

Aidha  akizungumzia kuhusu tangazo hilo, Waziri   Ummy alisema  ‘Mimi  niko tayari kuzungumza na mtoa huduma ambaye amekwazika na tangazo hili, ili aweze kueleza ni sababu zipi zinazomfanya asisajiliwe.  Tunafanya hivi kwa mujibu wa sheria ,kanuni na taratibu,’ alisisitiza.

Aliongeza kwamba Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala  Namba 23 ya Mwaka 2002 inaeleza  wazi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo alitaja idadi ya watoa huduma hiyo kuwa   wako 75,000 kwa takwimu za nchi nzima.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili  na Tiba Mbadala, Dkt. Edmund Kayombo alisema hadi sasa hawajapokea mrejesho wa tamko   hilo la  Serikali.

Kwa upande wake  Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama  Vya Tiba Asili Tanzania(SHIVYATIATA), Abdulrahaman  Lutenga alisema  hakuna mganga yoyote aliyepinga tamko hilo na Serikali, hivyo tamko lililotolewa  hivi karibuni la kupinga agizo hilo si halali kwa kuwa halikupitia katika shirikisho hilo.

‘ Hatutambui kampuni hii iliyotoa tamko la kupinga tangazo la Serikali kwani ya mtu binafsi yenye wanahisa 11,’ alisema Lutenga.

Akizungumzia kuhusu hatima ya tamko hilo, Dkt. Kayombo alisema baada ya siku walizotoa  kumalizika  watatangaza hatua zipi zitachukuliwa kama vile kuwaondoa wasiofuata sheria.

No comments: