Serikali Yafuta ‘Semina Elekezi’ Kwa Madiwani - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Wednesday, 23 December 2015

Serikali Yafuta ‘Semina Elekezi’ Kwa Madiwani


Serikali imesema mafunzo kwa ajili ya madiwani wote hayatakuwepo na badala yake wenyeviti na makamu wa wenyeviti kote nchini ndio watapatiwa mafunzo ya namna ya kusimamia halmashauri zao.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia Utumishi na Utawala Bora, Selemani Jafo alisema hayo wakati alipofanya ziara ya kutembelea Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo mjini Dodoma.

“Madiwani ni wengi wote kuwapatia mafunzo haiwezekani kila halmashauri itatoa mwenyekiti na makamu mwenyekiti, meya na naibu meya” alisema Jafo.
 Alisema mafunzo hayo yatahusisha wenyeviti wa halmashauri na makamu wao kutoka halmashauri 185 nchini na kuwaagiza wakurugenzi kuhakikisha viongozi hao wanafika Chuo cha Hombolo tayari kwa ajili kwa mafunzo hayo.

Alisema miaka ya nyuma kulikuwa na utaratibu wa kuwapatia mafunzo madiwani waliochaguliwa baada ya Uchaguzi Mkuu, lakini sasa ni wenyeviti na makamu wenyeviti wa halmashauri ndio watapatiwa mafunzo hayo.

Alisema halmashauri 185 zilizopo nchini zitapeleka watu wawili kila halmashauri na waliopata mafunzo hayo watakwenda kuwafundisha wengine.
 Naibu Waziri alisema kulikuwa na changamoto nyingi katika Uchaguzi Mkuu uliopita na madiwani walichaguliwa kutokana na sifa zao na wengine wananchi walifanya uchaguzi wa hasira, lakini mwisho wa siku kiongozi aliyetakiwa alipatikana.

Alisema madiwani wapya waliopatikana wapo wafanyabiashara, wanafunzi na watu wa kada mbalimbali ambao wote walitakiwa kufundishwa namna ya kutenda kazi zao.
 Hata hivyo, alisema mafunzo kwa ajili ya madiwani wote hayatawezekana, bali viongozi wa madiwani hao ndio watapatiwa mafunzo hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa, Dk Emmanuel Gibai alisema maandalizi kwa ajili ya mafunzo hayo yamekamilika. 

Awali yalipangwa kutolewa kwa madiwani wote, lakini kutokana na maelekezo hayo wahusika watakaotakiwa kupatiwa mafunzo hayo watayapata.
Post a Comment