Remija Salvatory na Nuru Mwasampeta
Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Omar Chambo amewaagiza
Madaktari wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama kuandaa utaratibu wa
kuwawezesha wahanga wa Mgodi wa Nyangalata kwenda Hospitali za rufaa
kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya zao.
Mhandisi
Chambo aliyasema hayo alipowatembelea wahanga hao waliolazwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Kahama kutokana na ajali ya kufukiwa na kifusi
na kufanikiwa kuokolewa baada ya kuishi chini ya ardhi kwa siku 41
katika Mgodi wa Nyangalata mkoani Shinyanga.
Katibu
Mkuu alitoa maagizo hayo baada ya mmoja wa wahanga hao, Joseph Buruge
kueleza kuwa ingawa ngozi za wachimbaji hao zinaonekana kuimarika
lakini bado kuna tatizo la vijipele vidogo vidogo mwilini ambavyo baada
ya muda hutoa usaa hivyo aliomba uchunguzi wa kina ufanyike ili kutibu
tatizo hilo.
“Kwa
kweli Mheshimiwa tunaendelea vizuri na matibabu na tunawashukuru
madaktari na wauguzi wote wanaotuhudumia na tunaishukuru Wizara na
Serikali kwa ujumla kwa misaada na huduma walizotoa, lakini kwa sababu
umekuja Mheshimiwa tuna maombi yetu ambayo tunaomba Serikari iweze
kutusaidia sisi wahanga wote” , alisema Buruge.
Buruge
alisema kuwa pamoja na kuwa afya zao zinaimarika lakini kuna viashiria
ambavyo si vizuri kwa sababu ya kula magome ya miti na wadudu chini ya
mgodi hivyo wanahitaji uchunguzi kwani magome ya miti yalikuwa
yakiwalevya kama wamekunywa pombe kali hivyo ni vyema uchunguzi
ukafanyika ili kujua kama magome hayo yalikuwa na sumu na athari zake
katika miili yao.
Pamoja
na hayo, wameomba pia kufanyika kwa uchunguzi wa tumbo kwa kuwa maji
machafu waliyokuwa wakinywa chini ya mgodi yalikuwa na kemikali
kwani yalikuwa yamechanganyika na baruti hivyo ni vema kufahamu baruti
iliwaathiri kiasi gani.
Baada
ya maombi hayo, Mhandisi Chambo aliwaahidi wahanga hao kuwa ataendelea
kufanya mawasiliano na Madaktari wa Hospitali hiyo ili kuhakikisha
majibu ya maombi yao yanafanyiwa kazi kwa wakati. Aidha aliwahakikishia
kuwa vipimo vyote wanavyotakiwa kufanyiwa vitagharamiwa na Serikali.
Alipotakiwa
kuanza taratibu za kuwahamishia wahanga hao katika hospitali ya Rufaa
ya Bugando, Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Robert Rwebagira
alisema kuwa wahanga hao wanahitajika kwenda Hospitali kubwa ya
Muhimbili kwani wataweza kupata huduma zote ambazo zitachukua si chini
ya miezi Sita.
Alisema
kuwa huduma za awali walizopatiwa wahanga hao zilikuwa ni kuangalia
miili yao (Physical treatment) na sasa wanahitaji matibabu ya
kisaikolojia na kiakili ambayo yatapatikana katika hospitali ya Rufaa
ya Muhimbili.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Kahama Mjini Jumanne Kishimba ameahidi
kushirikiana bega kwa bega na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Vita Kawawa
pamoja na Hospitali hiyo ili kuhakikisha kuwa wahanga hao wanapata
huduma stahiki na ndani ya wakati.
Wahanga
Watano wa mgodi wa Nyangalata waliopokelewa katika hospitali ya wilaya
ya Kahama tarehe 16/11/2015 ni Amos Muhongo, Joseph Buruge, Msafiri
Gerard, Chacha wambura na Onyiwa Kaiwao ambaye kwa sasa ni marehemu.
No comments:
Post a Comment