Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana
na kufanya mazungumzo na Spika wa Seneti na Mjumbe Maalum wa Rais wa
Jamhuri ya Burundi Mheshimiwa Reverien Ndikuriyo Ikulu jijini Dar Es
Salaam kuhusu hali ya kisiasa na usalama nchini Burundi na jitihada
zinazochukuliwa na Tanzania ikiwa ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Afrika
Mashariki
Akiwasilisha
ujumbe wa Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi kuhusu hali ya Burundi,
Spika Ndikuriyo amesema Serikali ya Burundi ipo tayari kufanya
mazungumzo na wadau wote wa siasa kuhusu hali ya Burundi na jitihada za
kuumaliza mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo
Akitoa
maelezo ya kikao hicho kwa niaba ya Rais Magufuli, Balozi Maiga amesema
serikali ya Burundi imekubali usuluhishi unaofanywa na Rais wa Uganda
Mh. Yoweri Kaguta Museveni kwa niaba ya Marais wa Jumuia ya Afrika
Mashariki kutokana na kikao kilichofanyika Jijini Dar es salaam mwezi
Julai mwaka huu na kwamba serikali ya Burundi iko tayari kushiriki
katika mazungumzo hayo ya amani.
“Mheshimiwa
Rais Magufuli amefanya mazungumzo na rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi
mwishoni mwa wiki iliyopita ambaye amemuhakikishia Rais Magufuli
utayari wake wa kushiriki katika mazungumzo hayo ya usuluhishi” Alisema Balozi Maiga .
Balozi Maiga ameongeza kuwa “nimeagizwa
nilipeleke taarifa kwa mawaziri wa nchi za nje wa nchi jirani juu ya
maandalizi ya mazungumzo hayo ambayo yataanza kule Uganda tarehe 28
mwezi Desemba na Waziri wa Ulinzi wa Uganda amekabidhiwa jukumu la
kuratibu mazungumzo hayo”
Ameongeza
kuwa suala jingine lililojitokeza katika mazungumzo hayo ni juu ya
uamuzi wa baraza la usalama la umoja wa Afrika kutaka kupeleka majeshi
yake nchini Burundi baada ya siku tano jambo ambalo Bunge la Burundi
limepinga.
Balozi
Mahiga amesema Burundi imepinga maamuzi hayo kwa kuwa inaamini kuwa
hakuna hali ama dalili za kutokea kwa mauaji ya kimbari kama ya Rwanda,
na kwamba kwa sasa kuna utulivu nchini humo tofauti na wasiwasi wa Umoja
wa Afrika, Jumuia za kimataifa hasa Umoja wa Ulaya, na kwa kiwango
fulani Umoja wa Mataifa unaotoa msukumo wa kutaka kuyapeleka majeshi ya
kulinda amani nchini Burundi.
“Wao
kama Burundi wakiwa ni washirika wakubwa wa kulinda amani katika bara
la Afrika wana wanajeshi 6000 nchini Somalia,wanajeshi 1000 Jamhuri ya
Afrika ya Kati na dhamira yao katika kushiriki kuleta amani, wao
watakuwa ni watu wa mwisho kuleta hali itakayosababisha hatari ya
kutokea kwa mauaji yanayofanana na mauaji ya kimbari” amesisitiza Balozi Mahiga
Dkt.
Maiga amesema kutokana na maelezo hayo, Rais Magufuli amependekeza kuwa
serikali ya Burundi ifungue milango ya mazungumzo na kuwakaribisha
Umoja wa nchi za Kiafrika kupeleka ujumbe wa aina yeyote ili kwa pamoja
waweze kutathmini hali usalama ilivyo nchini Burundi badala ya kukataa
pendekezo hilo moja kwa moja.
Aidha,
Balozi Mahiga amesema, Rais Magufuli amemuagiza kwenda nchini Burundi
kutazama, kujiridhisha na kutathmini hali halisi ilivyo hususani katika
suala la amani hasa ulinzi na usalama wa raia katika jiji la Bujumbura
na maeneo mengine ya nchi hiyo ili kufahamu sababu zinazowafanya warundi
kukimbia nchi yao na kukimbilia nchi majirani ikiwemo Tanzania kama
wakimbizi.
Ameongeza
kuwa safari yake ya kwenda Burundi kwa kiasi kikubwa itasaidia katika
kuendeleza mazungumzo yanayotarajia kufanyika huko Uganda.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Dar es Salaam.
22 Desemba, 2015
No comments:
Post a Comment