Jeshi
la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia askari polisi
sita, wawili wakiwa askari wa kawaida na wanne wa Idara ya Wanyamapori
kwa tuhuma za kusababisha vifo vya watu wawili wanaodaiwa kujihusisha na
ujangili.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kanda
hiyo, Kamishna Suleiman Kova, aliwataja askari hao wa kawaida kuwa ni
Bonny Mbange ambaye ni mkaguzi wa polisi E.909D/SGT na mwingine
aliyemtaja kwa jina moja la Filbert.
Kwa upande wa Askari wa Wanyamapori aliwataja kuwa ni Emmanuel Mbaga, Deogratias Mwageni, Joseph Jimmy na Asubile Mwakyusa.
Kamishna
Kova aliwataja watuhumiwa waliofariki kuwa ni Yasin Rashidi (46) na
Samson Michael (46) mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam.
Aidha,
Kamishna Kova alisema awali waliwakamata askari saba walioshiriki
katika mauaji hayo, lakini wakati wanahojiwa mmoja kati yao aitwaye Issa
Kazimoto mwenye namba F.5371D/C alifanikiwa kutoroka.
Alisema
taarifa za awali zinaonyesha kuwa askari hao na wenzao wa Idara ya
Wanyamapori kutoka kikosi maalum cha kuzuia ujangili walikuwa
wanafuatilia watu wawili kwa tuhuma za ujangili.
Alisema
Desemba 9, mwaka huu, zilitolewa taarifa Kituo cha Polisi Magomeni
kutoka kwa askari waliokuwa katika operesheni maeneo ya Sinza kuwa
watuhumiwa waliokuwa wanawafuatilia wamefariki dunia katika harakati za
kuwakamata.
Alisema
uchunguzi wa awali wa tukio hilo unaonyesha kuna utata tangu wakati wa
ukamatwaji hadi vifo vya marehemu hao wawili na ndiyo sababu askari hao
wanashikiliwa ili kupata ukweli wa vifo hivyo na uhalali wa nguvu
iliyotumika.
Aliongeza
kuwa ukaguzi wa miili ya marehemu hao unaonyesha kuwa walipata majeraha
ya risasi, hivyo uchunguzi wa kisayansi utafanyika ikiwa ni pamoja na
kuwahusisha madaktari bingwa wa uchunguzi wa miili.
Aidha,
Kamishna Kova aliwataka wananchi wenye taarifa zaidi kuhusu tukio hilo
walisaidie Jeshi la Polisi ili sheria ichukue mkondo wake.
No comments:
Post a Comment