Waziri
wa wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameuagiza uongozi wa
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Kanda ya Ziwa kuhakikisha
wanauingiza mkoa wa Kagera katika Gridi ya Taifa baada ya kubainika nchi
inaingia gharama kubwa kununua umeme kutoka Uganda.
Alitoa
agizo hilo jana wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Kagera na
kusisitiza katika mipango mipya ya Tanesco kwa sasa, ni lazima iondokane
na umeme wa gharama kubwa.
Katika
ziara hiyo ambayo alikagua mitambo ya kusambaza umeme katika wilaya za
Bukoba, Biharamulo na Ngara, Muhongo alisema umeme unaonunuliwa kutoka
Uganda wa megawati 5.2 , kila uniti hununuliwa senti nane za Kimarekani.
Aliagiza
kwamba kabla ya Tanesco kusaini mkataba mpya na Uganda, wanapaswa
kusaini mkataba wa muda wakati wakiendelea kuweka utaratibu wa
kuhamishia mkoa wa Kagera kwenye Gridi ya Taifa. Alisema mkoa huo
ukiingizwa kwenye gridi, Tanesco itaepuka gharama kubwa za kunununua
umeme wa gharama ya juu kutoka nchi hiyo.
Alisema
kwa sasa Gridi ya Taifa imefika Nyakanazi, wilayani Biharamulo. “Kwa
hiyo hata wilaya nyingine hazina budi kuingizwa katika gridi ili kufanya
mkoa uwe na umeme wa uhakika na wa bei nafuu utakaowafanya wananchi
kuzalisha kwa kutumia umeme…,” alisema.
Alisema
Tanzania lazima iwe na umeme wa uhakika na wa gharama nafuu ndipo
itafikia malengo ya nchi ya kipato cha kati. Alisisitiza kuwa, bila
umeme, viwanda haviwezi kuzalisha na ajira haziwezi kupatikana. Alisema
hakuna nchi yoyote duniani ambayo ina kipato cha kati ambayo watu wa
kati hawatumii umeme.
Alisema
Tanzania ina asilimia 42 wakati inatakiwa kufikia asilimia 75. “Kwa
hiyo Tanesco mtake msitake, lazima umeme uwepo tena wa bei nafuu ili
kuwezesha viwanda vyetu viweze kuzalisha kwa wingi na pato letu liweze
kupanda zaidi ya mara nne na asiyetaka kasi hiyo ataondoka atuachie kazi
zetu,” aliagiza Muhongo.
Wakati
huo huo, aliagiza uongozi wa Tanesco wilaya ya Biharamulo kwamba
ifikapo Januari 2 mwakani, wawapatie majibu wananchi wa kata ya
Nyarukongongo yenye kaya 800 ni lini watapatiwa umeme. Alisema
wameshachangia fedha zao na wanahitaji umeme.
Alisisitiza,
wakati huu sio wa kusubiri wateja wawafuate maofisa wa Tanesco ofisini
bali wao wanapaswa kuwafuata wateja vijijini. Aliwataka Tanesco kuacha
tabia ya kuomba fedha Hazina wakati zipo kwa wananchi wanaohitaji
kuunganishiwa umeme.
Aidha,
ameagiza uongozi wa Tanesco mkoani Kagera kuhakikisha wanafunga umeme
katika jengo la Forodha la Rusumo kwa upande wa Tanzania ndani ya wiki
moja ijayo na kuepuka hali ya sasa ambayo watumishi wanatumia umeme
kutoka Rwanda.
Meneja
wa Tanesco wa Kanda ya Ziwa, Aron Maganga alimweleza Waziri Muhongo
kuwa ifikapo mwaka 2018, mradi wa Gridi ya Taifa utakuwa umekamilika
katika mkoa wa Geita na itakuwa rahisi mkoa wa Kagera kuingizwa kwenye
gridi hiyo.
Maganga
alisema chini ya mpango wa sasa, shirika limetoa maagizo kwa mameneja
wote wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha ifikapo Januari 15 mwakani mita
mbovu zote zitarekebishwa na wateja wote wa zamani walioomba
kuunganishiwa umeme watakuwa wameunganishiwa umeme.
Waziri
aliwataka wananchi hao kuwa ifikapo Janurai 15, matatizo hayo ya
kufungiwa umeme na uwapo wa mita mbovu katika maeneo mbalimbali ya mkoa
wa Kagera, watoe taarifa kwa wakuu wa wilaya matatizo yao
yashughulikiwe.
Waziri
Muhongo ametembelea vituo vya kupokea na kusambaza umeme vya kuzalisha
umeme vya Kibeta, Biharamulo, Ngara na kukagua jengo la forodha la
Rusumo na mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Rusumo.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akimsikiliza
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella kabla ya kuanza ziara ya kukagua
miundombinu ya umeme mkoani humo.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kushoto) akimsikilizaMhandisi Filbert Mlaki.
Waziri wa nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akikagua moja ya mtambo wa kuzalisha umeme wa Kituo cha Kibeta
No comments:
Post a Comment