WAFUGAJI
waliovamia maeneo ya wakulima katika kijiji cha Dihinda wilayani
Mvomero mkoani Mogorogo na kusababisha mapigano yaliyoua mkulima na
ng’ombe 71, wamekimbia kijijini hapo na kutokomea kusikojulikana.
Akizungumzia
hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Wilaya ya Mvomero, Mkuu
wa Wilaya hiyo, Betty Mkwasa alisema ulinzi bado umeimarishwa eneo hilo,
na kwamba wafugaji waliovamia wamekimbia.
“Wafugaji
wamekimbia na sisi tutateketeza maboma yao, kwa sababu walivamia eneo
hili la wakulima na ng’ombe walioachwa wamepigwa mnada na fedha
imeingizwa kwenye mfuko wa serikali ya kijiji hicho,” alisema Mkwasa.
Aidha,
katika msako uliofanywa kwa ushirikiano wa Serikali ya Wilaya na Polisi
silaha moja ya askari iliyochukuliwa ilipatikana na kwamba wakulima
wametolewa hofu na kusisitizwa kuendelea na kazi zao kama kawaida.
Alifafanua
kwamba hali kwa sasa kijijini hapo ni shwari na kwamba mifugo iliyouawa
kwa kukatwakatwa mapanga yote imeshafukiwa na uongozi wa serikali ya
wilaya umepanga kuingia mkataba na viongozi wa vijiji na kata ili
kudhibiti, migororo baina ya makundi hayo.
Alisema
katika kudhibiti matukio ya mapigano au uvunjifu wa sheria na mpango wa
matumizi bora ya ardhi, Mvomero itaanza kuingia mkataba na watendaji wa
vijiji na kata na iwapo migogoro itatokea, wao ndio watawajibishwa.
Awali
Desemba 12, mwaka huu, kundi la wafugaji wa jamii ya Kibarbaig
waliwavamia wakulima na kuanza kuwashambulia kutokana na mmoja wa
wafugaji ambaye mifugo yake iliharibu mazao ya mkulima kutakiwa kulipa
fidia ya Sh 200,000.
No comments:
Post a Comment