Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, imetupilia mbali shauri la kesi ya
kupinga matokeo yaliyompa ushindi wa ubunge wa Kyela, Dk Harrison
Mwakyembe(CCM).
Kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa
ubunge wa jimbo hilo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge kupitia
Chadema, Abraham Mwanyamaki baada ya kushindwa kulipa Sh3 milioni ambazo
ni dhamana ya kesi kwa anaowalalamikia.
Sheria ya kesi
za kupinga matokeo ya ubunge inamtaka mlalamikaji kulipa dhamana ya Sh5
milioni kwa kila anayemlalamikia, ambapo Mwanyamaki alitakiwa kulipa
jumla ya Sh15 milioni kwakuwa aliokuwa akiwalalamikia walikuwa watatu.
Hata
hivyo Mwanyamaki baada ya kuomba huruma ya mahakama alipunguziwa hadi
Sh1 milioni kwa kila mlalamikiwa. Jumla alitakiwa alipe Sh3 milioni.
Pia
Mahakama hiyo imeamuru Mwanyamaki kulipa fidia ya gharama za
walizotumia walalamikiwa katika kesi hiyo, ambao ni Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Kyela, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Dk Mwakyembe.
Mwanyamaki
ni miongoni mwa waliyokuwa wagombea wa mkoani Mbeya, ambao walifungua
kesi mahakamini hapo, wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliopita.
Wengine
ni Liberatus Mwang’ombe (Chadema) dhidi ya mbunge Haroon Pilmohamde wa
CCM (Mbarali), John Mwambigija (Chadema), dhidi ya Saul Amoni wa CCM
(Rungwe), Dk Luca Siame (CCM) dhidi ya David Silinde wa Chadema (Momba),
Adam Zella (Chadema) dhidi ya Oran Njeza wa CCM (Mbeya Vijijini) na
Fanuel Mkisi (Chadema) dhidi ya Jophet Hasunga wa CCM (Vwawa).
Jaji
wa mahakama hiyo, Atuganile Ngwala alitoa uamuzi huo jana mahakamani
hapo baada ya wakili wa Mwanyamaki, Benjamini Mwakagamba akisaidiana na
Adrian Mhina kudai mahakamani hapo kwamba mteja wao alishindwa kutoa
kiasi hicho alichotakiwa kulipa ili kesi ya msingi iweze kuendelea,
hivyo wanaiachia mahakama iweze kutoa uamuzi wake juu ya suala hilo.
Baada
ya maelezo Jaji Ngwala akatoa nafasi kwa wakili aliyekuwa akimtetea Dk
Mwakyembe, Mpale Mpoki aliiomba mahakama imuamuru Mwanyamaki awalipe
gharama walizotumia tangu kesi ndogo ianze kulizikilizwa mahakamani
hapo.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Ngwala alisema ameridhika
na hoja ya wakili Mpoki, na kusema licha ya Mwanyamaki kushindwa kulipa
gharama hiyo na kesi kufutwa haina maana kwamba hatatakiwa kulipa
gharama nyingine.
“Mahakama inamtaka mdai (Mwanyamaki)
kulipa gharama zote kwa washtakiwa wote watatu aliowashtaki kwani ndiye
aliyeleta pingamizi hilo. Na kushindwa kwake kulipa kiasi cha Sh3
milioni tatu na kesi kuondolewa mahakamani hapa haimaanishi hatatakiwa
kulipa fidia hizo,” alisema Jaji Ngwala.
Katika hatua
nyingine, Jaji Ngwala alisema walalamikaji wengine walikamilisha
taratibu zote walizotakiwa ikiwamo kulipa Sh3 milioni, ili kesi ya
msingi ianze kusikilizwa kama ambavyo walioomba kwenye kesi ndogo ya
kuomba kupunguziwa gharama kutoka Sh5 milioni kwa kila mshtakiwa hadi
Sh1 milioni kwa kila mmoja.
Alisema Januari 7 kesi hizo
zitapangiwa majaji kwa ajili ya kuanza kusikilizwa, ambapo
walalamikaji, Liberatus Mwang’ombe wa Jimbo la Mbarali, John Mwambigija
wa Rungwe, wanatetewa na mawakili Benjamini Mwakagamba na Adrian Mhina,
Fanuel Mkisi wa jimbo la Vwawa anatetewa na mawakili Magreth Lyatuu na
Boniface Mwabukusi.
No comments:
Post a Comment