Aliyekuwa
mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa ataanza ziara ya kuzunguka
nchi nzima kuwashukuru Watanzania kwa kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu
wa Oktoba 25 na kesho atakuwa Tanga.
Katika
ziara hiyo, Lowassa ataambatana na viongozi waandamizi wa Chadema na
Ukawa kuwashukuru wananchi kwa namna walivyounga mkono upinzani na
ajenda nzima ya mabadiliko katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
Taarifa
kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya Habari na
Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene imesema kiongozi huyo atatoa
shukrani zake kwa wananchi kwa jinsi wanavyoendelea kuweka matumaini yao
kwa upinzani.
Taarifa
hiyo ilieleza kwamba wananchi bado wanaamini kwamba upinzani ndiyo
nguzo imara wanayoitegemea katika kuwaletea mabadiliko ya kweli kwa
ajili ya maendeleo yao na ustawi wa Taifa kwa ujumla.
“Wananchi
wanastahili shukrani kwa imani hiyo kubwa ambayo ni ishara ya wazi kuwa
matumaini yao kwa miaka mingine mitano yatasimamiwa na kuongozwa na
upinzani imara kupitia Ukawa,” alisema Makene katika taarifa hiyo.
Alisema
mbali na kupiga kura nyingi katika nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu
uliopita, wananchi waliwachagua wabunge wengi wa upinzani wanaotokana
na Ukawa. Alisema wabunge hao wameongeza nguvu kubwa ndani ya Bunge
hususan kupitia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo itakuwa serikali
mbadala.
Pia,
alisema wananchi wameviamini vyama vya upinzani ili kusimamia na
kuongoza halmashauri 34 nchi nzima, ikiwa moja ya misingi imara katika
kupigania mabadiliko ambayo Watanzania wanayataka.
No comments:
Post a Comment