Mwenyekiti
wa zamani wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema Rais wa Zanzibar, Dk
Ali Mohamed Shein ndiye mtu pekee mwenye uwezo wa kumaliza mgogoro wa
Zanzibar.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Profesa Lipumba alisema mgogoro wa Zanzibar
utamalizwa kwa Dk Shein kuiruhusu Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC)
kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25.
Alisema
pamoja na mazungumzo yanayoendelea kati ya CUF na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar (SMZ), Dk Shein ndiye mwenye uwezo kuumaliza mgogoro huo.
“Mazungumzo
yanaendelea na hatujui yatafika mwisho lini, lakini Dk Shein ndiye
anayeweza kuifanya Zanzibar iwe na amani au vurugu, ninashauri aruhusu
kutangazwa kwa matokeo,” alisema.
Alisema
amani na utulivu uliopo Zanzibar wakati wananchi wakisubiri hatima ya
mgogoro huo, haiwezi kuwa ya kudumu kwani ikiamuliwa uchaguzi urudiwe
wapo ambao hawatakubali.
Profesa
Lipumba alisema uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa huru na haki na hata
watazamaji wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali walishangaa matokeo yake
kufutwa.
Alisema
wananchi wa Zanzibar walishapiga kura na kwamba wanachosubiri ni
matokeo vinginevyo haki yao ya kidemokrasia itakuwa imechezewa.
Oktoba
28 mwaka huu, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha alifuta uchaguzi huo
kwa kile alichosema kulikuwa na kasoro ndani ya tume yenyewe na kwenye
vituo vya kupigia kura.
Profesa
Lipumba alisema mgogoro huo ukiendelea, utakwamisha msaada wa Dola za
Marekani 472.8 milioni uliokuwa utolewe na Shirika la Maendeleo ya
Milenia (MCC) la Marekani.
Alisema
Bodi ya MCC ilikutana Desemba 16 na kushindwa kupitisha msaada huo kwa
Tanzania huku hoja kubwa ikiwa kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu
Zanzibar.
Alisema miongoni mwa matumizi ya msaada huo ilikuwa kuunganisha wateja wapya 300,000 kupata umeme.
“Hapa
tunategemea busara za Dk Shein kuumaliza mgogoro ili tupate msaada huo
wenye masilahi ya Taifa au kuendelea na mgogoro na kuukosa msaada huo,” alisema.
Akizungumzia
suala hilo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya alisema
huu ni muda mwafaka kwa Dk Shein kuweka masilahi ya Wazanzibari mbele.
Alisema
atawekwa kwenye vitabu vya historia kama atafanya uamuzi wa kuruhusu
kutangazwa kwa matokeo hata kama viongozi wenzake wa CCM hawatapenda
uamuzi huo.
“Lakini
vurugu zikitokea, Shein atalaumiwa jumuiya za kimataifa yeye mwenyewe
na atashangaa viongozi wenzake wa CCM watakapojiweka pembeni,” alisema.
No comments:
Post a Comment