Kamanda Zahran Alloushi
Kiongozi
wa kundi la waasi la Jaish al-Islam nchini Syria Zahran Alloush ameuawa
katika shambulizi la ndege lililodaiwa kufanywa na serikali, likiwa pigo
kwa uasi wa karibu miaka mitano na mchakato wa amani unaoyumba.
Alloush
mwenye umri wa miaka 44 ndiye aliyekuwa kamanda mkuu wa kundi la Jaish
al-Islam, ambalo ndilo kundi la upinzani lenye nguvu zaidi katika ngome
ya waasi ya Ghouta Mashariki, iliyopo mashariki mwa mji mkuu wa Syria,
Damascus. Masaa kadhaa baada ya kuuawa kwa Alloush, wanachama waandamizi
wa Jaish al-Islam walimchagua Abu Himam al-Buwaydani kama mrithi wake,
liliarifu Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadaamu la Syria lenye makao
yake London, Uingereza.
Buwaydini
ni mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 40 na mpiganaji kutoka mkoa wa
Douma, ambaye anatokea katika familia yenye uhusiano wa karibu na kundi
la Udugu wa Kiislamu, alisema Mkurugenzi wa shirika hilo la uangalizi wa
haki za binaadamu lenye makao yake makuu mjini London.
Alloush
na makamanda wengine watano waliuawa katika shambulizi la angani
lililoulenga moja ya mikutano yao uliyofanyika Ghouta Mashariki siku ya
Ijumaa, lilisema shirika hilo na kuongeza kuwa haikuwa bayana nani
alifanya shambulizi hilo kati ya serikali ya Assad na Urusi.
Syria yadai kumuuwa
Mwanachama
mwandamizi wa Jaish al-Islam alilithibitishia shirika la habari la AFP
juu y akifo cha Alloush, na kusema ndege tatu ziliushambulia mkutano huo
wa siri wa makamanda. Serikali ya Syria inalitaja kundi la Jaish
al-Islam kama kundi la kigaidi, na televisheni ya serikali ilirejelea
matamshi hayo wakati ikitangaza kifo cha Alloush, ikisema jeshi la Syria
limeendesha operesheni maalumu iliyomuua Alloush kama sehemu ya "lengo
lake la kitaifa."
Chanzo
kutoka duru za usalama za Syria kililiambia shirika la AFP kuwa dazeni
kadhaa za waasi waliuawa katika mashambulizi yaliyofanywa na vikosi vya
serikali ya Syria kwa kutumia makombora mapya yaliyotolewa na Urusi.
Ndege
hizo zilifanya mashambulizi mawili dhidi ya mkutano huo, kila mmoja
likiwa na makombora manne, kilisema chanzo hicho cha habari. Wanachama
wasiopungua 12 wa Jaish ai-Islam pamoja na wengine saba kutoka kundi la
Ahrar al-Sham waliuawa.
Kundi la
Jaish al-Islam ndiyo lenye nguvu zaidi katika mkoa wa Ghouta Mashariki,
ambao ni ngome ya waasi mashariki mwa mji mkuu inayoshambuliwa mara kwa
mara na ndege za utawala wa Assad. Likiungwa mkono na Saudi Arabia,
kundi hilo lilishiriki hivi karibuni katika mazungumzo ya waasi mjini
Riyadhi, yaliyokuwa na lengo la kuyaunganisha makundi hayo kuelekea
mazungumzo ya amani na serikali.
Historia yake
Zahran
Alloush alizaliwa 1971 mjini Douma, moja ya miji mikubwa zaidi katika
mkoa wa Ghouta Mashariki. Baba yake alikuwa mhubiri mashuhuri wa Salafi
ambaye kwa sasa anaishi mjini Riyadh. Akifuata katika nyayo za baba
yake, Alloush alipata masomo ya dini nchini Syria na Saudi Arabia.
Alloush
alikamatwa mwaka 2009 na aliachiliwa Juni 2011 katika msamaha wa jumla,
miezi mitatu tu baada ya kuanza kwa uasi wa Waysria dhidi ya utawala wa
rais Bashar al-Assad. Alijiunga na uasi na mwaka 2013 aliunganisha
makundi kadhaa ya waasi chini ya kundi la Jaish al-Islam.
Kundi
hilo lilijipata umaarufu Ghouta Mashariki na limeendeleza upinzani
usiyoyumba dhidi ya Assad na kundi la Dola la Kiislamu. Lakini
limekosolewa pia kwa ukiukaji wa haki za binaadamu. Mwezi Julai
walilaaniwa kwa kuwauwa watu 18 wanaodaiwa kuwa wanachama wa Dola la
Kiislamu katika maknda wa video unaoigiza mikanda ya kikatili ya kundi
hilo la IS.
Na kwa
mujibu wa shirika la uagalizi wa haki za binaadamu la Syria, mwezi
Novemba Jaish al-Islam iliwatumia mateka kadhaa kama ngao katika vizimba
vya chuma katika jitihada za kuzuwia mashambulizi ya utawala katika
mkoa wa Ghouta Mashariki.
Habari za
mashambulizi yaliyomuua Alloush zilisambaa haraka miongoni mwa
wanaharakati na makundi ya waasi kupitia mtandaoni. "Tunamuomba Mungu
amkubali kamanda Zahran Alloush kama shahidi--- na tunaviombea vikundi
vya Ghouta viunganye ili kuziba mianya na kukamilisha kazi," aliandika
Khalid Khoja, kiongozi wa muungano wa taifa wa upinzani kwenye ukurasa
wake wa twita.
Pigo kubwa kwa vuguvugu la waasi
Wachambuzi
wanataraji kifo cha Alloush kuwa na athari kubwa kwenye vuguvugu la
waasi lililogawanyika na pia mchakato unaoandaliwa wa mazungumzo ya
amani. "Kifo chake kinasimama kama moja ya hasara kubwa zaidi kwa
upinzani katika uasi huo wa karibu miaka mitano," alisema mchambuzi
Charles Lister kwenye ukurasa wake wa twita.
"Katika
njia moja, Zahran Alloush amekuwa kiongozi adim mwenye mafanikio katika
vuguvugu la waasi wa Syria," alisema Aron Lund, mhariri wa mtandao
unaoripoti kuhusu mgogoro waSyria wa Carnegie Endowment. Kutokuwepo
kwake kunaweza kuathiri mchakato dhaifu wa mazungumzo ya Syria
yanayonuwia kutafuta suluhilo la kisiasa kwa mgogoro huo uliyouwa watu
zaidi ya 250,000.
Jaish
al-Islam lilikuwa moja ya makundi makuu ya waasi yaliyoalikwa mjini
Riyadh kwa mazungumzo mapema mwezi huu. Lilikubaliana juu ya kufanya
mazungumzo huko mbeleni na utawala wa Syria, hatua iliyoyakasirisha
makundi yenye msimamo mkali kama vile kundi la Al-Nusra Front.
"Mazungumzo
hayo yanahitaji ushiriki wa watu wenye msimamo mkali kama Zharan
Alloush ili kupata uhalali," alisema Lund. Lakini kifo cha Alloush
huenda kikaathiri mchakato wa amani, kwa kulivurga kundi la Jaish
al-Islam na pia kulidhoofisha.
No comments:
Post a Comment