Muda
mfupi baada ya Bodi ya MCC kutoa taarifa inayoonesha Tanzania haitapata
msaada kutoka shirika hilo kama ilivyotarajiwa kwa ajili ya mwaka 2016,
Mwenyekiti wa Chama (T), Freema Mbowe ametoa kauli nzito juu ya suala
hilo akisema kuwa kuchelewa kupatikana kwa fedha za MCC si tu kunachafua
jina la nchi na hadhi yake katika medani za kimataifa, bali kutaathiri
kwa kiasi kikubwa miradi yote iliyo chini ya ufadhili wa MCC.
MCC
imeahirisha msada huo wa USD Mil. 472.8 ambazo ni takriban trilioni
moja kwa fedha za Tanzania zilizolengwa kusaidia sekta ya nishati ya
umeme hususan ule wa vijijini, katika kuunganisha wateja wapya,
mabadiliko ya kimuundo ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO) ili lifanye
kazi na kutoa huduma kwa ufanisi katika sehemu za uzalishaji,
usafirishaji na usambazaji.
Fedha hizo pia zilikusudiwa kusaidia kuanza kwa mpango mkubwa wa kuboresha sekta ya umeme nchini.2014-2024.
Mbowe
amemtaka Rais John Magufuli kuchukua hatua za haraka za kiuongozi
kumaliza mtanziko wa kisiasa Zanzibar kwa mshindi wa nafasi ya urais
kutangazwa kutokana na uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba, mwaka huu.
Aidha
amesema kuwa Sheria ya makosa ya mtandao (Cyber Crime Act 2015) ambayo
ni mojawapo ya sababu zilizotumiwa na MCC kuahirisha msaada huo kwa
Tanzania hadi itakapokuwa imefanyiwa kazi, ni sheria mbaya sana
inayokinzana na kukua kwa technologia ya habari na mawasiliano na kuzuia
upashanaji wa habari miongoni mwa jamii ambayo ililenga kuweka makosa
ya kijinai ili kudhibiti wapinzani wa CCM katika uchaguzi mkuu na
kukipatia mazingira ya ushindi chama hicho.
"Sasa
imethibitika kuwa Bodi ya MCC iliyokaa tarehe 16 Dec 2015 imeahirisha
rasmi kuidhinisha msaada wa Millenium Challenge uliokuwa umekusudiwa kwa
Tanzania kwa mwaka wa fedha 2016. Sababu kuu mbili zilizosababisha
uamuzi huo ni:
1. Mkwamo wa Uchaguzi wa Rais na Wawakilishi Zanzibar na
2.Matumizi
mabaya ya she ria ya makosa ya mtandao hususan kuhusiana na uchaguzi
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa 2015."
"Ubabe
wa baadhi ya viongozi wa CCM ni janga la Taifa. Kuchelewa kupatikana
kwa fedha za MCC si tu kunachafua jina la nchi na hadhi yake katika
medani za kimataifa, bali kutaathiri kwa kiasi kikubwa miradi yote iliyo
chini ya ufadhili wa MCC," amesema Mwenyekiti Mbowe na kuongeza;
"Sheria
ya makosa ya mtandao (Cyber Crime Act 2015) ni sheria mbaya sana
inayokinzana na kukua kwa technologia ya habari na mawasiliano. Aidha,
kwa makusudi kabisa inafifisha uhuru wa kupashana habari na ni dhahiri
ilitungwa kwa nia mbaya ya kuthibiti kijinai uchaguzi mkuu.
"Tuliipinga
sheria hii Bungeni na ikapitishwa usiku wa manane kwa ubabe wa wabunge
wa CCM na hata tulipomtaka rais Kikwete asiisaini aliisaini kibabe
akijua anaandaa mazingira gani ya "kihalifu", " amesema Mwenyekiti Mbowe.
Ameongeza
kusema kuwa sheria hiyo ilitumika kuvamia vituo vya CHADEMA vilivyokuwa
vikitumika kukusanya matokeo ya kura za rais na wabunge na hadi leo
vijana zaidi ya 161, wakiwemo wanafunzi, wana kesi za "kubumba"
mahakamani.
Mwenyekiti
Mbowe amesema kuwa Sheria hiyo hiyo ilitumika kuficha dhana ovu
iliyotumika kuhalalisha kuvamia Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC) kilichokuwa kikiratibu watazamaji wa uchaguzi wa ndani kwa kibali
cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
"Vile
vile Sheria hii imetumika kuwakamata na kuwaweka ndani na hata
kuwanyima dhamana vijana wetu ambao walituunga mkono katika uchaguzi
mkuu.
"Namtaka rais Magufuli achukue hatua za kiuongozi na kiutawala kwa kufanya yafuatayo:
"Kwanza aumalize mgogoro wa kisiasa Zanzibar kwa kuhakikisha kuwa mshindi halali anatangazwa.
"Pili
achukue hatua ya kuifanyia marekebisho makubwa Sheria ya makosa ya
mtandao katika bunge lijalo. Aidha wale wote waliobambikiwa kesi
amuamuru DPP kuzifuta kesi hizo mara moja," amesema.
Mwenyekiti
Mbowe amesisitiza kuwa Rais Magufuli hana budi kuchukua hatua hizo za
haraka ili kulinusuru taifa na hasara ya kupoteza mabilioni hayo ya MCC
na zaidi kuepusha kuporomoka zaidi kwa biashara ya utalii nchini
Zanzibar.
Amesema
katika taifa ambalo sekta ya umeme inakabiliwa na matatizo makubwa
katika uzalishaji, usambazaji na usafirishaji huku wananchi wa kipato
cha chini wakibebeshwa mzigo mkubwa wa kumudu nishati hiyo na wengine
wakilazimika kutumia nishati mbadala kama mkaa unaotokana na miti hivyo
kusababisha uharibifu wa mazingira, serikali inayojua wajibu wake yenye
viongozi wanaothamini uwajibikaji, haikupaswa kushindwa kuchukua hatua
stahiki kutimiza vigezo vya msaada huo ambao umeshaisaidia Tanzania
katika miradi mingine kadhaa.
Imetolewa Ijumaa, Desemba 18, 2015 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
No comments:
Post a Comment