Mbunge
wa jimbo la Kibamba, John Mnyika amekosoa uamuzi wa Rais John Magufuli
wa kuhamishia wizara inayohusu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi) chini ya ofisi yake, akidai kitendo hicho kimelenga kuvibana
vyama vya upinzani ambavyo vimeshinda halmashauri nyingi nchini.
Mnyika
(pichani) aliyasema hayo jana wakati akitoa shukrani zake kwa wananchi
wa Kata ya Salanga iliyopo Kimara kwa kumchagua kuwa mbunge wao.
Alieleza kushangazwa na mabadiliko yanayofanywa na Dk Magufuli tangu
alipoingia madarakani.
Mbunge
huyo alisema Chadema na vyama vingine vya upinzani vimeshinda katika
uchaguzi wa nafasi za umeya na uenyekiti katika halmashauri mbalimbali
nchini, jambo hilo limemfanya Rais kuiweka Tamisemi chini yake ili
kupunguza uhuru wa halmashauri zinazoongozwa na upinzani katika kuleta
maendeleo.
“Katika
halmashauri za Dar es Salaam bado tunavutana, wanaleta madiwani wa viti
maalumu kutoka Zanzibar kuja kupiga kura huku bara. Tunawaambia
hatutakubali kwa sababu Chadema na Ukawa inaongoza kwa viti vingi vya
udiwani, lazima tuongoze jiji hili,” alisema.
Mnyika
aliongeza kuwa “Rais Magufuli amefanya kama alivyofanya Benjamini Mkapa
wakati wa utawala wake kwa kutaka kutawala kibabe. Hatafika mbali kwa
sababu ameshindwa kujenga mifumo thabiti, badala yake amebaki kuhimiza
usafi wa siku moja,” alisema.
Kiongozi
huyo ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa Chadema, alimtaka Rais Magufuli
kujenga misingi ambayo itajiendesha yenyewe bila uwepo wake. Alimtaka
pia kuweka msimamo thabiti wa kutengeneza Katiba mpya kwa kufanyia kazi
maoni ya wananchi.
No comments:
Post a Comment