Na Beatrice Lyimo-Maelezo
Asilimia
49 kati ya asilimia 100 ya matokeo ya uchunguzi wa makosa ya vinasaba
(DNA) yanayowasilishwa katika ofisi ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu
wa Serikali kwa mwaka yanaonyesha kuwa baba si mzazi halali wa mtoto
katika kesi hizo.
Hayo
yamesemwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele alipokuwa
akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano wa wadau
wa wakala wa afya ya mazingira leo jijini Dar es Salaam.
“Kesi
zinazopokelewa katika maabara yetu zinazohusu sampuli ya Vinasaba kwa
mwaka zinaonyesha kuwa asilimia 49% kati ya asilimia 100% ya matokeo
hayo huonyesha mzazi mmoja ambaye ni baba kuwa si mzazi halali wa mtoto
huyo”.
“Vinasaba
ni utambulisho wa kipekee wa kila kiumbe ambao unabeba taarifa muhimu
na inayorithisha tabia au umbile fulani la mhusika. Vinasaba ni kama
vile kitabu cha kumbukumbu kinachohusu maisha binafsi”, aliongeza Prof. Manyele.
Profesa
Manyele aliongeza kuwa mikoa ya kanda ya Ziwa, Arusha, Dar es Salaam na
Mbeya ndio inayoongoza kwa matokeo ya uchunguzi huo wa makosa ya
Vinasaba nchini.
Akizungumza
kuhusu lengo la mkutano huo, Profesa Manyele alisema kuwa ni kuimarisha
uhusiano uliopo kati ya wadau wa kemikali na wadau wa afya ya mazingira
kutoka katika halmashauri tofauti nchini pamoja na ofisi ya Mazingira.
Aidha
Profesa alibainisha baadhi ya majukumu yanayofanywa na wakala wa Mkemia
Mkuu wa Serikali kuwa ni kufanya uchunguzi ili kuhakiki ubora na
usalama wa vyakula, dawa, maji, maji machafu, bidhaa za viwanda na
mashambani, sampuli za mazingira na sampuli zinazohusiana na makosa ya
jinai.
“Matokeo
ya uchunguzi wa makosa ya jinai na vinasaba (DNA) huviwezesha vyombo
husika kufikia maamuzi stahili na kusaidia kutendeka kwa haki katika
tuhuma za kesi za jinai ikiwemo ulevi, mauaji, ubakaji, wizi wa watoto,
uhalali wa mtoto kwa mzazi, kwa kupitia vyombo husika” alifafanua Profesa.
Mbali
na hayo, alisema wakala kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatarajia kuwasilisha mapendekezo ya
kutunga sheria ya kuunda maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Sheria
ya kusimamia taaluma ya Wakemia, kuimarisha upatikanaji wa mitambo na
vifaa vya maabara kila teknologia inapobadilika pamoja na kuimarisha
zaidi taratibu za uchunguzi ziwe za kisasa ili kuendana na mabadiliko ya
sayansi na teknologia.
No comments:
Post a Comment