Burundi: wapiganaji 3 wauawa katika shambulizi dhidi ya afisa wa polisi - LEKULE

Breaking

5 Dec 2015

Burundi: wapiganaji 3 wauawa katika shambulizi dhidi ya afisa wa polisi

Polisi ya usalama wa taasisi za uongozi wa nchi ikipiga doria katika moja ya mitaa ya wilaya ya Ngagara, jijini Bujumbura, Aprili 27, 2015.
Na RFI
Washambuliaji watatu wameuawa na wengine wawili wamekamatwa leo Ijumaa mjini Bujumbura baada ya kuendesha shambulizi dhidi ya gari la afisa mwandamizi wa polisi, ambaye hakuwa katika gari hilo, chanzo cha polisi kimebaini.
Washambuliaji watano wakivalia sare ya polisi wa usalama wa taasisi za uongozi wa nchi (API), wameshambulia kwa roketi na risasi nyingi gari la jenerali Christophe Ndayishimiye, mkuu wa vitengo maalumu vya polisi katika barabara kuu inayogawa wilaya za Bwiza na Buyenzi (boulevard du Peuple Murundi) mjini Bujumbura, afisa wa polisi wa cheo cha juu ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia shirika la habari la Ufaransa la AFP.
"Vikosi vya usalama viliingilia kati mara moja (...) wapiganaji watatu wameuawa, wawili wako mikononi mwa polisi na silaha kadhaa zimekamatwa", kimesema chanzo hicho na kuongeza kuwa jenerali Ndayishimiye hakuwa katika gari lililolengwa na hakuna aliyejeruhiwa miongoni mwa askari polisi waliokua katika gari hilo.
Kwa mujibu wa afisa wa Idara ya Ujasusi (SNR), washambuliaji walikuwa ni "raia wa kawaida ambao walijifananisha na askari polisi wa API, wala hawakua askari polisi wa kiengo hicho".
Jenerali Ndayishimiye, ambaye anajulikana kwa jina la utani "Wakenya" (ikimaanisha"mtu mlemavu"), ni mpiganaji wa zamani kutoka kundi la zamani la waasi la CNDD-FDD katika vita viliyodumu zaidi ya mwongo mmoja (1993-2006).
Jenerali "Wakenya" ni mmoja wa watu muhimu waliohusika katika ukandamizaji wa watu walioandamana kwa muda wa wiki sita dhidi ya awamu ya tatu ya Rais Nkurunziza, mwishoni mwa mwezi Aprili, kisha machafuko yalizuka na kuongezeka tangu rais Pierre Nkurunziza alipochaguliwa katika uchaguzi uliosusiwa na upinzani na baadhi ya vigogo wa chama madarakani cha CNDD-FDD, ambao walilazimika kukimbilia nje ya nchi.
Ni mtu wa tano muhimu katika utawala ulio madarakani - na afisa mwandamizi wanne katika vikosi vya ulizi na usalama kulengwa na mashambulizi ya kuvizia tangu uchaguzi huo.
Mtu muhimu na mmoja kati ya vigogo wa vikosi vya usalama, jenerali Adolphe Nshimirimana, aliuawa Agosti 2 mjini Bujumbura katika shambulizi la roketi, wakati ambapo mkuu wa majeshi, jenerali Prime Niyongabo, alinusurika kuuawa katika shambulizi lililoendeshwa mwezi Septemba, shambulizi ambalo liligharimu maisha ya walinzi wake 7.
Mwishoni mwa mwezi Novemba, Kanali Serge Kabanyura, Kamanda wa kanda ya tano ya kijeshi, magharibi mwa Burundi, alijeruhiwa katika shambulizi lililoendeshwa kilomita ishirini Kusini Mashariki mwa mji wa Bujumbura, siku moja baada ya kulengwa kwa risasi mjini Bujumbura, Zéno Ndaruvukanye, mjumbe wa bodi ya uongozi ya chama tawala cha CNDD-FDD.

Mapigano kati ya vikosi vya usalama na wapiganaji yamekua yakishuhudiwa karibu kila siku mjini Bujumbura.

No comments: