Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwasili mtaa wa Mlandege
kukagua kiwanja cha nyumba ya Ghorofa kinacholalamikiwa na Wakaazi wa
Mtaa huo kwamba kimevamia pia eneo la wazi linalotumika kwa shughuli za
Kijamii.
Mmiliki
wa Kiwanja cha nyumba ya Ghorofa Mlandege Bwana Anuari Abdullah
akijitetea kupata kibali kinachomruhusu kuendeleza ujenzi wa nyumba
yake.
Baadhi
ya Wakaazi wa Mtaa wa Mlandege wakitafakari na kufurahia maamuzi
yaliyochukuliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ya
kuzuia ujenzi wa jengo la Ghorofa kwa kukosa taratibu zinazozingatia Mji
mkongwe wa Zanzibar.
MAKAMU
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amemuagiza Mkurugenzi
wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } kufanya uchunguzi wa kina na
kuwachukulia hatua za nidhamu kwa mujibu wa sheria watendaji wa Mamlaka
hiyo wanaotumia dhamana yao katika kusimamia huduma za maji kwa njia ya
kuwanyanyasa Wananchi.
Alisema
zipo dalili za wazi zinazoonyesha kwamba baadhi ya Watendaji wa Mamlaka
hiyo wanatekeleza majukumu yao ya kazi kwa kuendesha utashi wao binafsi
zaidi wa kisiasa.
Balozi
Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati akiwapa pole Wananchi wa Shehia
ya Dole Wilaya ya Magharibi “B” mara baada ya kukagua mifereji ya huduma
za Maji safi na Salama ya wananchi wa Shehia hiyo ambayo ilikatwa na
mengine kung’olewa kabisa vianzio vyake kufuatia operesheni iliyofanywa
na watendaji wa Mamlaka hiyo.
Opereshi
hiyo ya Tarehe 22 Oktoba iliyoathiri nyumba 24 zenye familia 22
ililalamikiwa na Wananchi hao kwa vile ilitekelezwa siku mbili tu kabla
ya Uchaguzi Mkuu wa Tarehe 25 Mwezi Oktoba mwaka huu ikionyesha wazi
kuwa baadhi ya watendaji wa Mamlaka hiyo waliweka utashi wao wa Kisiasa.
Balozi
Seif alisema Tabia iliyofanywa na baadhi ya Watendaji hao wa Zawa ya
kuendesha operesheni hiyo kwa kumsingizia yeye ndie aliyeagiza
kutekelezwa ilikuwa na lengo la kumchafua kisiasa.
Alisema
hilo ni jambo linaloonekana kupangwa maalum ndani ya kipindi cha
kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu ambalo si vyema likachanganywa pamoja kati
ya huduma za Kijamii na itikadi za Kisiasa.
Akiwapa
pole Wananchi hao wa Dole kwa kukosa huduma za maji safi aliwataka
watendaji wa Mamlaka ya Maji kuhakikisha kwamba huduma hiyo katika
Shehia ya Dole inarejeshwa tena kama kawaida ndani ya kipindi cha wiki
mbili zijazo.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } Dr. Mustafa Garu
aliahidi kutekeleza agizo hilo na kuwaeleza Wananchi hao kwamba Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar inachokifanya kwao ni kuwataka wachangie
huduma za Maji safi na salama ili kuiwezesha Mamlaka hiyo ipate nguvu
zaidi za kuimarisha miundo mbinu yake.
Alisema
takwimu ziko wazi zikionyesha kwamba Serikali Kuu imekuwa ikibeba
gharama za upatikanaji wa huduma za Maji safi na salama kwa zaidi ya
asilimia 65% wakati punguzo lililobaki la asilimia 35% tu huomba
kuchangiwa na Wananchi.
Wakati
huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
amemuagiza Mmiliki wa Kiwanja kinachotaka kujengwa Nyumba ya Ghorofa
katika Mtaa wa Mlandege Bwana Anuari Abdulla kusitisha mara moja ujenzi
huo.
Hatua
hiyo ya Balozi Seif imekuja kufuatia malalamiko makubwa yaliyotolewa na
wakaazi wa Mtaa huo wakimshutumu Mmiliki huyo kuvamia pia eneo la wazi {
Open Space } la shughuli za kijamii katika sehemu hiyo.
Balozi
Seif alimuonya Mmiliki huyo kwamba endapo ataendelea kukaidi agizo
alilopewa na Mamlaka Nne zinazosimamia na kushughulikia masuala ya
Ujenzi Serikali italazimika kumchulia hatua za kisheria dhidi yake.
Alifahamisha
kwamba wakaazi wa Mtaa wa Mlandege ambao wanaishi ndani ya eneo la Mji
Mkongwe lililopata hadhi ya kuwa Urithi wa Kimataifa wanapaswa
kuzingatia matakwa yaliyokubalika katika uhifadhi wa Mji huo wa
Kihistoria.
Mapema
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe wa
Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar kwamba Mmiliki wa kiwanja hicho amekuwa akikaidi maamuzi
anayopewa kuyatekeleza na mamlaka husika katika ujenzi huo.
Nd.
Sarboko alisema Bwana Anuari ameamua kuendeleza ujenzi huo kwa kutumia
kibali alichopewa na Mmoja wa Afisa wa Baraza la Manispaa ambacho tayari
kimeshafutwa kwa vile kinakiuka na kutozingatia sheria na taratibu
zilizowekwa.
Alisisitiza
kwamba Mmiliki huyo tayari ameshaonywa na Viongozi wa Taasisi Nne
waliokutana kujadili suala hilo na kumtaka asubiri maamuzi ya pamoja
yatakayotolewa baada ya kuzingatia hali halisi ya namna
yatakavyozingatia matakwa na haki ya kila upande unaohusika.
Alimtaka
Mmiliki huyo kuhakikisha kwamba mabati yaliyowekwa kufunga eneo la wazi
lililokuwa likitumika kwa wapita njia pamoja na kutumika kwa shughuli
za Kijamii anayaondoa mara moja vyenginevyo watendaji wa Mamlaka hiyo
watalazimika kutekeleza amri hiyo kwa kutumia kijiko katika kipindi
kifupi kijacho.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
10/12/2015.
No comments:
Post a Comment