Viongozi wa Chadema Mkoa wa Rukwa waliotangaza kujiuzulu nyadhifa zao ndani ya chama hicho hivi karibuni, wamesitisha uamuzi wao na kurejea madarakani.
Mratibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Frank Mwaisumbe alisema hayo juzi wakati akizungumza na mwandishi wetu kwa njia ya simu kutoka mkoani Mbeya.
Mwaisumbe alisema wamekubaliana na viongozi hao kurejea katika nyadhifa zao za kisiasa ndani ya chama hicho.
Alisema
kikao baina ya viongozi wa Chadema wa kanda hiyo na waliotangaza
kujiuzulu kilidumu kwa zaidi ya saa 11 juzi na kufikia uamuzi wa kurejea
madarakani kwa viongozi hao.
Akizungumzia
sababu za kujiuzulu kwa viongozi hao ambazo ni kutolipwa fedha mawakala
wa wagombea wa chama hicho mkoa na kutoridhishwa na uteuzi wa mgombea
ubunge wa viti maalumu, Aida Kenan, alidai zina mashiko lakini kabla ya
kutangaza katika vyombo vya habari kuachia ngazi walipaswa kuwasiliana
na uongozi wa juu wa chama.
Aliongeza
kuwa, mathalan katika suala la mawakala kulikuwa na fomu maalumu ambazo
wagombea walizijaza kuonyesha kuwa wanaweza kubeba gharama zote za
mchakato wa uchaguzi au la.
Alisema
wagombea waliojaza fomu kuonyesha hawana uwezo wa kuwalipa mawakala,
chama kilibeba gharama hizo na fedha zilitolewa kwa kila mgombea kwa
kuwa wao ndiyo walijua nani ni wakala na fedha hizo hazikupelekwa kwa
viongozi wa mkoa kama inavyodaiwa.
Kuhusu
uteuzi wa Kenan katika nafasi ya ubunge wa viti maalumu, alisema jina
lake lilitokana na maombi ya Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) ambao
walikuwa na nafasi mbili, lakini hakutokana na kura ambazo wagombea wa
Chadema walipata kwenye Mkoa wa Rukwa.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti viongozi wa mkoa ambao awali walijiuzulu,
Mwenyekiti Zeno Nkoswe na Katibu Ozem Chapita walikiri kukubali kurejea
madarakani baada ya kufanya kikao na viongozi wa chama hicho Kanda ya
Nyanda za Juu Kusini.
“Nimeafiki
kurejea katika wadhifa wangu wa uenyekiti wa mkoa, lakini bado
nawasubiri na viongozi wa kitaifa kuna mambo tuyaweke sawa. Si unajua
wao wanatutuhumu kwamba tulikimbilia kwenye vyombo vya habari na sisi
tuna hoja zetu,” alisema Nkoswe.
Baada
ya makubaliano na viongozi hao walifanya kikao na madiwani
waliochaguliwa kupitia chama hicho, ili kuhakikisha wanaongoza
Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga. Chadema ina viti 10 kati ya 19
vya udiwani.
No comments:
Post a Comment