Aliyekuwa mgombea Urais wa Chadema, Edward lowassa, amelitaka jeshi la Polisi nchini kuwachukulia hatua wale wote wanadaiwa kumuua, aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo na kwamba kama hawatafanya hivyo, watachukua hatua wao wenyewe.
Kauli
hiyo ameitoa ikiwa ni siku mbili sasa tangu Mahakama Kuu Kanda ya
Mwanza, kutoa hukumu kwa chama hicho kikuu cha upinzani kumuaga na
kumzika Marehemu Mawazo bila kuingiliwa na mtu yeyote.
Marehemu
Mawazo, alifariki Novemba 14 mwaka katika kijiji na kata ya Katoro,
wilaya na Mkoa wa Geita kwa kukatwa mapanga na watu wanaosadikiwa kuwa
ni wafuasi wa CCM.
Lowassa
ametoa kauli hiyo leo wakati akitoa salamu za rambirambi katika ibada
ya kuaga mwili wa Mawazo kwenye uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.
Lowassa
ambaye alikuwa mgombea wa Chadema na kuungwa mkono na vyama vya Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) amesema polisi wasipochukua hatua kwa
waliomuua marehemu Mawazo watajichukulia hatua wao.
Amesema
kuwa watu waliomuua Mawazo wanafahamika majina yao lakini Polisi kwa
kushirikiana na Chama cha Mapinduzi (CCM) wameshindwa kuwachukulia hatua
zozote zile mpaka sasa.
“Hawa
Polisi wanafanya mambo yao kiimra-imra, kiujanja ujanja, wao wameleta
magari ya washawasha yaliyonunuliwa kwa Dola za Kimarekani 282 milioni,
hawana nama ya kuyatumia, wameamua kuwachokoza wananchi ili waweze
kuyatumia.
“Wananchi
nawaomba sisi tuache vurugu ili sasa hayo magari yao walionunua tuone
watakavyo yatumia, wananua magari alafu shuleni hakuna madawati na
barabara hakuna,” amesema Lowassa.
Pia
amesema baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kutoa haki kwa familia na
chama hicho kumuaga Mawazo, imeonekana jeshi la polisi halina
intelejensia wanayodai bali ni waongo watupu.
Lowassa
amesema hukumu ya Jaji Lameck Mlacha wa Mahakama Kuu, iwe somo kwa
polisi wa Tanzania kutokana na kujawa wivu usiofahamika.
Freeman Mbowe
Mwenyekiti
wa chama hicho, Freeman Mbowe, akizungumza katika shughuli hiyo ya
kuaga mwili huo, amesema haki imepatikana mahakamani na kuwaumbua
polisi.
“Wananchi
wamechoka kuuliwa kama ilivyotokea kwa wafuasi wa Chadema tangu mwaka
2011 mpaka sasa wakati huu wa Mawazo…tumechoka kufa, mwenye akili na
afahamu,” amesema Mbowe.
Hata
hivyo, amesema wapo baadhi ya askari polisi wema na wenye kutekeleza
weledi wa kazi zao kiufasaha, lakini wapo ambao hawafai kuwatumikia na
kuwaongoza wananchi.
Aidha,
aliwashukuru watu wote waliojitolea kuisaidia familia ya Marehemu
Mawazo hasa mtoto wake Precious Mawazo (9) anayesoma darasa la nne
akiwamo Lowassa pamoja na wabunge 113 wanaotoka vyama vya Ukawa, kwa
kila mmoja kujitolea Sh. 300,000 na kupatikana 36 milioni.
Katika
hatua nyingine, Mbowe amesema chama hicho kinajiandaa kumfungulia
mashitaka ya madai Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo,
baada ya kuweka zuio la mwili wa Mawazo kutoagwa jijini Mwanza hadi
Mahakama Kuu ilipotupilia mbali zuio hilo.
“Kamanada
Mkumbo lazima alipe gharama zote za siku nane za kumweka Lowassa,
Sumaye, Mbowe na wabunge zaidi ya 50 jijini Mwanza wakisubiri mahakama
itende haki na hatimaye kushinda kesi,” amesema mwenyekiti Mbowe.
Frederick Sumaye
Waziri
Mkuu mstaafu wa serikali ya awamu ya tatu, Frederick Sumaye, amesema
nchi yetu awali ilikuwa inasifiwa kwa amani na utulivu, lakini sasa
inawaua watu wanaodai haki.
“Hii
ni kama ilivyokuwa Afrika Kusini wakati wa utawala wa Makaburu,
mpigania haki Steve Bicco, aliuawa kama alivyouawa Mawazo, lakini mwisho
wake makaburu hao walitoa haki kwa waliowengi licha ya kuwa na bunduki
na polisi wengi kuliko kwetu,” amesema Sumaye.
Sumaye
amesema Marehemu Mawazo alikuwa akidai haki majukwaani, lakini watu
waliotaka kudaiwa haki waliamua kumuua huku vyombo vya dola
vikipindapinda ili haki isipatikane kwa amani.
“Lazima tusimamie amani na tupinge kuonewa maana ipo simu moja watu watachoka kuonewa kama ilivyo sasa,” amesema.
Mtoto wa Mawazo
Mtoto
wa marehemu Mawazo, Precious Mawazo (9), amesema waliomuua baba yake
hawajakatisha ndoto yake ya kuwa mwanasiasa kwani siku moja atakuwa
mwanasiasa mkubwa.
“Wakati
wa uhai wa baba, ndoto yangu ilikuwa niwe mwanasiasa, lakini
nitaendelea na hiyo ndoto hadi niwe mwanasiasa mkubwa nchini…katuacha na
mdogo wangu akiwa na miaka miwili tunaamini Mungu atatusaidia,” amesema Precious.
Godbless Lema
Godbless
Lema wa Arusha akitoa salamu za rambirambi uwanjani hapo, amesema
marehemu Mawazo alikuwa rafiki yake wa damu tangu akiwa jijini Arusha na
kumshawishi kuingia kwenye siasa, lakini aliuliwa kinyama na watu
wasiopenda haki.
Lema
amesema ukimya wa wananchi katika mauaji wanayofanyiwa, si uoga bali ni
unatokana na uchungu walionao, kwani wauaji wakiwa huru hakuna
atakayekuwa salama.
Mchungaji Swai
Mchungaji
Bernard Swai wa kanisa la Winners jijini Mwanza, akihubiri katika misa
ya kumuaga, amesema wanadamu hawajumbwa na Mungu kwa ajili ya kuuana
bali kupendana.
“Lazima
wanadamu wajiulize kwanini vijana wengi wanatumiwa ili kuwaua wengine,
tunaiomba serikali iliyopo madarakani isimamie na kukomesha kabisa
mauaji yasiyo na hatia,” amesema Mchungaji Swai.
Amesema
damu ya Mawazo inalia mbele ya Mungu na wale waliofanya kitendo cha
kinyama kwa mtu huyo macho ya Mungu yanamuona popote alipo.
Hata
hivyo wengine waliotoa salamu za rambirambi ni Baraza la Vijana Taifa
(Bavicha), Baraza la Wanawake (Bawacha) na chama cha NCCR Mageuzi
kilichosimama kuwakilisha vyama vinavyounda Ukawa (CUF na NLD).
Mpekuzi blog
No comments:
Post a Comment