Dar es Salaam.
Agizo la Rais John Magufuli la kusitisha safari za nje linakabiliwa na ugumu katika utekelezaji wake kutokana na nchi kuwa na balozi 36 tu ambazo zitatakiwa kufanya kazi maeneo mbalimbali duniani.
Agizo la Rais John Magufuli la kusitisha safari za nje linakabiliwa na ugumu katika utekelezaji wake kutokana na nchi kuwa na balozi 36 tu ambazo zitatakiwa kufanya kazi maeneo mbalimbali duniani.
Muda mfupi baada ya
kuapishwa na kuanza utekelezaji wa majukumu yake ya mkuu wa nchi, Rais
alifuta safari zote za nje kwa watumishi wa Serikali na viongozi ili
kuokoa fedha zinazotumika kwa ajili hiyo na kuagiza shughuli hizo
zifanywe na mabalozi.
Rais alisema safari hizo
zitadhibitiwa na Ikulu ambayo itatoa kibali kwa safari maalumu, ikiwa ni
pamoja na kuweka masharti ambayo mtumishi anayetakiwa kusafiri
atatakiwa kuyatimiza kabla ya kupewa kibali.
Lakini
utekelezaji wa agizo hilo unakabiliwa na vikwazo vingi, hasa vikubwa
vitano ambavyo ni uchache wa balozi za Tanzania nje ya nchi, ukomo wa
madaraka ya mabalozi, wigo wa ufahamu wa mambo ya kitaalamu na ukosekana
kwa mazungumzo endelevu iwapo suala moja litawakilishwa na watu wawili
tofauti kwenye mikutano miwili tofauti.
Idadi ndogo ya balozi
Takwimu
za Umoja wa Mataifa (UN), zinaonyesha kuwa hadi sasa chombo hicho kina
wanachama 193 ambao nchi zinazaweza kuwa na uhusiano nazo wa
kidiplomasia, kwa mujibu wa makubaliano ya wanachama wa umoja huo. Kwa
mujibu wa wakosoaji, uchache huo utasababisha mabalozi hao kusafiri
sehemu mbalimbali duniani kushiriki kwenye shughuli ambazo viongozi wa
umma walitakiwa kwenda, hali ambayo itasababisha safari kuwapo kama
kawaida isipokuwa wanaosafiri ndiyo watakaobadilika.
“Ni
kweli kwamba idadi ya watu wanaosafiri itapungua, lakini ile dhana ya
safari itabakia vilevile,” alisema mmoja wa wakosoaji ambaye hakutaka
jina lake litajwe.
“Kwa mfano, mkutano wa Jumuiya ya
Madola unaofanyika Malta, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza ndiye
atatakiwa kwenda. Kwa hiyo ni safari pia.”
Bara zima la
Amerika Kusini lina ofisi moja tu ya ubalozi iliyoko Brasilia, Brazil,
wakati bara la Amerika Kaskazini lina balozi tatu, mbili zikiwa
Marekani--Umoja wa Mataifa jijini New York na Washington--, huku Ulaya
yenye nchi 50 ikiwa na balozi nane, wakati Asia, Arabuni pamoja na
Australia kuna ofisi nane za ubalozi.
Bara la Afrika lenye nchi 52, ndiko kuna balozi nyingi zaidi, kukiwa na ofisi 14.
Ugumu
katika utekelezaji unaosababishwa na idadi ndogo ya mabalozi pia
ulidokezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula mapema mwezi huu.
Akizungumzia
suala hilo, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue ambaye alikuwa akijibu
maswali kuhusu vikwazo vitano vya utekelezaji wa agizo hilo la Rais,
alisema suala hilo linaweza kujibiwa vizuri zaidi na Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Lakini msemaji wa wizara hiyo, Mindi Kasiga alisema atumiwe ujumbe wa barua pepe ili ajibu suala hilo.
Ukomo wa madaraka ya mabalozi
Suala
jingine linalozungumziwa ni ukomo wa mabalozi katika mamlaka yao, hasa
pale wanapotakiwa kumuwakilishi Rais wakati hawabebi madaraka hayo ya
mkuu wa nchi. Mara nyingi wakuu wa nchi huona umuhimu zaidi wa kuwa na
mazungumzo baina yao kuliko na mabalozi inapotokea wamekutana kwenye
mikutano ya mikubwa kama ya Jumuiya ya Madola, Umoja wa Mataifa, Sadc na
mingine inayoweka maazimio muhimu kuhusu masuala kama ya mazingira,
afya, na ya kibiashara.
Lakini Balozi Sefue alisema
Rais atakuwa akihudhuria mikutano michache na hivyo uamuzi huo
hautaathiri nchi. “Ni mikutano michache sana ambayo wanahudhuria wakuu
wa nchi,” alisema Balozi Sefue. “Pale ambapo tutajiridhisha kuwa ubalozi
hauwezi kutuwakilisha vizuri, basi tutaruhusu mtu atoke hapa nyumbani.
Hiyo itakuwa ni baada ya kujua ni nani atakayekwenda na atakwenda
kufanya nini,” alisema Balozi Sefue.
Kwa uzoefu wake,
alisema hata viongozi watakaopewa ruhusa hawatakuwa na misafara mirefu
kama ilivyokuwa awali kwa kuwa wapo baadhi yao ambao wanakuwa hawafanyi
chochote huko waendako.
“Nilipokuwa Washington niliwahi
kushuhudia. Kuna msafara ulikuja, mkubwa sana na kwa kipindi chote
walichokaa pale, wapo baadhi hawakupata nafasi ya kufanya chochote. Hili
nalo ni miongoni mwa mambo yatakayozingatiwa katika vibali
vitakavyokuwa vinatolewa kwa wale watakaokidhi masharti,” alisisitiza.
Kuhusu
ukubwa wa ujumbe ambao kiongozi anaruhusiwa kuambatana nao aendapo nje
ya nchi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mindi Kasiga amewahi
kufafanua kuwa, kwa mujibu wa itifaki, kila mmoja ana maelekezo yake.
“Msafara
wa Rais hauwezi kulingana na wa makamu wake, Waziri Mkuu au waziri wa
kawaida ambao pia hutofautiana na makatibu wakuu au wakuu wengine wa
idara na vitengo vya Serikali,” alisema Kasiga wakati akitoa ufafanuzi
juu ya gharama za safari za nje wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Uwakilishi wa mamlaka ya Rais
Mbali
na vikwazo hivyo, suala jingine ni mabalozi kubeba majukumu ya Rais
kwenye mikutano ya nje jambo ambalo wakosoaji wanasema litawawia vigumu
hasa watakapotakiwa kufanya uamuzi kwa madaraka ya mkuu wa nchi.
Lakini
Balozi Sefue alisema mabalozi watakaotumwa kwenye mikutano hiyo
watabeba kofia hiyo ya mkuu wa nchi na taarifa itakayotumwa nchini
itakuwa na uzito unaostahili hivyo suala hilo halitaathiri ushiriki wa
nchi.
Mabalozi kutokuwa na utaalamu
Uwezo
wa mabalozi kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya kitaalamu pia ni
moja ya mambo yanayoonekana kuwa kikwazo kwa agizo la Rais Magufuli
kuzuia safari za nje.
Lakini Balozi Sefue alisema
matukio yanayohusu masuala ya kitaalamu kama kilimo, mazingira, afya,
madini na mawasiliano ambayo yanahitaji watendaji waliobobea kwenye fani
hizo, yatawekewa utaratibu licha ya kuwa changamoto kwa mabalozi.
“Kila
ubalozi una wataalamu wa masuala mbalimbali ambao wanaweza kutoa
mchango unaostahili kwa lolote linaloweza kuhitajika,” alisema.
“Si
rahisi kukosa mtu mwenye uwezo wa kumsaidia balozi kutekeleza majukumu
yake kiasi cha kuhitaji mtu mwingine kutoka nyumbani. Lakini
likijitokeza hilo, tutatuma mwakilishi.”
Akizungumzia
suala hilo, Balozi Mulamula alisema mapema mwezi huu kuwa utekelezaji
huo utachukua muda kidogo kutokana na balozi nyingi kukosa fedha na
watalaamu.
Suala la fedha kwenye balozi za Tanzania
limekuwa kilio kikubwa kila wakati wa Bunge la Bajeti na mwaka huu suala
hilo liliibuka kwenye hotuba ya kambi ya upinzani iliyosema kiasi cha
Sh30 bilioni ziloizotengwa kwa wizara hiyo hazikutosha kuwawezesha
mabalozi kufanya kazi yao kwa ufanisi.
Suala la weledi
pia lilizungumzwa kwenye hotuba ya kambi ya upinzani ya mwaka 2014/15
ikisema uteuzi holela wa mabalozi usiozingatia sifa, unalikosesha Taifa
fursa nyingi za kiuchumi kwa kuwa wengi hawana ufahamu wa fursa zilizoko
kwenye nchi wanazokwenda.
Lakini mapema mwezi huu,
Balozi Mulamula alisema suala hilo sasa litaangaliwa kwa jicho la karibu
zaidi, hasa uteuzi wa mabalozi.
Alisema watatoa
mwongozo ambao utawataka wawakilishi hao wasibweteke katika utendaji wao
kwa kuwa kuna mpango wa kuanzisha utaratibu wa kupima matokeo ya
utendaji wao kwa kila baada ya kipindi kitakachoelekezwa.
“Kwa sasa tutakuwa tunawapima mabalozi wetu kwa malengo tuliyokubaliana nao ambayo yanaweza kuwa ya mwaka au zaidi.
Tutakuwa tunamuuliza balozi umeweza kuleta watalii au kuwahamasisha wawekezaji wangapi nchini?” alisema.
“Hii ni kwa sababu zamani tulikuwa tunakwenda kienyeji lakini kwa sasa hapa kazi tu.”
Mazungumzo endelevu
Kikwazo
kingine kinachoonekana kwenye utekelezaji wa agizo hilo ni kukosekana
kwa mazungumzo endelevu iwapo suala moja litawakilishwa na watu wawili
tofauti kwenye mikutano miwili tofauti.
“Mfano iwapo
kutakuwa na mkutano wa suala fulani la Jumuiya ya Afrika Mashariki
nchini Kenya, kwa agizo hilo la Rais, atakayewakilisha ni balozi wa
Tanzania nchini Kenya,” alisema mkosoaji huyo na kuongeza:
“Iwapo
suala hilo litaendelezwa kwenye mkutano mwingine wa jumuiya nchini
Uganda, ni dhahiri atawakilisha balozi wa Tanzania nchini humo ambaye
hakuwapo kwenye mkutano wa Kenya. Kwa hiyo kutakuwa na upungufu.”
Balozi
Sefue hakutaka kufafanua kuhusu hoja hiyo na badala yake akaielekeza
kwa Wizara ya Mambo ya Nje, ambayo alisema ina nafasi nzuri zaidi ya
kulizungumzia.
No comments:
Post a Comment