Serikali
imezungumzia tishio la Serikali ya Marekani la kusitisha misaada kwa
Serikali ya Tanzania kutokana na mgogoro wa kisiasa Zanzibar na
kukamatwa kwa maofisa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.
Ofisi
ya Ikulu jana ilisema masharti yaliyotolewa na Serikali ya Marekani
yanatekelezeka na yatamalizwa kabla ya kikao cha Bodi ya Shirika la
Maendeleo ya Milenia (MCC) kukaa Desemba, mwaka huu.
Wiki
iliyopita, Serikali ya Marekani iliitaka Serikali ya Tanzania kumaliza
haraka mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar, vinginevyo upo uwezekano wa
kusitishwa msaada wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 472 (Sh. bilioni
999.4), za awamu ya pili ya fedha za MCC la nchi hiyo.
Fedha
hizo za MCC awamu ya pili ni kwa ajili ya kuiwezesha Tanzania kusambaza
umeme na kuwaunganisha wananchi wengi katika Gridi ya Taifa na
uimarishaji wa taasisi zinazohusika na na sekta ya nishati.
Mambo
ambayo Serikali ya Marekani iliitaka Tanzania kumaliza haraka ni suala
mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar pamoja na kupata ufafanuzi wa watuhumiwa
waliokamatwa kwa makosa ya mtandaoni, wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 25,
mwaka huu.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue jana alisema suala hilo haliisumbui serikali na ni tatizo dogo ambalo linatatuliwa.
Alisema
serikali ina uhakika wa kumaliza masuala hayo kabla ya kikao hicho cha
Bodi ya MCC kukaa ambao masuala hayo yatakuwa yameshatatuliwa na
kupatiwa ufumbuzi.
Alisema Bodi ya MCC ilikaa kikao chake cha kwanza Septemba, mwaka huu na inatarajia kukaa tena kikao chake Desemba, mwaka huu.
Alisema serikali ina uhakika Bodi ya MCC ikikaa kikao cha Desemba, mwaka huu itapitisha pasipo na shaka yoyote.
Aliongeza
kuwa suala la sheria ya makosa mtandaoni, kuna watu walikamatwa na
watafikishwa mahakamani ambapo mahakama yenyewe ndiyo itakayotoa hukumu
na kama wana makosa watahukumiwa na kama hawatakutwa na makosa basi
wataachiwa huru.
Balozi Sefue alisema suala hilo ni la kisheria, watu wametuhumiwa na wamepelekwa mahakamani ambako itaamua.
Kuhusu
mgogoro wa Zanzibar, Balozi Sefue alisema kuna vikao vinavyoendelea vya
kupata muafaka na mgogoro huo nao utamalizwa kwa haraka zaidi.
Marekeni
ilieleza kuwa mambo hayo iliyotaka ipatiwe ufumbuzi, yataiwezesha MCC
kuipima Tanzania katika sifa za kupata fedha hizo.
No comments:
Post a Comment