Dar es Salaam.
Rais John Pombe Magufuli amekuwa wa kwanza tangu mfumo wa vyama vingi kuanza nchini kutumia muda mrefu kutangaza Baraza la Mawazi kutokana na kile wasomi, wachambuzi wa siasa kusema pengine anapata wakati mgumu kupata mawaziri watakaoendana na kasi yake.
Rais John Pombe Magufuli amekuwa wa kwanza tangu mfumo wa vyama vingi kuanza nchini kutumia muda mrefu kutangaza Baraza la Mawazi kutokana na kile wasomi, wachambuzi wa siasa kusema pengine anapata wakati mgumu kupata mawaziri watakaoendana na kasi yake.
Katiba ya mwaka 1977 inamtaka Rais
kumteua waziri mkuu ndani ya siku 14 tangu alipoapishwa na kulipeleka
jina lake bungeni, lakini katiba hiyo ipo kimya kuhusu uteuzi wa
mawaziri, hivyo Rais anaweza kutumia muda wowote.
Wakati
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa alipoingia madarakani mwaka 1995 aliteua
baraza la mawaziri Novemba 28, siku tano baada ya kuapishwa, Jakaya
Kikwete alitangaza Baraza la kwanza Siku 14 baada ya kuapishwa na Dk
Magufuli hadi sasa, siku 25 zimepita tangu aapishwe Novemba 5, mwaka huu
hajafanya hivyo.
Kazi ambazo Rais Magufuli ameanza
kuzifanya bila mawaziri ni kuzuia safari za nje, kuzuia sherehe za Uhuru
na kuanza kupambana na wabadhirifu wa fedha za umma.
Wasomi
hao wakilinganisha alichokisema kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa
Bunge, walisema kuwa ana njozi za Tanzania aitakayo huku akieleza wazi
kuwa anatambua kuna mawaziri, wabunge wanakula rushwa na akibainisha
wazi hana imani kama waliomo ndani ya CCM wanakula pia.
Mhadhiri
kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Elijah Kondi, alisema kuwa sababu za Magufuli kuchelewa kutaja Baraza la
Mawaziri ikilinganishwa na Serikali zilizopita inatokana na utendaji wa
Mawaziri wa Serikali iliyopita, wengi hawakufanya vizuri na baadhi yao
hata ushindi wao wa ubunge una maswali mengi.
Alisema
tayari ana njozi za anachotaka kukifanya, anapata wakati mgumu wa ni
nani mtu sahihi wa kumsaidia kutimiza njozi zake, hata ndani ya CCM
baadhi yao hawaaminiki na amekuwa akisema hivyo mara nyingi.
Alipozungumzia rushwa pia hakusita kuwahusisha walio ndani ya CCM, japo
siyo moja kwa moja.
“Inawezekana waliopo wengi anaona
hawawezi kuendana na kasi yake, pengine hata wale anaoona wana afadhali
walishawahi kupata kashfa mbalimbali, huku yeye akiwa na njozi za kuanza
upya na watu wenye utashi wa mabadiliko ya kweli na ya wote, ”alisema
Kondi.
Profesa George Shumbusho, mhadhiri wa Chuo Kikuu
cha Mzumbe alisema Rais anapata wakati mgumu kuteua mawaziri kutokana
na changamoto alizozitaja siku ya kuzindua Bunge kuwa nyingi na nzito,
zinazohitaji watu makini kuzitekeleza.
Alisema analazimika kufanya upembuzi yakinifu kujua ni
nani na atashughulikia eneo gani kama anavyotaka yeye, liendane na kasi
na utendaji wake.
“Ninachokiona anataka kuunda baraza
makini hataki kurudi na kuhoji utekelezaji wa kazi, kingine anahitaji
aunde litakalokaa muda mrefu na kufanya utekelezaji badala ya kuunda
lingine kwa muda mfupi, ”alisema Profesa Shumbusho.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mhadhiri mwandamizi ambaye ni Mkuu wa
Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT),
Emmanuel Mallya, alisema anachukua muda kutaja Baraza la Mawaziri
kutokana na kutaka litakalotambua anataka nini kifanyike katika Serikali
yake ambayo amekuwa akiitaja moja kwa moja kuwa ya Magufuli.
Alifafanua
kuwa hataki kukurupuka na kujilaumu baadaye kutokana na utendaji
usioridhisha unaoweza kujitokeza asipokuwa makini, ndiyo maana anachukua
muda na kujaribu kuonyesha ni jinsi gani inawezekana kusimamia vitu na
vikaenda.
“Kwa kuangalia kasi yake, unaona kabisa
anapata wakati mgumu kupata viongozi watakaofanya kazi kwa lengo moja ya
mageuzi na mabadiliko, ndiyo maana anachukua muda ili akija nalo liwe
makini, ” alisema Mallya.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi
ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda, alisema kwenye
mitandao ya kijamii kuna utani unazunguka kuwa kwa kasi yake anaweza
kufanya kazi hata bila kuwa na mawaziri.
“Ni utani,
lakini ukiuchunguza mara mbili unaona kabisa hata wananchi wameona
anachokifanya na wanahitaji kukiona hicho kutoka kwenye Baraza lake,”
alisema.
Alisema kasi yake na kubana matumizi alikoanza
nako anahitaji kuwa makini kwa sababu alitamka anataka kuwa na baraza
dogo la mawaziri.
Alifafanua kuwa kwenye Serikali ya
Awamu ya Nne mwaka 2005, mawaziri na naibu wao idadi yao ilikaribia 60,
wakitumia mashangingi yanayokula mafuta, posho, hivyo ili kudhibiti hilo
atachukua muda pia, ikiwamo kuvunja baadhi ya wizara kama ataona itafaa
na kumsaidia anachotaka kukifanya.
No comments:
Post a Comment