KAMPUNI
ya Said Salim Bakhresa (SSB) inachunguzwa na vyombo vya dola kwa tuhuma
za kushiriki kukwepa kodi na hivyo kuikosesha serikali mabilioni ya
fedha kutokana na makontena yaliyohifadhiwa kwenye bandari yake ya nchi
kavu (ICD) ‘kupotea’ bila kulipiwa kodi.
Tayari
Mamlaka ya Mapato (TRA) imepiga marufuku SSB kuingiza makontena katika
bandari hiyo kavu ambako ndiko kunadaiwa kufanyika kwa vitendo hivyo vya
ukwepaji wa kodi kutokana na baadhi ya makontena kupotea katika
mazingira ya kutatanisha.
Katika
barua iliyoandikwa kwenda kwa Meneja Mkuu wa SSB iliyosainiwa na
Wolfgang Salia kwa niaba ya Kamishna wa Ushuru na Forodha wa TRA,
inaeleza kuwa usitishwaji huo unatokana na kampuni hiyo ya Bakhresa
kuchunguzwa kwa tuhuma za kuwepo madai ya kujihusisha na ukwepaji wa
kodi kwa baadhi ya kontena zilizoingia na kutoka kwenye ICD yake.
Kwa
mujibu wa barua hiyo, vitendo hivyo vya ukwepaji wa kodi vimefanywa
kinyume cha Sheria ya Ushuru wa Pamoja wa Nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki ya Mwaka 2004 na hivyo kuikosesha Serikali mapato.
“Unafahamu
kwamba uondoaji wa bidhaa kutoka eneo linalodhibitiwa na forodha,
ambalo kodi na ushuru wa serikali haujalipwa ni kinyume na sheria kwa
mujibu wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Usimamizi wa Forodha
ya mwaka 2004 na kanuni zake kwa vile husababisha upotevu wa mapato ya
Serikali.
“Kwa
sababu hiyo, imeamuriwa kukuzuia kupeleka makontena katika bandari yako
kavu kuanzia tarehe ya barua hii, hadi suala hili litakapotatuliwa.
Pande zote zinazohusika zinapaswa kutii amri hii.
“Kutokana
na sababu hizo, tunasimamisha upelekaji wa makontena katika bandari
yako kavu. Usitishaji unaanza mara moja. Hata hivyo utoaji wa bidhaa
zilizopo katika bandari hiyo tajwa utaendelea,” ilisema sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa Novemba 17, mwaka huu.
Mkurugenzi
wa Huduma na Elimu kwa Walipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
Richard Kayombo alipoulizwa juu ya suala hilo jana, alikiri kampuni
hiyo kuchunguzwa, lakini akagoma kuzungumzia kwa undani kwa kuwa suala
hilo liko kwenye uchunguzi.
“Mimi
siwezi kulizungumzia suala hilo kwa sababu liko kwenye uchunguzi na
wanaofanya uchunguzi huo ni state organ (vyombo vya dola). Katika hatua
hiyo, mimi siruhusiwi kusema lolote,” alisema Kayombo.
Meneja
wa Kundi la Makampuni ya Said Salim Bakhresa, Said Mohamed alipotafutwa
kuzungumzia suala hilo, alisema yeye hahusiki na masuala ya ICD badala
yake mambo hayo aulizwe Meneja wa ICD aliyemtaja kwa jina moja la Khan. “Mimi niulizie unga umekosekana... Sihusiki kabisa na mambo hayo,” alisema Mohamed.
Hata hiyo, Mohamed aligoma kutoa mawasiliano ya Khan, akisema: “Hiyo namba mimi hapa sina, wewe mtafute tu huko ICD atakupa maelekezo zaidi.”
Habari
zilizopatikana jana pia zilieleza kuwa mmoja wa wafanyakazi wa SSB
anayeishi maeneo ya Kinyerezi (jina tunalihifadhi), alivamiwa na kundi
la maofisa wa Serikali kuanzia asubuhi hadi jioni na kufanya upekuzi
kwake.
“Tangu
asubuhi hawa jamaa wamekuja hapa wakamchukua mjumbe wa eneo hili na
kwenda naye kufanya upekuzi, hadi sasa hivi wanaendelea kufanya kazi
hiyo,” alisema Tito Bagule, mkazi wa eneo hilo.
Tayari
Rais John Magufuli ameshamsimamisha Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade
kutokana na tuhuma za uzembe na rushwa na kusababisha upotevu wa
makontena zaidi ya 349 yenye thamani ya Sh bilioni 80.
Upotevu
huo umegundulika baada ya makontena hayo kuonekana kwenye mifumo ya
Mamlaka ya Bandari, lakini haimo kwenye mifumo ya TRA.
Kabla
ya kusimamishwa kazi, Bade alikiri kupotea kwa makontena hayo, wizi
ambao alisema unafanywa kati ya bandari kuu na bandari kavu (ICD) ya
Ubungo.
Alisema
kutokana na upotevu wa kontena hizo mmiliki wa bandari hiyo ameamriwa
kulipa faini ya Sh bilioni 12.6 na hadi sasa alishalipa Sh bilioni 2.4.
Katika
hatua nyingine, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI),
Diwani Athuman, amesema tayari jeshi hilo limeanza upelelezi kuhusu
kashfa ya upotevu wa makontena iliyobainishwa hivi karibuni na
kusababisha baadhi ya vigogo wa TRA kusimamishwa kazi.
Pamoja
na upelelezi huo, alisema wameanza uchunguzi wa mali za wafanyakazi
wote waliohusishwa na kashfa mbalimbali TRA kama ilivyoagizwa na Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa ili kubaini kama zinaendana na kipato chao halisi.
Akizungumza
na mwandishi wetu jana, Diwani alikiri kuwa jeshi hilo linawashikilia
watumishi wanne kati ya watano wa TRA ambao jeshi hilo liliagizwa
liwakamate na kuwahoji kuhusu sakata la upotevu wa kontena 349.
“Tuliagizwa
tuwakamate watumishi watano, mpaka sasa tumewakamata wanne, mmoja ndio
tupo kwenye utaratibu wa kumkamata, lakini kikubwa ni kwamba tumeanza
upelelezi, kama tulivyoagizwa,” alisisitiza DCI Diwani.
Kuhusu
suala la mali za watumishi hao, alisema ni jambo ambalo bado lipo
kwenye upelelezi na linahusisha taratibu nyingi za kisheria, hivyo
asingependa kulizungumzia kutokana na sababu za kipelelezi.
Kutokana
na ziara ya ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam, Waziri Mkuu
Majaliwa alibainisha kupitishwa kwa makontena zaidi ya 300 bandarini
bila kulipiwa kodi na kuisababishia hasara Serikali ya zaidi ya Sh
bilioni 80.
Kutokana
na kashfa hiyo, Rais Magufuli alimsimamisha kazi Bade na kumteua Katibu
Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Philip Mpango kukaimu nafasi hiyo mpaka
hapo uchunguzi utakapokamilika.
Maofisa
wengine waliosimamishwa ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki, Mkuu wa
Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya, Mkuu wa Kitengo cha
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni Mpande, Hamisi Ali
Omari na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu, Eliachi Mrema. Wengine ni
Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.
No comments:
Post a Comment