Mchakato wa kunyang’anya mashamba na viwanda kutoka kwa wamiliki walioshindwa kutekeleza masharti waliyopewa na Serikali umeanza.
Taarifa tulizozipata
zimeeleza kuwa miongoni mwa mashamba na viwanda hivyo ni kutoka mkoani
Morogoro, Lindi, Arusha, Mbeya, Tanga, Kilimanjaro na Dar es Salaam.
Wiki
iliyopita, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilitoa tangazo kwa wawekezaji
walionunua viwanda na mashamba ya Serikali ikiwakumbusha kurejea kwenye
mikataba yao.
Taarifa
hiyo iliyosainiwa na Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru (pichani)
ilieleza kuwa inarejea mikataba yote ya mauzo ya viwanda na mashamba
iliyoingiwa kupitia Mpango wa Ubinafsishaji na kwamba kuna wawekezaji
wamekiuka masharti ya mikataba yao.
Miongoni
mwa masharti hayo yaliyokiukwa ni kutoendelezwa viwanda na mashamba kwa
mujibu wa mikataba, kushindwa kutekeleza mpango wa uwekezaji, baadhi ya
wanunuzi kuuza mashine walizozikuta bila kurudisha mashine mbadala,
kutokamilisha malipo ya ununuzi wa viwanda na mashamba na kubadilisha
matumizi ya viwanda na mashamba bila idhini.
“Ninawaagiza
wawekezaji wote walionunua viwanda na mashamba yaliyokuwa yanamilikiwa
na Serikali kwa ajili ya uwekezaji wawasilishe taarifa zao za sasa ndani
ya siku 30, kinyume na hapo Serikali itachukua hatua stahiki ikiwamo
kurejesha viwanda na mashamba hayo kwenye miliki yake,”ilisema taarifa hiyo.
Lakini
zikiwa zimebaki siku 24 kwa tangazo hilo kufika kikomo taarifa
zinaeleza kuwa tayari mashamba yameanza kurejeshwa kwenye umiliki wa
Serikali, kwa madai ni utekelezaji wa agizo la Serikali.
Katibu
Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Kidata
akizungumzia taarifa hizo za kuanza kurejeshwa kwa baadhi ya mashamba
alisema hawezi kutoa maelezo kuhusu madai hayo kwa kuwa hana taarifa
nayo.
Lakini alisema anatambua kwamba mambo yanaendeshwa kwa sheria na taratibu zake tofauti na madai ya taarifa hizo.
“Sidhani kama mtu anaweza kuamka tu na kusema hili lifanyike. Lazima taratibu zifuatwe,” alisema Kidata.
Hata
hivyo, Kidata alifafanua kuwa wizara hiyo imekuwa ikiendesha ikirejesha
ardhi serikalini kutoka kwa wamiliki walioshindwa kuendeleza masharti.
Alisema
mtu anapopewa dhamana ya kumiliki ardhi, dhamana hiyo huambatana na
masharti ikiwamo kuendeleza na anaposhindwa hunyang’anywa.
“Lakini kabla ya kufanya hivyo hupewa notisi na asipoifanyia kazi uamuzi wa mwisho ni kuichukua,”alisema Kidata.
Alisema Serikali chini ya wizara hiyo itaendelea kufanya hivyo kama wamiliki watakiuka masharti wanayotakiwa kufuata.
Kwa
upande wake, Mafuru alisema serikali imetoa tangazo hilo na kuwapa
wahusika siku 30 ili ndani ya muda huo, wajipange na kuandaa taarifa za
utekelezaji wa miradi waliyopewa kuiendesha.
No comments:
Post a Comment