MAHAKAMA YA TANZANIA YAFUNGUA MILANGO KWA WANAHABARI - LEKULE

Breaking

27 Nov 2015

MAHAKAMA YA TANZANIA YAFUNGUA MILANGO KWA WANAHABARI

Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Shaban Ally Lila akifunga Mafunzo ya siku mbili ya Waandishi wa Habari za Mahakama yaliyofanyika jijini Dar es salaam.
Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Shaban Ally Lila akitoa ufafanuzi kuhusu Kichwa cha Habari ya Mahakamani kilichoandikwa bila kuzingatia Weledi na moja ya Gazeti la Kila siku wakati wa mafunzo ya siku mbili ya Waandishi wa Habari za Mahakama yaliyofanyika jijini Dar es salaam. Picha/Aron Msigwa –MAELEZO.


Mahakama ya Tanzania imesema kuwa itendelea kufanya kazi na vyombo vya Habari nchini katika kuuhabarisha umma kuhusu utekelezaji wa jukumu la Kikatiba ililonalo la kutafsiri sheria mbalimbali na kuzitolea maamuzi ili kuwawezesha wananchi kujua na kupata Haki zao kwa wakati.
Akifunga Mafunzo ya siku 2 ya waandishi wa Habari za Mahakama jana jijini Dar es salaam Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Shaban Ally Lila aliwataka waandishi hao kutimiza wajibu wao wa kuueleza umma taarifa sahihi za mashauri mbalimbali yanayotokea mahakamani kwa kuzingatia sheria.
Alisema vyombo vya habari na mahakama vinahitajiana, vinafanya kazi pamoja kwa manufaa ya umma huku akieleza kuwa mikutano ya mara kwa mara kati ya wanahabari na mahakama kunaongeza kuaminiana na kujenga mahusiano mazuri.
Alifafanua kuwa kazi ya Mahakama kikatiba ni kutafsiri sheria mbalimbali na kuzitolea maamuzi kwa mujibu wa sheria kulingana na mashauri yananayowasilishwa Mahakamani na kuongeza kuwa hakuna Jaji wa Mahakama ya Tanzania anayeamua kesi bila nje ya utaratibu wa sheria zilizopo.
Alisema wao kama majaji hutumia sheria zilizopo katika kutoa maamuzi hata kama haziwapendezi wahusika na kuongeza kuwa jambo wanalolifanya ni kutoa maoni na mapendekezo kwa mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi.
" Sisi kama Majaji hutumia sheria zilizopo kutoa maamuzi,hatutungi sheria jukumu letu kikatiba ni kutafsiri sheria mbalimbali na kuzitolea maamuzi pia tunatumia fursa ya maamuzi tunayoyatoa  kuelimisha jamii kuhusu sheria iliyotumika kutoa haki katika kesi husika" Alisema.
Aliwataka waandishi wa Habari za Mahakama kujipa muda wa kutosha pindi wanapofika Mahakamani kufuatilia mashauri yanayoendeshwa ili waweze kuwa na taarifa za kutosha pindi shauri linapofunguliwa na kutolewa hukumu ili kuwawezesha wananchi kupata taarifa za kutosha za mwenendo wa Mashauri.
Aliongeza kuwa Mahakama ya Tanzania imedhamiria  kufanya kazi na waandishi wa habari nchini kwa kuzingatia kwamba wakati majaji wanapotoa hukumu mahakamani kunakuwa na idadi ndogo ya wananchi wanaoshuhudia kuliko ile iliyo nje ila vyombo vya habari kutokana na umuhimu wake huwapasha habari mamilioni ya watanzania  walio nje ya Mahakama.
Alisema Mahakama itaendelea kujenga mahusiano mazuri na Vyombo vya Habari hususan waandishi wa Habari za Mahakama kwa kutenga maeneo ndani ya Mahakama yatakayotumiwa na waandishi hao kuwawezesha kufanya kazi zao bila vikwazo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Pia alieleza kuwa Mahakama, itaendelea kutoa taarifa za ufafanuzi wa hukumu mbalimbali zitakazotolewa kwa vyombo vya habari pia Nakala za taarifa za Hukumu kwa waandishi wa habari ili kuwawezesha wananchi kujua ukweli wa yale yanayojili mahakamani kuondoa upotoshaji unaotokea.
Aidha alisema kuwa Mahakama itaendelea kushirikiana  na Baraza la Habari Tanzania (MCT) katika kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari za Mahakama ili waweze kuandika habari zenye ukweli na uhakika.
Mhe. Shaban Lila alisema kuwa Mahakama iko tayari kupokea maoni yanayohusu utendaji kazi wake ili iweze kuyafanyia kazi kwa manufaa ya vyombo vya habari na wananchi. 
Awali akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo kabla ya kumkaribisha Jaji Kiongozi kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Mahakama ya Tanzania Bi. Wanyenda Kuta aliwaambia washiriki wa mafunzo hayo kuwa Mahakama inaendelea kutekeleza nguzo 3 ambazo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na Upatikanaji wa Haki kwa Wakati, Kuongeza Imani wanachi kwa Mahakama pia kuboresha miundombinu ya Mahakama nchini.
Alisema kuwa wandishi wa Habari za mahakama waliohudhuria mafunzo hayo yaliyoandalia na Mahakama ya Tanzania na Baraza la Habari Tanzania (MCT) wamejifunza masuala mbalimbali ambayo yamewajengea ufahamu waandishi wa Habari za Mahakama kuhusu lugha za kimahakama, uandishi bora wa habari za Mahakama, Uhuru wa Mahakama pamoja na kujua Haki za Washitakiwa na Watuhumiwa wanapofikishwa mahakamani.
Kwa upande wake Meneja wa Maadili wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Allan Lawa  akizungumza na wanahabari hao aliwataka waandike habari za Mahakama kwa usahihi na umakini mkubwa kufuatia Mafunzo
waliyoyapata.

Bw. Lawa aliishukuru Mahakama mafunzo hayo na hatua ya uongozi wa mahakama  kuyakubali mapendekezo yaliyotolewa na Waandishi wa Habari za Mahakama ikiwemo kutenga eneo ndani ya mahakama litakalotumiwa na waandishi wa Habari za Mahakama, utoaji wa Nakala za kesi na ufafanuzi wake mara hukumu zinapotolewa, Mahakama kukubali kushawishi uanzishaji wa madawati ya Habari za Mahakama kwenye vyombo vya Habari pamoja na mahakama kukubali kuendesha mafunzo ya mara kwa mara kwa waandishi wa Habari za Mahakama na wahariri wao.

No comments: