Hatimaye aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amejitokeza kwa mara ya kwanza kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam na kumtaka Rais Jakaya Kikwete amalize haraka mgogoro wa uchaguzi uliopo Zanzibar kabla ya kumpisha mrithi wake, Dk. John Magufuli.
Akizungumza
na waandishi wa habari kwenye ofisi kuu za CUF jana, Lipumba alisema
jaribio lolote la kutaka Rais Kikwete aondoke na kumuachia Magufuli
suala hilo ni sawa na kumtwisha rais ajaye (Magufuli) mzigo mkubwa ambao
hatauweza na mwishowe ni kusababisha madhara makubwa visiwani humo
ikiwamo vurugu na uvunjifu wa amani.
Profesa
Lipumba aliyasema hayo ikiwa imepita takriban miezi mitatu tu tangu
atangaze kujiuzulu uenyekiti wa CUF Agosti 6, 2015 ili awe mwanachama wa
kawaida wa chama hicho.
Lipumba
alitangaza kuchukua uamuzi huo wa utata kutokana na kile alichodai kuwa
ni kupinga uamuzi wa chama chake na vingine vinavyounda umoja wa katiba
ya wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kuwapokea waliokuwa makada wa CCM na kuwapa nafasi
ya kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba
25, 2015.
Akielezea
zaidi kuhusiana na hali ya Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu, Lipumba
alisema njia pekee ya Rais Kikwete kumaliza mgogoro huo ni kuitaka ZEC
iendelee na mchakato wa majumuisho ya kura na kumtangaza mshindi ambaye
ni wazi anajulikana kuwa ni Maalim Seif, hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa karatasi za matokeo ya kura zilizokusanywa kutoka kwenye vituo vyote visiwani humo.
Alisisitiza
kuwa endapo Rais Kikwete atamkabidhi madaraka Magufuli kabla ya
kumaliza mgogoro uliopo Zanzibar, ni dhahiri atakuwa amemuweka kwenye
wakati mgumu na upo uwezekano kuwa mrithi wake huyo atatumia nguvu kubwa
kutatua mgogoro huo, jambo ambalo ni la hatari zaidi kwa hatma ya
Zanzibar na taifa.
Aliongeza kuwa Dk. Magufuli hataweza kuiongoza nchi kwa amani ikiwa Zanzibar kutakuwa na machafuko, hivyo Rais Kikwete anapaswa kulimaliza jambo hilo kabla hajamaliza muda wake wa uongozi.
Aliongeza kuwa Dk. Magufuli hataweza kuiongoza nchi kwa amani ikiwa Zanzibar kutakuwa na machafuko, hivyo Rais Kikwete anapaswa kulimaliza jambo hilo kabla hajamaliza muda wake wa uongozi.
“Kama
watu wanavyomuita Magufuli kuwa ni tingatinga au bulldozer, basi ni
dhahiri atatumia nguvu katika kutatua mgogoro huo… na jambo hilo
litakuwa ni la hatari kubwa kwa Zanzibar na taifa,” alisema Lipumba.
Lipumba
aliongeza kuwa wananchi wa Zanzibar hawawezi kurudia kufanya uchaguzi
kwa mara ya pili kwa kuwa walishapiga kura na zikahesabiwa, na mgombea
wao waliyemtaka alishaibuka mshindi.
Aidha,
Lipumba alimtaka rais wa sasa, Dk. Ali Mohamed Shein, kukumbuka
uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 pale ZEC ilipomtangaza yeye (Dk. Shein) kuwa
mshindi kwa kupata asilimia 50.2 dhidi ya Maalim Seif asilimia 49.8,
lakini Maalim Seif alikubali na Dk. Shein akawa Rais.
Alisema
Dk. Shein akumbuke pia matukio yaliyotokea mara baada ya uchaguzi wa
mwaka 2000 ambao majimbo 16 ya mkoa wa Mjini Magharibi uchaguzi wake
ulifutwa na ukarudiwa kwa nguvu na CUF waliitisha maandamano Januari 27,
2001 na makumi ya watu kuuawa huku watu wengine zaidi ya 2,000 kuwa
wakimbizi Shimoni, Mombasa Kenya; jambo ambalo nchi haipaswi
kulishuhudia tena.
Lipumba
alisema sasa ni wakati muafaka kwa Dk. Shein kuonyesha ukomavu wa
kisiasa kwa kukubali maamuzi ya Wazanzibari bila kuruhusu visiwa hivyo
kuingia katika machafuko.
Lipumba
alisema katika katiba ya Zanzibar , Sura ya 9, inazungumzia ZEC na
kadri alivyoisoma, hakuna kifungu chochote kinachoipa mamlaka ZEC wala
Mwenyekiti wa ZEC uwezo wa kufuta Uchaguzi Mkuu.
Alisema
katiba hiyo na sheria yake haijawapa mamlaka ZEC wala Mwenyekiti
kufuta uchaguzi, bali Sura ya 9, kifungu cha 119, fasiri ya 10, inaeleza
kuwa maamuzi ya ZEC yatafanyika ikiwa kuna akidi imetimia na akidi hiyo
lazima pawapo na Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa ZEC na wajumbe
wengine wanne ndipo kikao cha maamuzi kinaweza kufanyika.
Aliongeza
kuwa kwa mujibu wa katiba hiyo, maamuzi yoyote ya ZEC yatakayotolewa
lazima yatokane na uwingi wa wajumbe wa ZEC waliokuwapo katika kikao
rasmi ambacho akidi yake imetimia asilimia mia moja.
Alisema Mwenyekiti wa ZEC, Jecha, alitoa maamuzi ambayo hayakutokana na kikao rasmi cha tume hiyo.
Alisema
hata kikao hicho kikifanyika, Katiba ya Zanzibar na Sheria za Uchaguzi
za Zanzibar hazijawapa mamlaka ZEC ya kufuta uchaguzi bali ZEC imepewa
mamlaka ya kuahirisha uchaguzi kama kumetokea tatizo.
Katika
hatua nyingine, Lipumba alisema kama Dk. Magufuli ana nia ya dhati ya
kuleta maendeleo na kutokomeza ufisadi nchini kama alivyoahidi wakati wa
kampeni zake, basi aanze kuwashughulikia watuhumiwa wa kashfa ya
akaunti yaTegeta Escrow.
Alisema
Dk. Magufuli anapaswa kuwakamata watuhumiwa wote waliohusika katika
kashfa hiyo na kuwafikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
No comments:
Post a Comment