Baada
ya kusota rumande kwa zaidi ya miaka mitatu hatimaye Mwenyekiti wa
Chama cha Soka Pwani (Corefa), Hassani Othman maarufu kama Hasanoo
ameachiwa huru kwa dhamana katika Mahakama ya Kisutu.
Hasanoo
anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kusafirisha pembe za ndovu
kutoka Dar es Salaam kwenda Hong Kong, zenye thamani ya Sh1.1 bilioni na
wenzake amesota rumande kwa zaidi ya miaka miaka mitatu baada ya upande
wa mashtaka kuizuia dhamana yake.
Hakimu
Mkazi Mkuu, Thomas Simba leo amemuachia huru Hasanoo na wenzake baada
ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili
wanaominika, mmoja kati yao kuwasilisha fedha taslimu Sh 50 milioni ama
hati ya mali yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Washtakiwa
kusalimisha hati zao za kusafiria mahakamani na wasitoke nje ya jiji la
Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama.
Hasanoo
na wenzake wamekamilisha kasoro mmoja wao hakuwa na wadhamini hivyo
amepelekwa rumande hadi atakapoyakamilisha masharti hayo.
Kesi
hiyo ambayo ipo katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa mashahidi
wa upande wa mashtaka itaendelea kusikilizwa Novemba 17,2015.
Upande wa serikali iliwakilishwa na Mawakili, Paul Kadushi na Faraja Nchimbi.
Mbali
na Hasanoo washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Ally
Kimwaga, Dastan Mwanga, Godfrey Mwanga, John Mlai na Khalid Fazaldin.
Kwa
pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Septemba Mosi na Novemba 20, mwaka 2012,
kati ya Dar es Salaam na Hong Kong walikula njama ya kujihusisha na
biashara ya nyara za serikali bila ya kuwa na leseni inayowaruhusu
kufanya hivyo.
Kwa
nia ovu walipanga, wakatekeleza, wakasimamia na kuwezesha kifedha
kufanyika kwa biashara ya nyara za serikali kwa kusafirisha vipande 569
vya Pembe za ndovu, vyenye uzito wa kilogramu 1330 na thamani ya Sh
1,185,030,000 kwenda Hong Kong.
Siku
hiyo ya tukio washtakiwa hao wanadaiwa kujihusisha na biashara ya nyara
za serikali kinyume na kifungu cha 80 na 34 ya uhifadhi wa Wanyama Pori
namba 5 na kwamba kwa nia ovu waliendesha biashara hiyo ya nyara za
serikali bila ya kuwa na kibali halali kinachowaruhusu kufanya biashara
hiyo.
No comments:
Post a Comment