Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeanza jana mjini Dodoma na moto ambao wengi waliutabiri huku harufu ya ushabiki wa vyama ikitawala.
Katika
zoezi la kumtafuta Spika wa Bunge hilo lililotanguliwa na maswali na
majibu kwa wagombea nane waliojitokeza, Mgombea Uspika kupitia Chadema,
Goodluck ole Medeye alikwaruzana kimtazamo na mbunge wa jimbo la Mtama,
Nape Nnauye.
Swali
la Nape lililokuwa kati ya maswali matatu aliyoulizwa Ole Medeye
lilionekana kumuudhi mgombea huyo. Nape alimtaka Ole aeleze kama ameacha
tabia ya ubaguzi kwa madai kuwa Godbless Lema aliwahi kumtuhumu kuwa ni
mbaguzi.
Ingawa
Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Andrew Chenge alikataa swali hilo
lisijibiwe akieleza kuwa halikuwa swali, Ole Medeye alihitimisha kwa
kumueleza Nape alichokuwa nacho moyoni ingawa hakumtaja jina.
“Kuna
mbunge hapa aliniuliza swali ambalo kwa lugha za kibunge tunaliita ni
swali la kuudhi. Mbunge huyo nimemsamehe, sina chuki naye kwa sababu
najua kinachomsumbua ni utoto tu, akikua ataacha,” alisema Ole Mideye.
Uchaguzi huo ulikamilika na kumuwezesha Job Ndugai kuwa spika wa Bunge hilo baada ya kupata asilimia 70 ya kura zote.
No comments:
Post a Comment