Sanjay
Rughani (pichani) anakuwa Mtanzania wa kwanza kuiongoza benki ya
Standard Chartered Tanzania akipokea uongozi wa benki hiyo kutoka kwa
aliyekuwa mkurugenzi wake, Liz Lloyd, ambaye amerudi katika makao makuu
ya benki hiyo, London, kuchukua nafasi ya Mshauri wa Kisheria wa benki
hiyo.
Sanjay
alijiunga na benki ya Standard Chartered Tanzania mwaka wa 1999 akiwa
kama Meneja msaidizi wa kitengo cha Fedha. Baada ya miaka miwili Sanjay
alipata cheo cha Meneja wa kitengo cha Fedha kwa Bara la Afrika, kazi
ambayo aliifanya akiwa katika makao makuu ya benki hiyo, London. Alirudi
nyumbani Tanzania mwaka wa 2002 na kupata cheo cha Mkuu wa Kitengo cha
Fedha nchini Tanzania, kazi ambayo aliifanya hadi mwaka wa 2006.
Mwaka wa
2007, Sanjay alipata tena cheo kingine, wakati huu akihamishiwa Ghana,
ambapo aliongoza Kitengo cha Fedha nchini humo huku pia akisimamia
Afrika Magharibi, yaani Gambia, Cote d’ Ivoire na Sierra Leone, kazi
ambayo aliifanya hadi Mei, 2013.
Juni, 2013
Sanjay alipandishwa tena cheo na kuwa Mkuu wa Operesheni za Kifedha na
Mratibu wa Huduma za Kifedha kwa Bara la Afrika akiongoza kitengo hicho
ambacho ni sehemu ya Kitengo Kikuu cha Fedha katika nchi kumi na tano za
Afrika, akilenga kuboresha huduma za kifedha za benki hiyo zilingane na
huduma zake za kimataifa katika nchi zilizoendelea. Sanjay alifanya
kazi hii hadi alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Benki hiyo hapa Tanzania
hapo mwanzoni wa mwezi huu wa kumi na moja.
Lamin Manjang, Mkurugenzi wa benki ya Standard Chartered Kenya na Afrika Mashariki, amesema, “Nafurahi
kumkaribisha tena Sanjay nyumbani Tanzania na kwenye timu yangu ya
Afrika Mashariki kufutatia umahiri wake katika kazi mbalimbali ambazo
amezifanya katika benki yetu. Pia nafurahi kuwa sasa benki yetu nchini
Tanzania ina Mkurugenzi wake wa kwanza wa Kitanzania. Hii inaonyesha
ubora wa wafanyakazi wetu nchini Tanzania. Tunaendelea kuweka kipaumbele
kwa kuwapa wafanyakazi wetu bora nyadhifa mbalimbali za uongozi barani
Afrika ili kuweza kuboresha maendeleo katika nchi mbalimbali ambapo
tunafanya shughuli zetu za kibenki.”
Tanzania
inaendelea kupewa kipaumbele katika mipango ya benki hiyo katika bara la
Afrika na Afrika Mashariki haswa kutokana na ukuaji wake wa kiuchumi na
kuweko katika ‘Klabu ya 7%’, ambayo ni listi ya nchi ambazo uchumi wake
unakadiriwa kuendelea kukua kwa kasi zaidi katika miaka kumi ijayo.
Kufuatia kuteuliwa kwake Mkurugenzi huyo mpya wa benki ya Standard Chartered Tanzania, Sanjay Rughani alisema, “Tanzania
ina fursa nyingi sana za kibiashara na ninafurahi kurudi nyumbani
kuiongoza benki ya Standard Chartered kwenda kwenye hatua nyingine ya
kimaendeleo. Nchi yetu inaendelea kuchangia mafanikio ya Umoja wa Afrika
Mashariki kwa njia mbalimbali ikiwemo ukuaji mzuri wa uchumi. Pia
ugunduzi wa hifadhi za gesi nchini Tanzania unatarajiwa kuleta maendeleo
zaidi ya kiuchuni hapa nchini kwetu.”
Sanjay ana
shahada ya udhamili ya Kifedha na Rasilimali watu, na shahada ya Uchumi.
Pia ni mwanachama wa Chama cha Wahasibu, ACCA. Sanjay pia ni Mjumbe wa
Bodi wa benki ya Standard Chartered Uganda. Ameoa na ana watoto wawili.
No comments:
Post a Comment