Zuma
amesema kuna mambo kadha yaliyoibuliwa ambayo pia yatashughulikiwaRais
wa Afrika Kusini Jacob Zuma ameahidi kuwa vyuo vikuu havitaongeza ada ya
masomo mwaka ujao baada ya wanafunzi wa vyuo hivyo kuandamana kwa wiki
moja.
Maandamano hayo ya wanafunzi ndiyo makubwa zaidi kushuhudiwa nchini humo tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi 1994.
Wanafunzi
hao awali walikataa pendekezo la serikali la kuweka nyongeza ya ada
katika 6%, badala ya kati ya 10% na 12% iliyokuwa imependekezwa na
wasimamizi wa vyuo.
Bw Zuma alitangaza hatua hiyo huku mamia ya wanafunzi wakikusanyika nje ya afisi yake.
Kabla
yake kuhutubu kupitia runinga, polisi walikuwa wametumia mabomu ya
kutawanya waandamanaji kutawanya wanafunzi waliotaka kuingia jengo la
Union Building, lenye makao makuu ya serikali mjini Pretoria.
Jumatano, polisi walikuwa wamekabiliana na wanafunzi waliokuwa wakitaka kuingia majengo ya Bunge mjini Cape Town.
Vyuo vikuu kadha tayari vilikuwa vimefungwa kutokana na machafuko hayo.
"Tumekubaliana
kwamba karo ya vyuo vikuu haitaongezwa mwaka 2016,” Bw Zuma alisema
baada ya kukutana na wakuu wa vyuo na wawakilishi wa wanafunzi.
“Kuna
mambo ambayo yamebuliwa mkutanoni ambayo yanahitaji kufuatiliwa zaidi –
haya ni pamoja na elimu bila malipo, vyuo kujisimamia na ubaguzi wa
rangi.”
Wakati wa
maandamano hayo, vyuo vikuu vilikuwa vimejitetea na kusema vinahitaji
kuongeza karo ili kudumisha viwango vya ubora wa elimu, vikisema
vimeathirika na kupunguzwa kwa ufadhili kutoka kwa serikali.
Waandishi
wa habari wanasema maandamano hayo yameonyesha wengi wameanza
kutofurahishwa na chama tawala cha African National Congress (ANC),
kilichoingia mamlakani 1994, hasa kuhusu umaskini, ukosefu wa ajira na
ufisadi serikali.
Wengi wa wanafunzi weusi wanasema wametoka familia maskini, na nyongeza ya karo itawazuia kusoma.
Baadhi ya wanafunzi Wazungu pia walijiunga na maandamano hayo, kuonyesha uungaji mkono wao kwa wanafunzi wenzao weusi.
No comments:
Post a Comment