CCM inafuatilia kwa karibu zoezi zima la uchaguzi kote nchini. Leo, tarehe 25.10.2015, saa kumi alasiri, CCM itafanya mkutano na waandishi wa habari. Hata hivyo, kabla ya hapo, tunapenda kuelezea yafuatayo yanayojiri katika zoezi la upigaji kura linaloendelea:
1.
Utaratibu wa kupiga kura ndani ya kituo unachukua muda mrefu na
kusababisha watu kukaa muda mrefu kwenye mistari. Ni muhimu wasimamizi
na wasimamizi wasaidizi vituoni kuharakisha zoezi hili ili wananchi
wasikate tamaa na kuamua kuondoka.
2.
Wapo wapiga kura waliojiandikisha na wakapewa kadi za kupiga kura
lakini majina yao leo hayajaonekana kwenye orodha za wapiga kura
vituoni. Tunaiomba Tume ifanye kila liwezekanalo ili wananchi hawa
wapate haki yao ya kupiga kura. CCM inapenda kuona kila Mtanzania mwenye
sifa ya kupiga kura anapiga kura na changamoto zilizojitokeza katika
Tume zisiwe sababu ya watu kuikosa haki hii ya kikatiba.
3.
Kumekuwa na ripoti mbalimbali zinazosambazwa na wafuasi wa vyama vya
upinzani, nyingine zikiambatana na picha, zinazosambazwa kwenye mitandao
ya kijamii, zikituhumu wizi wa kura. Pamoja na kwamba baadhi ya ripoti
na picha hizi hazina maana yoyote, na nyingine ni za kutunga, na
zinastahili kupuuzwa, tunaiomba Tume iwe inatoa maelezo ya mara kwa mara
kuhusiana na yanayoripotiwa ili kuweka rekodi sahihi na kuwasaidia
wananchi kutopotoshwa na propaganda za kisiasa. Tunasisitiza matumizi
bora ya vyombo vya habari, ikiwemo mitandao ya kijamii, katika kipindi
hiki tete.
4.
Bado tunasisitiza uchaguzi wa amani. Hadi sasa, katika sehemu kubwa ya
nchi yetu, dalili zote zinaonyesha kwamba upigaji kura umekuwa wa
utulivu. Viongozi wa CCM wa ngazi zote wameelekezwa kuwa macho dhidi ya
hujuma kwa CCM. CCM inapenda kuzisaidia mamlaka husika kupata na
kushughulikia na taarifa za uvunjifu wa amani na uvurugaji wa taratibu
za uchaguzi.
Mwana-CCM
yoyote anayeshuhudia au kusikia mipango ya kuvunja amani na kuhujumu au
kuvuruga zoezi la uchaguzi atume ujumbe mfupi kwenda nambari 15016,
akielezea mahali alipo, tukio husika na ikiwezekana wahusika. Ujumbe huu
ni bure. CCM itazishughulikia taarifa hizo na kuzipeleka kwa mamlaka
husika.
Imetolewa na:-
January Makamba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni
No comments:
Post a Comment