Wakati kukiwa kuna taarifa zinazoenezwa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii zikisema mkuu wa Majeshi ya ulinzi nchini Jeneral Davis Mwamunyange amewekewa sumu na hali yake sasa hivi ni mbaya, huku taarifa hizo zikisema sababu ya kuwekewa sumu imetokana na masuala ya kisiasa,hatimaye Serikali imeibuka kwa mara nyingine na kukanusha taarifa hizo na kusema ni za uongo zenye nia ya kufakaranisha Taifa.
Akikanusha Uvumi huo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Afisa Habari wa Serikali ambaye pia ni mkurugenzi wa Idara ya Habari –Maelezo Assah Mwambene amesema Jeneral Mwamunyange yupo salama na anaendelea na kazi zake,akidai kuwa taarifa hizo zinalengo la kuchonginisha watanzania na jeshi na kuharibu picha ya Amani na utulivu uliopo nchini.
Mwambene amewataka Watanzania kupuuza taarifa hizo huku akiwasihi kutoingiza siasa kwenye masuala nyeti ya nchi ikiwemo jeshi,kwani jeshi ni taasisi isiyojihusisha na siasa.
Wakati huo huo pia Serikali imetolewa ufafanuzi juu ya taarifa zilizoandikwa kwenye Gazeti la Tanzania Daima ambazo zilikuwa zinaubeza uteuzi uliofanywa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete kwa kuwateua wakuu wa wilaya wapya, wakidai uteuzi huo ulikuwa ni wakulipa fadhira kwa kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi CCM.
Akifafanua uteuzi huo, Mwambene amesema watu wanaobeza uteuzi huo watakuwa hawajui sheria za nchi na kufahamu mamlaka ya Rais.
Amesema kwa mujibu wa sheria,kanuni za nchi na taratibu Rais anamamlaka ya kufanya uteuzi wakati wowote inapobidi kwa malengo ya kuboresha utendaji wa kazi serikalini.
“Serikali imesikitishwa na taarifa zilizotolewa na gazeti la Tanzania daima kuhusiana na uteuzi wa Rais,taarifa hizi ni za kichochezi na zinalenga kumchonganisha Rais na wananchi wake”amesema Mwambene.
Aidha,Mwambene amevitaka vyombo vya habari nchini kufanya utafiti na kusoma kabla ya kuandika habari na pia akaviasa kuandika habari zenye lengo la kujenga umoja na mshikamano badala ya kuandika habari zenye lengo la kuwagawa Watanzania.