Richard Mabala
Nampongeza Dr Magufuli kwa kutangazwa rais wetu mpya. Nampongeza pia kwa kutambua kwamba Watanzania wanataka mabadiliko ndiyo maana alichamasisha M4C iwe Magufuli for Change na mikono inayozunguka. Kwa njia hii bila shaka aliweza kuwavutia wengine ambayo vinginevyo wangepiga kura kwa Ukawa. Watu wanataka mabadiliko. Nampongeza pia kwa sifa yake ya kuchapa kazi na nategemea kuona hata kazi zaidi.
Lakini ni matumaini yangu kwamba kweli atasikiliza kilio cha watu. Walichangamkia opposition, na kudai mabadiliko kwa sababu. Nimewaangalia watu wengi wanajisikia wamekata tamaa leo. Hata maandamano mawili niliyoyaona ya 'kusherehekea' ushindi hayakuwa na shamrashamra ya aina yoyote.
Hivyo nakupa pole pia. Tofauti na huko nyuma una kazi kubwa ya kuwashawishi watu kwamba hata ndani ya chama chako uwezekano wa mabadiliko yapo kwa faida ya wananchi wote. Tutaanza kupima kuanzia baraza lako la mawaziri. Watakuwa ni walewale ambao wengi wao wana tuhuma nzito ya ufisadi (hata katika hela ya mboga) au utatuletea watu wa aina ya Marehemu Filikunjombe ambao wameelewa kwamba tunahitaji mwelekeo mpya. Au utaweza hata kushirikisha magwiji wa mabadiliko ili Tanzania tunufaike sana na ahadi zako na tupate dira na itikadi inayoeleweka.
Aidha tunajua una kazi kubwa sana maana mfumo wa chama chako ni mgumu sana ndiyo maana hata kama tuna imani na wewe tuna wasiwasi pia. Na mwenendo wa uchaguzi baada ya kupiga kura umetuzidishia wasiwasi. CCM kinaweza kujirudi back to its roots kama chama cha wakulima (wadogo si wawekezaji) na wafanyakazi (waajiriwa si wamiliki) na kutetea haki zao? Kinaweza kuweka kipaumbele kwenye huduma za jamii badala ya huduma za waheshimiwa? Ni chama cha wananchi kwanza au wenyenchi kwanza? Ni chama shirikishi au elekezi?
Tatu, ni mategemeo yangu kwamba utaweza kuwadhibiti watu wasio na staha. Wengine tulikereka kweli na matusi mazito, matusi very personal ambayo yalikuwa hayahusiani na siasa ya mtu, visingizo, kashfa, n.k. Tulijiuliza ndiyo itikadi ya awamu ya tano lakini tulifarijika kwamba hukuonekana ukiunga mkono matusi ya aina hiyo. Wewe sasa ni Rais wa Watanzania wote, waliokupigia kura kwa moyo mkunjufu na wasiokupigia kura kwa moyo mkunjufu na nia njema pia. Nitafurahi sana ukikomesha hii hali ya kuona mtu yeyote mwenye mawazo tofauti ni adui ili tuweze kushirikiana kujenga nchi yetu pamoja na kuondoa hii hali ya mfarakano na mfadhaiko iliyoko ndani ya jamii kwa sasa.
Nakutakia mapumziko mema kwanza baada ya kampeni kali sana kisha kazi njema na mafanikio pamoja nasi.
No comments:
Post a Comment