Msemo wa "Hapa Kazi Tu" Wamgharimu MC Wa Bongo Star Search - LEKULE

Breaking

11 Oct 2015

Msemo wa "Hapa Kazi Tu" Wamgharimu MC Wa Bongo Star Search


Zikiwa zimebaki siku 14 kabla ya kupiga kura za kumchagua rais, wabunge na madiwani, hali inaonesha kuwa watanzania wanapaswa kuchukuliwa kwa umakini mkubwa kila neno au ishara inayohusiana na siasa katika shughuli ambazo hazihusiani na siasa ili wasiharibu ‘hali ya hewa’.

Jana (Oktoba 9) katika fainali za shindano la Bongo Star Search (BSS) 2015, lililofanyika katika ukumbi wa King Solomon, Dar es Salaam, MC wa shindano hilo, Caesar Daniel alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuitaja kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’, inayotumiwa na mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli.

Mara tu baada ya kuitaja kauli mbiu hiyo katika hali ambayo haikutarajiwa, ukumbi uligeuka kuwa uwanja wa siasa kwa muda baada ya wahudhuriaji wengi wanaomuunga mkono mgombea wa Chadema, Edward Lowassa kushindwa kuvumilia na kupiga kelele za Mabadiliko na kuonesha vidole viwili juu na ishara ya ‘Mabadiliko’ inayotumiwa na vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa.

Kufuatia hali hiyo, muanzilishi wa shindano hilo ambaye pia ni ‘Chief Judge’ wa shindano hilo, alimkemea haraka MC huyo.

“Hapa umeajiliwa na BSS na sio vinginevyo, fanya kazi ya BSS …usije ukatuletea shida,” alisema Madam Ritha huku kelele zikiendelea.

Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa ndani ya ukumbi huo wa King Solomon kwa dakika chache, Master Jay alionekana kusita hata kutaja neno ‘Kazi’ kwa kuhofia kutokewa na kile kilichomkuta MC.

“Dah, ngoja nisilisema hilo . …watu wasije wakanichenjia,” alisema Master Jay.

Kama ilivyowahi kuonekana katika matamasha kadhaa, baadhi ya watu wanaomuunga mkono Magufuli walitinga ndani ya ukumbi wakiwa wamevaa fulana zenye nembo za ‘Hapa Kazi Tu’. Lakini walipoonekana wakienda kuwatuza watumbuizaji, baadhi ya watu wengine walifuata na kuonesha ishara za vidole viwili.


Shindano hilo lilimalizika kwa amani na utulivu huku wahudhuriaji wakionekana wakiwa na na furaha kubwa huku shangwe zikiongezeka baada ya mshiriki wa shindano hilo Kayumba Juma kutangazwa kuwa mshindi.

No comments: