Kingunge Atoa Maneno Mazito Kwa CCM Na Kikwete - LEKULE

Breaking

24 Oct 2015

Kingunge Atoa Maneno Mazito Kwa CCM Na Kikwete


Aliyekuwa kada mkongwe wa CCM, mzee Kingunge Ngombale Mwiru amekishukia chama chake hicho cha zamani na viongozi wake wa sasa kwa madai kuwa ‘kimechanganyikiwa’.

Akiongea leo katika mkutano wa kufunga kampeni za vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa baada ya kumnadi mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, Mzee Kingunge alidai kuwa mwenendo wa kampeni na matamko ya viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho huku akitoa mfano wa lugha kali pamoja na matusi yaliyotumika kwenye majukwaa ya kampeni.

Mzee Kingunge alimsihi Rais Jakaya Kikwete kutotumia nguvu ya dola kuzuia sauti ya wananchi walio wengi ambao alidai wameamua kumuingiza Ikulu Edward Lowassa. 
 
Alimshauri Rais Kikwete kujipanga kukabidhi kwa amani madaraka kwa mgombea urais atakayeshinda ambaye anaamini ni Lowassa kama alivyokabidhiwa nafasi hiyo kutoka kwa rais wa serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

“CCM imekuwa na utaratibu wa kukabidhi madaraka kwa amani, Mwinyi alimkabidhi madaraka Mkapa kwa amani, Mkapa naye alimkabidhi yeye kwa amani, sasa nay eye afanye hivyo.”

Alisema kuwa kuna dalili kwamba Rais Kikwete anataka kuyapinga matakwa ya wananchi walio wengi kwa kuchakachua matokeo na kufanya hujuma kwenye mchakato wa uchaguzi kwa kutumia nguvu ya dola hivyo akamsihi aache kwa kuwa ataliingiza taifa kwenye machafuko.

Mwanasiasa huyo mkongwe alionesha kusikitishwa na kauli zilizotolewa na Rais Kikwete kwa kuwachukulia wapinzani kama ‘adui’ na kwamba wapigwe. Alisema mchezo wa siasa ni ushindani na sio uadui.

Mzee Kingunge aliwakumbusha wananchi kuwa mwalimu Nyerere aliwahi kumtangaza adui wa Tanzania anayefaa kupigwa kuwa ni Idd Amin na sio wananchi wa Tanzania.

“Nyerere alikaa na wazee wa Dar es Salaam, akasema tumpige adui Idd Amin, akatangaza apigwe na kweli tukampiga,” alisema na kudai kuwa alishangaa kumsikia Rais Kikwete akitangaza kuwa wapinzania ni maadui na wapigwe.


Mzee Kingunge alitangaza kuitosa CCM na kuhamia upande wa Mabadiliko akidai kuwa viongozi wa sasa wa CCM wamepoteza dira na chama hicho kimekosa muelekeo na kimekata pumzi, hivyo hakiwezi tena kuwafikisha watanzania kwenye kilele cha mafanikio.

No comments: