Kilimanjaro Yavunja Rekodi ......Majimbo 7 kati ya 9 Yanyakuliwa na Wapinzani - LEKULE

Breaking

27 Oct 2015

Kilimanjaro Yavunja Rekodi ......Majimbo 7 kati ya 9 Yanyakuliwa na Wapinzani



Mkoa wa Kilimanjaro, umevunja rekodi ya uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 baada ya upinzani kunyakua majimbo saba kati ya majimbo tisa.

Mwaka 1995, upinzani ulinyakua majimbo sita ya Hai,Siha,Rombo, Moshi Vijijini, Moshi mjini na Vunjo na kuiachia CCM majimbo ya Mwanga, Same Mashariki na Magharibi.

Lakini kati ya mwaka 2000 na 2010, CCM ikafanikiwa kukomboa majimbo ya Siha na Moshi Vijijini lakini katika uchaguzi wa 2015, majimbo hayo yameangukia tena mikononi mwa upinzani.

Mbali na majimbo hayo, katika historia ya vyama vingi, safari hii upinzani umejipenyeza katika jimbo la Same Mashariki ambalo lilikuwa ngome ya CCM na kuwa miongoni mwa majimbo ya upinzani.

Majimbo ambayo sasa yanashikiliwa na upinzani ni Hai,Siha,Moshi Vijijini,Moshi Mjini, Vunjo, Rombo na Same Mashariki huku CCM ikibaki na majimbo mawili ya Mwanga na Same Magharibi.

Katika tukio lingine, aliyekuwa mgombea Ubunge Jimbo la Moshi mjini kwa tiketi ya CCM, Davis Mosha, amempongeza mpinzani wake, Jaffar Michael wa Chadema kwa kupata ushindi wa kishindo.

Michael aliibuka na ushindi wa kura 51,646 dhidi ya kura 26,920 alizopata Mosha, na hivyo kumfanya Michael ambaye ni Meya wa mji wa Moshi aliyemaliza muda wake kutangazwa mshindi.

Juzi saa 4:26 usiku, Mosha alimtumia Michael ujumbe mfupi wa maandishi (SMS), akimpongeza kwa ushindi wa kishindo, kitendo ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya jimbo hilo.

“Mhe Japhary Michael nachukua nafasi hii kukupongeza kwa ushindi wa kishindo katika nafasi ya Ubunge Jimbo la Moshi,”alisema Mosha ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara matajiri nchini.

“Najua kuna sehemu tulikwaruzana ama kuhitilafiana kwa maneno. Hiyo ilikuwa siasa sio ugomvi binafsi nisamehe na Mungu akubariki. Kama utahitaji msaada wowote tafadhali tuwasiliane,”alisema.

No comments: