Mgombea Urais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za vifo vya Mbunge wa Jimbo la Ludewa, mkoani Njombe Ndugu Deo Filikunjombe Haule, Kepteni William Silaa pamoja na abiria wengine wawili ambao wameaga dunia Alhamisi, Oktoba 15, 2015 kwa ajali ya helkopta iliyotokea katika eneo la Hifadhi ya Selous mkoani Morogoro.
Katika
salamu za rambirambi ambazo amewatumia Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Njombe
Ndugu Deo Sanga, na Meya wa Manispaa ya Ilala Mstahiki Jerry Silaa,
Dkt. Magufuli amesema: “Kwa hakika, nimeshtushwa na kuhuzunishwa mno
na taarifa za vifo vya Ndugu Filikunjombe na Ndugu Silaa ambavyo
nimetaarifiwa kuwa vimetokea kwa ajali ya helkopta aliyokuwa akiitumia
Ndugu Filikunjombe kwa Kampeni zake za Ubunge katika jimbo hilo la
Ludewa.
Katika salamu zake hizo za rambirambi Dkt. Magufuli ameongeza kuwa: “Kama
unavyojua, namfahamu vizuri Ndugu Filikunjombe. Alikuwa Mbunge
mwenzangu katika Bunge lililomaliza muda wake mwaka huu. Nimefanya kazi
naye kwa karibu na kwa miaka mitano ndani ya bunge letu.
"Alikuwa
mtumishi hodari, mtumishi mwaminifu na mwadilifu kwa wananchi wa
Tanzania, na hasa wananchi wa Jimbo la Ludewa, ambao aliwawakilisha kwa
miaka mitano iliyopita akiwa Mbunge wao. Hata nilipofanya ziara ya
kampeni katika jimbo lake la Ludewa mwezi uliopita nililala nyumbani
kwake, hiyo inaonesha nilivyokuwa karibu naye. Tutakosa utumishi wake
mahiri sana.”
Salamu zake za rambirambi kwa Mstahiki Meya Jerry Silaa, Dkt. Magufuli amesema: “Nimesikitishwa
sana na taarifa ya kifo cha Baba yako Kepteni William Silaa, kwani ni
tukio lisilozoeleka. Ni jana tu nimeshiriki nawe katika kampeni kwa
ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 katika jimbo unalogombea Ubunge, jimbo la
Ukonga, naungana nawe katika kipindi hiki kigumu cha msiba mkubwa.
Nakupa pole wewe binafsi, familia yenu, ndugu, jamaa na marafiki wote”.
Aidha aliongeza “Nakutumia
wewe Ndugu Sanga, Mwenyekiti wetu wa CCM mkoa wa Njombe salamu za
rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo cha Ndugu Filikunjombe
na abiria hao wengine. Aidha, kupitia kwako namtumia rambirambi nyingi
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anna
Semamba Makinda na Wabunge wote kwa kuondokewa na mwenzao.”
Dkt. Magufuli ameongeza “Nakuomba
pia unifikishe salamu zangu za rambirambi kwa wananchi wa Jimbo na
Wilaya ya Ludewa ambao wamepoteza Mbunge wao aliyewatumikia kwa ustadi
mkubwa kwa kipindi chote. Aliwawakilisha vizuri na kujali sana maslahi
yao.
“Ametuma pia salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Ndugu Filikunjombe kwa kuondokewa na mhimili wa familia na rafiki yao mpenzi.
“Ametuma pia salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Ndugu Filikunjombe kwa kuondokewa na mhimili wa familia na rafiki yao mpenzi.
Amewaombea kwa Mwenyezi Mungu awape subira na nguvu ya uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi. "Pia naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu aziweke pema peponi roho ya Deo Filikunjombe Haule”. Amen.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
CCM Ofisi Ndogo, Lumumba
DAR ES SALAAM.
16 Oktoba, 2015
No comments:
Post a Comment