38 kizimbani kwa kufanya vurugu Mbagala wakati wa uchaguzi - LEKULE

Breaking

30 Oct 2015

38 kizimbani kwa kufanya vurugu Mbagala wakati wa uchaguzi


 Watu 38 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi  K isutu wakikabiliwa na mashtaka manne likiwamo la kutoa vitisho vya shinikizo kwa msimamizi  atoe matokeo ya Ubunge ya Mbagala bila ya kufuata utaratibu na  kuchoma maboxi 11 ya kupigia kura  na karatasi za kupigia kura zenye thamani ya Sh 2.2 milioni.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali  Mwandamizi, Joseph Maugo akishirikiana na Wakili wa Serikali, Genis Tesha  walidai mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru kuwa Oktoba 27,2015 katika eneo la Mbagala Majimatitu  kwa nia ya uhalifu walifanya mkusanyiko na kuleta hisia ya uvunjifu wa amani.

Alidai kuwa washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 74 na 75cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho 2002.

Katika shtaka la pili, wanadaiwa kuwa Oktoba 27,2015  huko Mbagala Majimatitu, kinyume  na kifungu cha 79 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho 2002 washtakiwa  hao walikusanyika  na kufanya waliyodhamiria kuyafanya na kusababisha uvunjifu wa amani na kuleta hofu katika jamii.

Maugo katika shtaka la tatu, washtakiwa hao kwa pamoja kinyume na kifungu cha 326(1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho 2002 walichoma maboxi 11 ya kupigia kura na karatasi za kupigia kura zenye thamani ya Sh 2.2 milioni mali ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Wakili huyo wa Serikali katika shtaka la nne  alidai kuwa siku hiyo ya tukio washtakiwa  hao, walitoa vitisho na kumshinikiza msimamizi wa uchaguzi  atoe matokeo ya ubunge ya Mbagala bila ya kufuata utaratibu wa sheria.

Washtakiwa hao wanadaiwa kufanya kosa hilo kinyume na kifungu 89B (1)(b) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho 2002.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana  na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi  wa kesi bado haujakamilika.

Hakimu Mchauru alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao wanaaminika ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh 2 milioni hata hivyo washtakiwa hao walipelekwa rumande baada ya kushindwa kukamilisha masharti hayo.

Kesi imeahirishwa hadi Novemba 12, 2015  kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

No comments: