Zantel yalisaidia jiji la Tanga vifaa vya usafi - LEKULE

Breaking

7 Sept 2015

Zantel yalisaidia jiji la Tanga vifaa vya usafi


1
Meneja Mshauri wa Zantel, Charles Jutta akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi msaada wa vifaa vya usafi kwa  mkoa wa Tanga, kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mheshimiwa Magalula Said Magalula.
2
Mkuu wa Wilaya ya Tanga Abdula Lutavi akiteta jambo na Meneja Mshauri wa Zantel, Charles Jutta (Kushoto) mara baada ya makabidhiano ya vifaa vya usafi baina ya Zantel na jiji la Tanga anayeshudia katikati ni meneja mauzo wa Zantel Tanga.
3
Mkuu wa mkoa wa Tanga Magalula Said Magalula (kulia) akishiriki zoezi la usafi katika eneo la Mwembe Mawazo jijini Tanga muda mfupi baada ya kupokea vifaa vya kufanyia usafi kutoka kampuni ya Zantel kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mheshimiwa Abdula Lutavi.
Kampuni ya simu za mkononi ya Zantel jana imetoa msaada wa vifaa vya usafi kwa halmashauri ya jiji la Tanga venye lengo la kusaidia shughuli za usafi katika jiji hilo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Mahusiano ya Serikali wa Zantel, Bwana Charles Jutta alisema msaada huo ni sehemu ya juhudi za kampuni yake kuziunga mkono jitihada zinazofanywa na halmashauri ya jiji la Tanga katika kutunza na kuweka mazingira safi na salama kwa wakazi wake.
‘Kampuni ya Zantel inaamini katika kushirikiana na serikali ili kuhakikisha jamii yetu inaishi katika mazingira safi na salama, na vifaa hivi tulivyotoa leo vitasaidia swala la usafi jijini hapa kama sehemu ya wajibu wetu kwa jamii’ alisema Jutta.
Akiongelea sababu za kampuni yake kushirikiana na manispaa ya jiji la Tanga, Jutta alisema kuwa imani ya kampuni ya Zantel ni kuhakikisha mazingira yanatunzwa ili kuhakikisha jamii inakuwa na afya bora na ustawi.
‘Mazingira ndio hutoa taswira ya jamii husika, na sisi kama Zantel tunaamini jamii isiyoishi kwenye usafi sio tu iko katika hatari ya kupata magonjwa, bali pia haitaweza kustawi sawasawa’ alisema Jutta.
Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Magalula Saidi Magalula alisema msaada huo unaenda sambamba na jitihada za ofisi yake katika kushughulikia kuboresha usafi wa mkoa wake.
‘Kwanza niwashukuru Zantel kwa kutambua juhudi zetu na nitumie fursa hii kuzitaka kampuni zingine kuiga mfano huu. La pili niwahakikishie kuwa tumepata vifaa hivi wakati mwafaka kwani taarifa za mlipuko wa kipindupindu zipo Dar es Salaam, zipo Morogoro na mikoa hii ina mwingiliano mkubwa na sisi kwa hiyo vifaa hivi iwe changamoto kwa sisi kuongeza kasi ya kufanya usafi zaidi, kila jumamosi wananchi tuendelee kushiriki katika shughuli za kufanya usafi’ alisema Magalula
Mheshimiwa Magalula ameishukuru kampeni ya Zantel kwa msaada huo huku akitaka makampuni mengine nayo yajitokeze kuunga mkono juhudi za manispaa yake.
‘Jiji letu limekuwa likikipa kipaumbele kikubwa swala la usafi, na leo tunaishukuru kampuni ya Zantel kwa msaada huu, ambao tuna hakika utasaidia katika kupeleka kasi swala la usafi hapa Tanga’ alisema Mheshimiwa Magalula.

No comments: