WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema uongezaji virutubisho kwenye vyakula umeibua
mguso mpya na kuleta mlipuko baina ya sekta binafsi na sekta za umma
(PPP) ambazo zinasimamia masuala ya afya kwa kiwango kikubwa.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema kazi kubwa zaidi inabidi ifanyike ili elimu
ya kutosha iweze kufikishwa kwa mabilioni ya watu ambao milo yao ya kila
siku haina virutubisho vya kutosha.
Ametoa
kauli hiyo jana usiku (Jumatano, Septemba 9, 2015) wakati akizungumza na
washiriki zaidi ya 400 kutoka nchi 30 wanaohudhuria mkutano wa kwanza
wa kimataifa wa urutubishaji vyakula ulioanza jana jijini Arusha.
Mkutano huo utamalizika kesho, Septemba 11, 2015.
“Bila
kuwa na sera zinazoeleweka na jamii, bila kuwekeza zaidi na bila kuwa na
timu ya wataalamu waliobobea kwenye masuala la chakula, tuko hatarini
kupoteza kasi tuliyoanza nayo na tunaweza tusifanikiwe kutimiza malengo
tuliyotarajia,” alionya Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu ambaye alifungua mkutano huo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete,
alisema urutubishaji wa vyakula unaohimizwa ni uongezaji wa madini na
vitamini kwenye vyakula vinavyosindikwa viwe vya mafuta au nafaka ili
kupambana na udumavu na utapiamlo. Alisema hivi sasa virutubisho
vinavyoongezwa kwenye vyakula ni pamoja na madini ya chuma, zinc,
vitamini A na vitamini B12.
“Uongezaji
wa virutubisho unaendana na kampeni ya siku 1,000 za mwanzo wa maisha
ya mtoto (1,000 days of a child’s life) ambayo inaendeshwa na Serikali
yetu kwa kuzingatia kuwa faida zake zinagusa ukuaji na afya ya mtoto,
ukuaji wa ubongo wa mtoto, ujenzi wa kinga imara za mwili, uelewa mkubwa
unaomwezesha mtoto kufanya vizuri masomoni na uhakika wa maisha marefu
ambao unachangia ukuaji wa uchumi na pato la Taifa,” alisema.
Kuhusu
juhudi za Serikali, Waziri Mkuu alisema Serikali kupitia Mamlaka ya
Serikali za Mitaa imelenga kupanua huduma za urutubishaji wa vyakula
vijijini ambako asilimia 70 ya Watanzania wanaishi. “Mifumo imewekwa ili
kusaidia wenye viwanda vya kusindika nafaka na mafuta waweze kuongeza
virutubishi hivyo,” alisema.
Alisema
Tanzania ilianza kampeni za kuongeza virutubisho kama vile madini joto
(iodine) kwenye chumvi tangu miaka ya 90 na matokeo yake hivi sasa
hakuna wagonjwa wa goitre kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Hivi
sasa kila kaya inatumia chumvi yenye madinijoto na asilimia zaidi ya 80
ya kaya zinatumia chumvi ya aina hii. Matokeo yake ni kupungua kwa
ugonjwa wa goitre na kufikia chini ya asilimia tano kwa watoto wenye
umri kati ya miaka 6-12 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kwenye miaka
ya 1980,” alifafanua.
Kwa
upande wake, Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) wa Masuala ya Kupambana na
Njaa, Mfalme Letsie III wa Lesotho alisema suala la kurutubisha vyakula
lisiachwe kuwa la Serikali peke yake bali linahitaji nguvu ya pamoja
kutoka kwa wadau mbalimbali na hata ikibidi Serikali zote za Bara la
Afrika.
“Vyanzo
vya upungufu wa virutubisho na utapiamlo na vingi na vina njia
mbalimbali za kukabiliana nazo. Lakini hapa nataka nisisitize kwamba,
tunahitaji utashi wa kisiasa kutoka kwa wakuu wa nchi zote duniani na
siyo kwa bara la Afrika peke yake ili suala hili liweze kufanikiwa,”
alisema.
“Nikiwa
Balozi wa AU wa kupambana na njaa, ninazitaka nchi zote na Serikali
zilizoko madarakani ziweke sheria mahsusi au sera za kitaifa ambazo
zitaweka bayana suala la urutubishaji wa vyakula kama njia ya kupambana
na njaa na pia kumaliza kabisa tatizo la upungufu wa virutubisho vya
kutosha kwenye milo ya kila siku ya watu wetu,” alisema huku
akishangiliwa.
Naye
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kebwe S. Kebwe alisema Serikali imelenga
kuajiri maafisa lishe kwenye Halmashauri za Wilaya 157 ili kukabiliana
na tatizo la upungufu wa viinilishe kwenye vyakula.
Alisema
kati ya mwaka 2010 na 2013 Serikali imeongeza kiasi cha fedha kutoka sh.
bilioni 19/- hadi sh. bilioni 33/- ili zisaidie kusimamia masuala ya
lishe na urutubishaji wa vyakula.
Mapema,
akitoa taarifa kuhusu Mkutano huo wa Kwanza wa Kimataifa, Mkurugenzi
Mtendaji wa Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN), Dk. Marc Van
Ameringen alisema mkutano huo unawajumuisha watendaji kutoka serikalini,
taasisi binafsi, vyuo vikuu na taasisi za utafiti ili kwa pamoja waje
na suluhisho la kudumu juu ya urutubishaji vya vyakula kama njia ya
kupambana na njaa na udumavu.
Alisema
wana maeneo matano ambayo wameyalenga yakiwemo uboreshaji wa sheria;
utoaji wa elimu zaidi na ushawishi kwa jamii; haja ya kupata uwekezaji
zaidi kwenye eneo hilo; haja ya kupata msukumo kutoka Serikali za nchi
mbalimbali na kuhakikisha kuwa urutubishaji wa vyakula unaingizwa kwenye
mikakati ya kitaifa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, SEPTEMBA 10, 2015.
No comments:
Post a Comment